Alama Nyekundu Juu ya Theluji—Ikiwa si Masika ya Mapema
“UKISHAONWA, hausahauliki kamwe; rangi nyekundu-nyangavu inashtua katika mwanga mdogo wa jua katika mazingira meusi ya sakafu ya msitu.” Ndivyo kilivyosema kitabu cha Audubon Society, kiitwacho Western Forests, juu ya mmea wa thelujini, Sarcodes Sanguinea. Unashtua hata zaidi unapoonwa mapema kidogo, huo unapojisukumiza kutoka kwa vipande-vipande vya theluji. “Ni mmea usio wa kawaida ulio thabiti, mnene, wenye rangi nyekundu-nyangavu kabisa, vingujani vikipishana kwenye shina la chini na kujikunja kati ya vishada vya maua juu,” yaeleza Western Forests. Unapatikana kwenye milima ya misitu ya konifera ya California na Oregon kusini.
Mmea wa thelujini ni mmoja kati ya saprofiti, kikundi kisicho na mata ya kijani, bila klorofili, na hivyo hakifanyizi usanidimwanga. Saprofiti hutegemea mimea iliyokufa au inayooza au mata ya wanyama. Uyoga wa mwavuli, uyoga vumbi, na aina nyingine za uyoga na bakteria ni saprofiti, lakini pia katika kikundi hiki kuna mimea inayotoa maua. Mmea wa thelujini ni mmojawapo.
Baadhi ya mimea mikubwa ya saprofiti hutegemea kabisa uyoga fulani kuwa chakula, ambao huitwa uhusiano wa maikohizoli—jumla yenye kunufaisha pande zote ya uyoga (myco) na mfumo wa mizizi (rhiza) wa mimea mikubwa zaidi. Katika hali hizo, mizizi ya saprofiti kwa kawaida hukosa vinywele vya mizizi. Uyoga huchukua kazi ya kufyonza madini na unyevu. The Encyclopedia Americana (Chapa ya Kimataifa) husema: “Umaana wa maikohizoli kuwa ushirika wa kufaana uligunduliwa mwishoni mwa karne ya 19 na mbotania Mjerumani Albert Bernard Frank kama tokeo la uchunguzi wa ukuzi wa ukungu kwa ajili ya serikali ya Prussia.”