Gari la Abiria la Angani Lenye Kutokeza la Utah
“GARI la Abiria la Angani Lenye Kuinuka Zaidi Ulimwenguni.” Hivyo ndivyo gari hilo la juu linavyotangazwa kibiashara katika Bridal Veil Falls (Maporomoko ya Maji ya Bridal Veil) katika Bonde la Provo, Utah, U.S.A. Nilijiuliza, ‘Je! hiyo inaweza kuwa kweli?’ Ninakumbuka nikichukua gari la kwenda juu katika Catalonia, Uhispania, karibu miaka 15 iliyopita nikienda kuzuru milima ya Montserrat, na gari hilo lilionekana kuwa lenye kuinuka zaidi nikilinganisha. Basi kwa nini wanasema kwamba gari lenye kuinuka zaidi lipo hapa katika Bridal Veil Falls? Kwa sababu linainuka meta 374 kwenye nyuzi za chuma zenye umbali wa meta 534—mwinuko wa wastani wa digrii 45 kutoka chini. Behewa lenye kubeba watu sita linapofika karibu na kituo cha milimani, kwenye urefu wa juu wa meta 1,900, mwendo wa mwinuko huwa digrii 62!
Mambo hayo yote ni ya kiufundi. Safari yenyewe, kwenye behewa la watu sita, inapendeza tunapoinuka kutoka kwenye barabara kuu na kupita Bridal Veil Falls upande wa kushoto. Tunapanda kwa mwendo wa wastani wa kilometa 8 kwa saa. Milima yenye mawe-mawe yatuzunguka—Mlima Timpanogos ukiinuka kufikia meta 3,600 ukiwa nyuma yetu na ule tunaopanda, Mlima Cascade, ukiwa mbele. Maporomoko hayo yana maanguko mawili ya maji yanayoporomoka kwa zaidi ya meta 180 kabla ya kujiunga na Mto Provo. Baadhi ya maji hayo yanachukuliwa kwa bomba hadi kwenye kituo cha nguvu ya umeme kilichopo umbali wa kilometa 6.
Njia hiyo ya gari iliyotengenezwa na Waswisi ilifunguliwa katika 1962 na imebeba watu zaidi ya milioni 1.5 bila hata aksidenti moja mbaya. Kama unahofu kusafiri katika njia hiyo ya juu, broshua moja inasema hivi: “Njia hizo za gari za kwenda juu kama ilivyo na hiyo, ndizo njia salama zaidi kihistoria na kwa takwimu za kusafiri kati ya sehemu mbili.” Basi wakati mwingine ukitumia njia ya juu, jaribu uone—je, inainuka kushinda hii katika Utah?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Kwa hisani ya Mountainland Travel Region