Kutambua Ishara za Mkazo wa Akili Katika Mtoto Wako
“Mara nyingi hisia za mkazo huwa zina sababu: Kwa kawaida hizo huwa matokeo ya matukio au hali fulani.” —Dakt. Lilian G. Katz.
RUBANI anaweza kuonaje anakoenda akiendesha ndege kwenye usiku wenye giza na ukungu? Anapoondoka na anapotua chini anategemea ishara. Zaidi ya vyombo mia moja viko kwenye viendeshaji vya ndege katika chumba cha rubani wa ndege kubwa, kila kimoja chavyo kikitoa taarifa na kumtahadharisha rubani juu ya matatizo yawezayo kutokea.
Kukua katika ulimwengu wetu wenye kujaa mikazo ya akili ni kama kusafiri angani kukiwa na dhoruba. Wazazi wanaweza kuongozaje mwendo ulio shwari kuanzia utoto hadi awe mtu mzima? Kwa kuwa watoto wengi huwa hawaongei juu ya mikazo yao ya akili, wazazi wanapaswa kujifunza kutambua dalili.
Mwili “Waongea”
Mkazo wa akili wa mtoto kwa kawaida huwasilishwa kwa mwili. Matatizo ya kiakili, kutia ndani matatizo ya tumbo, kuumwa kichwa, unyong’onyevu, matatizo ya kulala, na matatizo ya kutoa uchafu kwa mwili, huenda zikawa dalili za kuonyesha kuna kasoro.a
Kupoteza uwezo wa kusikia kwa Sharon kulikuwa upeo wa kipindi cha upweke mkubwa. Amy alipoenda shuleni, maumivu yake ya tumbo yalisababishwa na woga wa kutenganishwa na mama yake. Ukabidhi wa tumbo wa John ulitokana na msongo wa kuona mapigano ya jeuri ya wazazi wake.
Kutendwa vibaya kingono kulikuwa na matokeo mabaya ya kimwili kwa Ashley mwenye umri wa miaka 10. “Nakumbuka sikwenda shuleni kwa juma moja [baada ya kunajisiwa] kwa sababu nilikuwa mgonjwa,” akumbuka. Kitabu When Your Child Has Been Molested chaeleza: “Mzigo wa kutendwa vibaya kingono waweza kumkaza mtoto hata akose afya.” Miongoni mwa dalili za tamauko baya jinsi hiyo ni vidonda, maumivu wakati wa choo, matatizo ya tumbo ya mara kwa mara, kuumwa kichwa, na maumivu ya mfupa au misuli ambayo hayana sababu hasa.
Ugonjwa unapoonekana kuwa wa matatizo ya akili, wazazi wanapaswa kuchukua dalili kwa uzito. “Hata kama mtoto anasingizia au la,” ase-ma Dakt. Alice S. Honig. “Kilicho cha maana ni chanzo cha tatizo.”
Tabia Hutoa Dalili Zilizo Wazi Kuliko Yanayosemwa
Badiliko la ghafula katika tabia mara nyingi lahitaji msaada. Kitabu Giving Sorrow Words chaandika: “Mwanafunzi mzuri aanzapo kuanguka mtihani, jambo hilo lahitaji kuangaliwa, na jambo hilo liangaliwe pia kwa mtoto ambaye alikuwa mwenye matata anzaapo kugeuka na kuwa na tabia nzuri.”
Timmy mwenye umri wa miaka saba alianza kudanganya-danganya kwa ghafula mama yake alipojiingiza kabisa katika kazi yake. Tabia ya kijeuri ya ghafula ya Adam mwenye umri wa miaka sita ilisababishwa na hisia za kuwa wa chini shuleni. Kurudia kwa Carl mwenye umri wa miaka saba kwa tatizo la kukojoa kitandani kulionyesha tamaa yake ya kupata upendeleo wa wazazi, ambao sasa ulionekana umegeuziwa dada yake mchanga.
Tabia ya kujidhuru mwenyewe ni yenye kusumbua hasa. Aksidenti za mara nyingi za Sara mwenye umri wa miaka kumi na miwili hazingesemwa kuwa ni udhaifu. Tangu talaka ya wazazi wake, kujiumiza mwenyewe kulikuwa njia ambayo alitumia bila kujua ili kunasa shauku ya baba yake ambaye alikuwa mbali. Yawe ni majeraha madogo au yenye uzito kama kujaribu kujiua, kujidhuru kindani kwa tabia ya kujiangamiza ni dalili ya mkazo mwingi wa akili.
Kuongea Kutoka Moyoni
“Kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake,” akasema Yesu Kristo. (Mathayo 12:34) Moyo uliojawa na hisia mbaya kwa kawaida huonyeshwa na asemayo mtoto.
“Watoto wanaokuja nyumbani wakisema ‘Hakuna mtu anipendaye’ kwa kweli wanakuambia kwamba hawajipendi wenyewe,” asema Dakt. Loraine Stern. Jambo hilo laweza pia kuwa sawa na kujigamba. Ingawaje kujigamba kunaonekana kuonyesha kinyume cha kujishusha, majivuno kuhusu matimizo ya kweli au ya kuwaziwa huenda yakawa jitihada ya kushinda hisia nyingi za kujiona kuwa wa hali ya chini.
Ni kweli, watoto wote huwa wagonjwa, hujiendesha isivyofaa wakati mmoja mmoja, na pindi fulani hujisikia wametamaushwa. Lakini matatizo kama hayo yakiwa ya kawaida na hakuna sababisho hasa, wazazi wanapaswa kuangalia maana ya ishara hizo.
Baada ya kuchunguza tabia ya utoto ya matineja sita waliokuwa wakichochea mashambulizi yenye jeuri, Mary Susan Miller aliandika: “Ishara zote zilikuwako. Wavulana hao walikuwa wakionyesha ishara hizo katika mwendo wa maisha yao kwa miaka mingi, lakini hakuna mtu aliyejali. Watu wazima waliona, lakini hawakujali.”
Sasa kuliko wakati mwingine wowote, wazazi wanapaswa kuwa chonjo kutambua dalili za mkazo wa akili wa utotoni na kuchukua hatua.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Je! ni Mkazo wa Akili Katika Tumbo la Uzazi?
Hata kijusu chaweza kutambua mkazo wa akili, woga, na hangaiko ambalo mama yake anawasilisha kupitia badiliko la kemikali katika mkondo wa damu. “Kijusu kinachokua kinahisi kila mpigo wa mkazo ambao mwanamke mwenye mimba anahisi,” aandika Linda Bird Francke katika kitabu Growing Up Divorced. “Ingawa mfumo wa neva wa kijusu na wa mwanamke haujaunganishwa moja kwa moja, kuna uhusiano wa njia moja kati yao wawili ambao hauwezi kukatwa.” Hilo laweza kueleza kwa nini, kulingana na gazeti Time, vitoto vinavyokadiriwa kuwa asilimia 30 vyenye umri wa miezi 18 na vichanga zaidi hupatwa na magumu ya mkazo wa akili kuanzia unyamavu hadi matatizo ya mahangaiko yasiyotokana na chanzo hususa. “Watoto wanaozaliwa na wanawake wasio na furaha, wenye mshuko wa moyo mara nyingi wenyewe huwa wasio na furaha na walioshuka moyo pia,” Francke amalizia.
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
Mtoto Anapojaribu Kujiua
“Ni nini kingetendeka ikiwa ningelala kwa miaka mia moja?” Lettie alimwuliza baba yake. Alifikiri hilo ni swali la kitoto. Lakini Lettie hakuwa anacheza. Baada ya siku kadhaa alilazwa hospitalini kwa sababu ya kumeza tembe za kulala za chupa nzima.
Wewe unapaswa kufanya nini kama mtoto wako anafikiria juu ya kujiua au akijaribu kujiua? “Tafuta msaada unaofaa haraka,” chasihi kitabu Depression—What Families Should Know. “Kutibu wanaoelekea kujiua si kazi ya wale wasio stadi sana, hata wale wanaojali sana mtu aliyeshuka moyo. Huenda ukafikiri umesadikisha mshiriki wa familia yako asijiue wakati anaponyamaza tu na kuweka hisia zote ndani mpaka zitoke kwa njia yenye kusikitisha sana.”
Kukiwa na kutendewa vizuri kuna matumaini kwa mtoto anayejaribu kujiua. “Watu walio wengi ambao hujaribu kujiua kwa kweli huwa hawataki kujiua wenyewe,” kitabu kilichonukuliwa juu chasema. “Wao hutaka tu kuacha kuumia. Majaribio yao huwa ni kilio cha kutaka msaada.” Katika kundi la Kikristo, wazazi ambao wanashindwa kushughulikia mielekeo ya kujiua wanaweza kupata tegemezo la upendo na mashauri mazuri ya Kimaandiko kutoka kwa wazee.
[Maelezo ya Chini]
a Tofauti na tatizo la kushuka moyo sana, ambalo hutia ndani magonjwa ya mawazio tu, ugonjwa wa mkazo wa akili ni halisi. Hata hivyo, sababisho lake, ni la kihisia-moyo badala ya kimwili.