Vifo Vinavyotokana na “Cancer” (Donda Baya) ya Matiti
◆ Uchunguzi wa chama kiitwacho World Health Organization unaonyesha wazi kwamba wanawake zaidi sasa wanakufa kutokana na cancer ya matiti kuliko wakati mwingine wo wote, ingawa jitihada sasa zinafanywa mapema kuichunguza na kupasua. Kulingana na uchunguzi huo, si wengi sana wanaokufa kwa sababu ya cancer hiyo katika sehemu kubwa zaidi ya Asia, Afrika na Latin Amerika. Lakini, kwa wastani, mwanamke mmoja kati ya 25 anakufa kutokana na ugonjwa huo katika Ulaya ya Magharibi na Amerika ya Kaskazini. Ripoti hiyo yasema, “Ni wazo la kusikitisha kwamba njia za utabibu za sasa hazielekei kumaliza sana ugonjwa huo wala vifo vingi vya wanawake, ingawa kwa wazi zina matokeo mazuri kwa watu wengi mmoja mmoja.” Katika Amerika ya Kaskazini na Ulaya ya Magharibi akina mama hawanyonyeshi sana watoto matiti yao. Watu wengi wanaona hilo ni jambo lenye kusababisha kadiri kubwa zaidi ya cancer ya matiti.