Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (Inaendelea)
ILIKUWA Ijumaa. Kulikuwa na kimya ya kutisha katika kambi nzima wakati kwa ghafula kikundi chenye amri kilipokuja na baada ya muda mfupi kikaweka shabaha za kulenga bunduki uani. Hii ikafanya uvumi wa kila namna uenee. Wasiwasi ukaongezeka zaidi amri nyingine zilipotolewa za kuacha kufanya kazi saa moja kabla ya wakati wa kawaida. Paul Buder angali akumbuka vile askari wa SS alivyomwambia akicheka-cheka, jamii ya wafanya kazi wenzake ilipokuwa ikitembea kijeshi: “Leo ndiyo Siku ya Kupaa! Mmoja wenu atakwenda mbinguni leo.”
Jamii ya wafanya kazi alimokuwa Heinrich Dickmann ilipoingia, msimamizi wa kambi akamkaribia akamwuliza kama anajua yanayoendelea. Alipojibu kwamba hajui, akaambiwa kwamba ndugu yake August atapigwa risasi.
Lakini hakukuwa na wakati wa kuzungumza mengi. Amri zikatolewa wafungwa wote watembee kijeshi kuelekea uwanjani. Mashahidi wa Yehova wakawekwa pale pale mbele ambapo ndipo wenye kupiga risasi wangesimama. Macho yote yakawa yamekazwa upande huo. Walinzi-askari wa SS wakaingia wakitembea kijeshi; ulinzi ukawa mkali mara nne kuliko ilivyo kawaida. Bunduki zikafunguliwa nazo risasi zikatiwa ndani. Askari wa SS walikalia ukuta ule mrefu wakitazamia litakalotukia—walikuwa wengi kama njugu hata ungeweza kudhani kikundi chote kilikuwa kimeamriwa kuwapo kuona tamasha hii ya kumwaga damu. Lango lililo kubwa lilikuwa limejengwa kwa vyuma vikubwa vya mviringo nao askari wa SS wenye kutaka kusisimuliwa na mambo haya walikuwa wamesimama na kuliegemea wakiwa wamesongamana kweli kweli. Wengine wao hata walikuwa wamepanda juu yake waone vizuri zaidi. Macho yao yalitaka sana kuona damu ikimwagika. Nyuso nyingine zilionyesha hofu kuu, kwa maana walijua litakalotukia karibuni.
Akifuatwa na wakuu kadha wa SS, August akaletwa, amefungwa mikono kwa mbele. Kila mtu akastaajabia namna alivyotulia na asivyoona wasiwasi, kama mtu ambaye tayari ameshinda vita. Karibu ndugu mia sita walikuwapo, naye ndugu yake wa kimwili Heinrich alikuwa amesimama hapo karibu tu.
Kwa ghafula vipaza-sauti vikaanza kuvuma huku vikuza-sauti vikifunguliwa. Ungeweza kusikia sauti ya “Miraba Minne” ikisema hivi: “Enyi wafungwa, sikilizeni’.” Kukawa kimya-a-a-a. Kilichosikika tu ni kupumua kwa kifua kwa dude hili lilipokuwa likiendelea kusema hivi:
“Mfungwa aitwaye August Dickmann wa Dinslaken, aliyezaliwa Januari 7, 1910, akataa utumishi wa kijeshi, akijidai yeye ni ‘raia wa ufalme wa Mungu.’ Yeye kasema: Amwagaye damu ya mwanadamu damu yake itamwagwa. Amejiondoa katika jamii ya watu na kulingana na maagizo ya kiongozi Himmler wa SS atauawa.”
Kukiwa kumekimya kabisa katika ua wote, “Miraba Minne” akaendelea kusema: “Nimemwambia Dickmann saa moja iliyopita atauawa saa 12:00.”
Mkuu mmoja akakaribia akauliza kama mfungwa huyo aweza kuulizwa tena kama amebadili nia na kama ana nia ya kutia sahihi karatasi za utumishi wa jeshi, naye “Miraba Minne” akajibu: “Hiyo haifai kitu.” Akamgeukia Dickmann, akasema kwa ukali: “Ewe nguruwe, geuka,” halafu akatoa amri ya kupiga risasi. Dickmann akapigwa risasi mgongoni na askari watatu wa SS. Baadaye mkuu wa SS akakaribia akamlenga risasi ya kichwa, damu ikatiririka shavuni mwake. Baada ya askari mdogo wa SS kumwondoa pingu, ndugu wanne wakaagizwa wamtie katika sanduku jeusi wampeleke katika chumba fulani hospitalini.
Ingawa wafungwa wengine wote sasa waliruhusiwa warudie majumba yao ya kiaskari, mashahidi wa Yehova wakaagizwa wabaki. Sasa “Miraba Minne” akapata nafasi ya kudai vya kutosha alivyotaka. Kwa mkazo mwingi akauliza nani aliye tayari sasa kutia sahihi yale maneno—si kwa kukana imani yake tu, bali pia kwa kuonyesha nia ya kuwa askari. Hakuna aliyeitikia. Halafu wawili wakajitokeza! Lakini kusudi lao halikuwa kutia sahihi maneno hayo. Wakaagiza sahihi zao wote wawili walizokuwa wametia karibu mwaka mmoja mapema zifutwe!
“Miraba Minne” akakasirika vilivyo. Kwa hasira nyingi akaondoka uani. Akina ndugu walitaabika sana jioni hiyo na siku chache zilizofuata. Lakini wakaendelea kuwa imara.
Kuuawa kwa Dickmann kulitangazwa mara kadha katika radio siku chache zilizofuata, yaelekea kwa tumaini la kutisha Mashahidi wengine waliokuwa huru.
Siku tatu baadaye ndugu yake Heinrich akaitwa kwenye “idara ya kisiasa.” Wakuu wawili wa Gestapo (polisi) wakawa wametoka Berlin kuja kuona kuuawa kwa ndugu yake kumekuwa na matokeo gani kwake. Kulingana na alivyosema mwenyewe, mazungumzo yafuatayo yaliendelea:
“‘Uliona ndugu yako alivyopigwa risasi?’ Nikajibu: ‘Ndiyo.’ ‘Umejifunza nini?’ ‘Mimi ni mmoja wa mashahidi wa Yehova nami nitaendelea kuwa mmoja wao.’ ‘Basi wewe ndiwe utakayefuata kupigwa risasi.’ Nikaweza kujibu maulizo kadha ya Biblia, mpaka mwishowe wakili mmoja akapaza sauti akisema: ‘Sitaki kujua yaliyoandikwa, nataka kujua maoni yako.’ Naye alipokuwa akijaribu kunionyesha uhitaji wa kutetea nchi yangu mwenyewe, akazidi kusema kama hivi: ‘Wewe ndiwe utakayefuata kupigwa risasi . . . ndiwe utakayekuwa wa pili kung’olewa kichwa . . . utakuwa wa pili kuangushwa.’ Mpaka yule wakili mwingine akasema: ‘Ni kazi bure. Haya, maliza kuandika.’ “
Kwa mara nyingine yale maneno yakawekwa mbele ya Ndugu Dickmann ayatie sahihi. Akakataa, akisema: “Nikiitambua serikali kwa kutia sahihi nitakuwa ninaonyesha nakubaliana na kuuawa kwa ndugu yangu. Siwezi kufanya hivyo.” Akajibiwa hivi: “Basi anza kufikiria utakuwa hai mpaka lini.”
Lakini ni nini kilichompata “Miraba Minne,” aliyekuwa amemfanyia Yehova mzaha na kumkaidi sana kama wasivyopata kufanya wanadamu wengi? Baada ya hapo alionekana kambini mara chache tu, halafu hakuonekana tena. Walakini, wafungwa wakagundua kwamba muda mfupi baada ya kuuawa kwa August Dickmann, Miraba Minne alipatwa na ugonjwa mbaya sana. Akafa miezi mitano baadaye bila ya kupata nafasi nyingine ya kufanyia Yehova wala mashahidi wake mzaha. “Miraba Minne” alikuwa amesema hivi Machi 20, 1938 alipotenga mashahidi wawe peke yao, “Nimeanza kupigana na Yehova. Tutaona mwenye nguvu ni nani, mimi au Yehova.” Mshindi akajulikana. “Miraba Minne” kashindwa. Na ingawa ndugu zetu walifunguliwa katika kifungo cha upweke miezi michache baadaye, na hata nyakati fulani wakafarijika sana, habari zikaendelea kuvuma katika kambi yote kwamba “Miraba Minne” ni mgonjwa sana na kwamba wakuu walipokuwa wakimtembelea kitandani pake alikuwa akilia-lia kigonjwa: “Wanafunzi wa Biblia wananiombea nife, kwa sababu niliagiza mtu wao apigwe risasi!” Uhakika pia ni kwamba alipokwisha kufa binti yake alikuwa akijibu hivi alipoulizwa kilichosababisha kifo cha baba yake: “Wanafunzi wa Biblia ndio waliomwombea baba afe.”