Visiwa Vinavyoelea vya Ziwa Titicaca
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA PERU
VISIWA vieleavyo? Ndiyo, visiwa katika ziwa hili lisilo na kifani katika Amerika Kusini hufanya hivyo. Na watu huishi juu yavyo.[1]
Ziwa Titicaca, lenye kupakana na Peru upande wa magharibi na Bolivia upande wa mashariki, ndilo ziwa lililoinuka juu zaidi ulimwenguni liwezalo kupitiwa na vyombo vikubwa vya baharini. Likiwa kwenye meta 3,810 juu ya usawa wa bahari, laenea kilometa 190 kuelekea kaskazini-magharibi hadi kusini-mashariki na ni la zaidi ya kilometa 80 kwenye upana walo mkubwa zaidi.[2]
Baadhi ya visiwa vingi vya Ziwa Titicaca ni kama mikeka inayoelea ya totora kavu, mafunjo yaliyo kama matete yakuayo katika maeneo fulani yasiyo ya kina kirefu ya ziwa hilo. Matete hayo hukua kutoka chini ya ziwa hilo, hupita katika meta kadhaa za maji, na kuenea meta kadhaa juu ya uso wa maji. Ili kufanya kisiwa, yale matete hukunjwa na kufumanishwa yakiwa yangali yametia mizizi chini ya ziwa ili kutengeneza jukwaa, au sakafu, lililo kama manyasi lenye kukalia uso wa maji. Ndipo matete hayo hujazwa matope na kuimarishwa kwa matete ya ziada yaliyopasuliwa katika marefu yayo. Wakaaji huishi katika vijumba vya matete vilivyojengwa juu ya visiwa vya matete vyenye kuelea.[3]
The Encyclopædia Britannica yasema kwamba watu wameishi kwa muda mrefu katika visiwa hivi. Yatoa maoni haya pia: “Wakaaji wa ziwa hilo hutengeneza vyelezo vyao maarufu—mashua zilizoundwa kwa mafungu ya matete yaliyokaushwa na kufunganishwa, yafananayo na ile jahazi ya mafunjo iliyo na umbo la mwezi-mwandamo katika picha za majengo ya kale ya ukumbuko wa Kimisri.”[4]
Hivi majuzi, Mashahidi wa Yehova walijipatia mashua ya kuwahubiria watu katika visiwa vya Ziwa Titicaca. Mashua hiyo huendeshwa na mtambo ulio nje ya mashua nayo yaweza kubeba watu 16.[5] Mashahidi watembeapo kutoka kao hadi kao katika visiwa hivi vya matete, wao husema mtikisiko mdogo hutokea chini ya nyayo zao.[6] Jambo la kufurahisha ni kwamba, ujumbe wa Ufalme wa Mungu sasa unawafikia watu hata katika visiwa hivi vya mbali vieleavyo!