Kuacha Kuwa Nyumba za Akiba Kuwa Stediamu
Na mleta habari za Amkeni! katika Hispania
KUANZIA kilele cha kilima hadi pwani ya bahari, sehemu yenye kuonekana sana ya mtandao wa eneo la Galicia, kaskazini-magharibi mwa Hispania, ni ile hórreo. Ni viboma vichache vya makao ya watu katika Galicia ambavyo havinayo. Hórreo, ambayo kwa kawaida huwa imefanyizwa kwa jiwe granaiti au mbao na kupambwa kwa msalaba nyakati zote, ingeweza kwa urahisi kudhaniwa kimakosa kuwa ni ziara la maziko ya familia.
Hata hivyo, kusudi layo ni la kimwili zaidi. Ni nyumba ya akiba, au ghala, ambayo hutumiwa kuhifadhi mahindi, viazi, na mazao mengine yakiwa makavu wakati wa ile miezi ya kipupwe yenye unyevu. Nguzo zilizo kama uyoga ambazo hukaliwa nayo hutumika kuwazidi panya maarifa, ambao wangependa sana kufanya mavuno yawe mlo wao.
Lakini miaka 30 iliyopita, hórreo fulani katika kijiji kidogo cha Xeoane iliondolewa msalaba wayo. (Angalia foto iliyo juu.) Hii nyumba ndogo ya akiba—ya meta 10 za mraba—ilitumika kuwa mahali pa mikutano pa Mashahidi wa Yehova katika Galicia. Watu wengi kufikia 23 walikuwa wakisongamana ndani ya nafasi hiyo ndogo sana, wakiwasili na kuondoka wakati wa giza ili kuepuka kukamatwa wakati wa utawala wa kimabavu wa Franco.
Sasa, karibu miongono miwili imepita tangu Mashahidi wa Yehova walipopewa uhuru wa kidini katika Hispania. Hivi majuzi, Mashahidi katika Galicia walifanya mkusanyiko wa wilaya wao wa kila mwaka. Gazeti la jimbo, La Voz de Galicia, lilisema hivi:
“Kama vile Wakristo wa mapema walivyokutana katika mapango ya kuzikia wafu ili wafanye sherehe zao, zilizokatazwa na wenye mamlaka, ndivyo Mashahidi wa Yehova wa kwanza wa Galicia, huko nyuma katika miaka ya ’50, walivyotumia hórreo. . . . Sasa kuna [Mashahidi] 4,000 katika ile mikoa minne ya Galicia. . . . Wakati huu, mahali pao pa mikutano—stediamu ya michezo ya manispaa—pana nafasi kubwa zaidi.” Kwa kweli hatua kubwa zimepigwa tangu ile hórreo ya hali ya chini! Na sasa, kotekote katika Hispania, kuna Mashahidi kama 80,000 katika makundi zaidi ya elfu moja!
[Picha katika ukurasa wa 14]
Mkusanyiko mkubwa katika stediamu ya mpira wa miguu katika Barcelona