Ukurasa wa Pili
Katika Juni 1988 Kanisa Katoliki la Kiroma lilipata mtengano, au mgawanyiko, walo wa kwanza katika muda wa zaidi ya karne moja. Askofu mkuu mfuata mapokeo Lefebvre aliondoshwa katika ushirika. Mwaka mmoja baada ya mwachano huo, yule kasisi mwasi alidai kwamba kulikuwa na ongezeko la asilimia 10 kufika 20 katika idadi ya wafuasi wake.
Kwa wakati huo, mamia ya wanatheolojia Wakatoliki walitia sahihi ujulisho rasmi wenye kuteta juu ya kile ambacho wanakiona kuwa ni utumizi mbaya wa papa wa mamlaka katika kuweka rasmi maaskofu wapya na katika mambo ya mafundisho, kama vile kudhibiti uzazi.
Kisiasa, Wakatoliki wamegawanyika kwa kina kirefu, wengine wakishikilia desturi za zamani kupita kiasi, wengine wakitetea mageuzo ya kijamii na hata mapinduzi ya kutumia silaha. Mkatoliki wa wastani huenda akavurugwa na migawanyiko hii.