Duara za Afrika Zisizoeleweka
Katika ukanda mpana wa nchi wenye urefu wa kilometa 2,000 kwenye ukingo wa magharibi wa Jangwa la Namib huko kusini-magharibi mwa Afrika, kuna duara zenye mchanga usioweza kutokeza mimea ambazo zina kipenyo cha meta mbili hadi kumi. Kila duara imezingirwa na nyasi ndefu. Wageni fulani husema kwamba duara hizo hufanya ardhi ionekane kana kwamba ina ugonjwa wa ndui au alama zilizoachwa na matone makubwa ya mvua. Kulingana na mapokeo ya eneo hilo, duara hizo zina nguvu za kichawi. Makabila fulani yanaamini kwamba kila duara imezingira kaburi la mtu wa kabila la San aliyekufa katika mojawapo ya mapigano ya karne nyingi kati yao na wakoloni.
Pia, kwa muda mrefu wanasayansi wamejaribu kuelewa kisababishi cha duara hizo. Mnamo 1978, watafiti walitia alama katikati ya duara hizo kwa vyuma vilivyochongoka wakidhani kwamba baada ya muda fulani zitasonga. Miaka 22 baadaye, duara hizo hazikuwa zimesonga. Gazeti la London The Daily Telegraph, linaripoti kwamba kumekuwa na maoni mengi kuhusu chanzo cha duara hizo kama vile “utendaji wa mchwa, sumu kutoka kwenye mimea inayokua sehemu hizo, sumu kutoka kwa madini fulani na hata eti hizo ni sehemu ambapo mbuni hujisafisha kwa mchanga.” Gretel van Rooyen, profesa wa mimea katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini, alisimamia utafiti uliofanywa ili kuchunguza duara hizo. Anasema hivi: “Tulichunguza maoni yote yaliyotolewa na yote yakathibitishwa kuwa si ya kweli.”
Jambo muhimu ambalo huenda watafiti hao waligundua ni kwamba nyasi zilinyauka zilipopandwa kwa kutumia udongo kutoka katika duara hizo. Lakini zilikua vizuri zilipopandwa katika udongo uliotolewa katika sehemu zenye nyasi zinazozunguka duara hizo, kuonyesha wazi kwamba kuna tofauti kati ya udongo wa sehemu hizo mbili. Ingawa uchunguzi uliofanyiwa udongo huo haukuonyesha chochote, Van Rooyen anatarajia kwamba uchunguzi utakaofanywa kwa kutumia kifaa fulani kinachogawanya atomu na molekyuli kwa kutumia uzito wake utatoa habari zaidi. Anajiuliza kama kuna vitu vyenye sumu katika udongo ulio ndani ya duara hizo. Van Rooyen anasema hivi katika gazeti New Scientist: “Lakini hata kama tutapata vitu hivyo vyenye sumu, jambo litakalotutatanisha ni kujua jinsi vilivyoingia katika udongo huo.” Kwa sasa, duara hizo ni mojawapo ya mambo yenye kutatanisha ya dunia.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]
Courtesy of Austin Stevens