Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w76 7/1 kur. 292-294
  • Unabii wa Paradiso

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Unabii wa Paradiso
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
w76 7/1 kur. 292-294

Unabii wa Paradiso

1. Akiisha kukazia uhakika wa utimizo wa neno lake, Yehova anaahidi nini, kama ilivyoandikwa katika Isaya 55:12, 13?

LILE ambalo Yehova Mungu amesema juu ya uhakika wa kwamba neno lake litatimia, latutia nguvu tuukubali unabii wa ajabu unaotimia sasa kwa tumaini lenye hakika. Anawatolea unabii wale wanaomtafuta na kuitia jina lake na kurudi kwake katika toba na haki. (Isa. 55:6, 7) Akifunua namna mawazo na njia zake zilivyo juu ya zile za wanadamu wasiokamilika, wenye kufa, aendelea kusema: “Maana mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani; mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; na miti yote ya kondeni itapiga makofi. Badala ya michongoma utamea msunobari, na badala ya mibigili, mhadesi; jambo hili litakuwa la kumpatia [Yehova] jina, litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali.”​—Isa. 55:12, 13.

2, 3. (a) Ni ukombozi gani wa ajabu unaosimuliwa humo? (b) Ni nani ‘wangefurahi,’ na Zaburi 126:1, 2 yasimuliaje vizuri maono yao?

2 Je! maneno hayo hayasimulii vizuri kukombolewa kwenye kusisimua kwa watu waliohamishwa na kurudi kwao pamoja na kukaribishwa kwa furaha! “Maana,” yaani, kwa uhakikisho wa yale ambayo Yehova amesema juu ya mawazo na njia zake zilizo juu kuelekea watu wake, “mtatoka kwa furaha.” Walipaswa watolewe katika nchi ya Babeli, wakiwa watu waliokombolewa. Kukombolewa huku kungekuwa pamoja na kufurahi, si kufurahi kwa watu wa Mataifa katika wonyesho wo wote wa kusikitikia watu wa Yehova waliohamishwa, bali kufurahi kwa watu Wake ambao Yeye alikuwa akikomboa katika njia hiyo ya ajabu, tofauti na tumaini au tamaa ya watu wa Mataifa. Furaha ya mabaki ya Kiisraeli na wenzi wao waliojitoa kwa sababu ya kufunguliwa kwa ajabu katika Babeli ya kipagani kwarudiwa katika maneno ya mwanzo ya Zaburi 126 hivi:

3 “[Yehova] alipowarejeza mateka wa Sayuni; tulikuwa kama waotao ndoto. Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, [Yehova] amewatendea mambo makuu.”​—Zab. 126:1, 2; 2 Nya. 36:20-23.

4, 5. Katika ukombozi waliopata katika mwaka wa 537 K.W.K., Wayahudi waaminifu wangewezaje kuona kwamba Yehova alikuwa ameonyesha ukweli wa neno lake?

4 Ukombozi ulipotokea katika mwaka wa 537 K.W.K., mabaki waaminifu wa Kiyahudi waliweza kuutazama unabii ulioongozwa na Mungu wa Isaya 44:28 mpaka 45:3, uliokuwa umetangulia kuandikwa karne mbili, na waliweza kuona namna Mungu wao alivyokuwa ameonyesha Neno lake kuwa kweli kwa kumtumia mtumishi wake aliyetiwa mafuta, Koreshi Mwajemi, katika kuwakomboa. Habari ya kweli ya Ezra 1:1-5 yapatana sana na unabii wa Isaya kwa kuarifu hivi:

5 “Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la [Yehova] alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, [Yehova] akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi, asema hivi; [Yehova], Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Mungu wake na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya [Yehova], Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya [Yehova], iliyoko Yerusalemu.”

6. Sababu gani Wayahudi hawakutoka Babeli kwa ukimbizi wa ovyo-ovyo?

6 Kwa hiyo mabaki ya Kiyahudi na wenzi wao hawakuondoka katika Babeli katika mwaka wa 537 K.W.K. kwa sababu ya kushikwa na woga wa ghafula au kwa ukimbizi wa ovyo-ovyo. Isingeweza kuwa hivyo ikiwa wangetoka “kwa furaha,” kama ilivyokuwa imetabiriwa. Walitoka kwa utaratibu, bila kuogopa kwa kuwaona wale waliokuwa wakiwafuatia. Walitoka wakiwa na hakika sana kwamba yule Mungu aliyekuwa amewafungua angewatangulia awaongoze katika njia na ya kwamba angewakinga nyuma. Yeye alikuwa amewapa ahadi kwa sababu hii: “Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu; tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya [Yehova]. Maana hamtatoka kwa [woga wa ghafula], wala hamtakwenda kwa kukimbia, kwa sababu [Yehova] atawatangulia; na Mungu wa Israeli atawafuata nyuma; awalinde.”​—lsa. 52:11, 12.

7. (a) Walikuwa na sababu gani ya kuwa hakika kwamba wangefika salama kwao? (b) Walirudi katika nchi ya kwao kama wakati gani, na hili lashuhudiaje kwamba neno la Yehova halirudi kwake bila matokeo?

7 Walitoka katika Babeli wa kale kwa amani, kwa kujipanga wenyewe vizuri, na wangefika kwao kwa amani, chini ya ulinzi na uongozi wa kimungu. Hivyo ndivyo neno la kimungu lisilokosa lilivyowahakikisha: “Maana mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani.” (Isa. 55:12) ‘Wangeongozwa’ waletwe kwao, nchi iliyokuwa imekaa hali ya ukiwa muda wa miaka 70. Kama tafsiri ya Mwalimu Leeser ya maandishi ya kale ya Kiebrania isomwavyo: “Kwa maana kwa furaha mtatoka, na katika amani mtapelekwa kwenu.” Au, kama The New American Bible isemavyo: “Ndiyo, kwa furaha mtaondoka, katika amani mtarudishwa.” Ikawa hivyo, na, mwezi wa saba (Tishri) wa mwaka wa 537 K.W.K., mabaki ya Kiyahudi na wenzi wao waaminifu wakawa wamekaa katika sehemu zao za miji, wakaanza kuirudisha ibada ya Mungu wao katika nchi ya kwao. (Ezra 2:68 mpaka 3:2) Kama vile mvua na theluji inavyoshuka kutoka mbinguni na kutimiza kusudi la Mungu, vivyo hivyo neno la unabii la Yehova halikurudi kwake bila kuleta matokeo yake.​—Isa. 55:10, 11.

8, 9. (a) Walipofika kwao, je! wahamishwa wa kale waliona kwamba nchi yao ilikuwa paradiso? (b) Mungu alikuwa ameahidi kungetukia nini katika wakati wake wakiisha kuanza kufanya kazi?

8 Ile njia ambayo mabaki ya Kiyahudi na wenzi wao wenye kumwogopa Mungu walifuata kutoka Babeli haikuwa ya kupitia katika paradiso, wala sehemu yenye mashamba kando ya njia haikugeuka kwa mwujiza ikawa paradiso mbele yao ili kuwachangamsha katika safari ya miezi mingi. Wala nchi ya kwao yenye kukaa ukiwa muda mrefu, yenye kumelea michongoma haikuchukua kwa ghafula sura ya paradiso mbele ya macho yao. Lakini matumaini yao kulingana na ahadi ya Mungu yalikuwa nini walipokwisha kurudishwa katika nchi yao wenyewe waipendayo na kwa bidii wakaanza kufanya kazi, bila kutazamia mgeuzo wo wote wa miujiza? Aa, kwa habari hii kuhani wao mkuu Yesua mwana wa Yehozadaki au gavana wao aliyewekwa mwana wa Shealtieli aliweza kuwasomea maneno yenye kuchangamsha, yenye kutia moyo ya Isaya 55:12, 13:

9 “Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; na miti yote ya kondeni itapiga makofi. Badala ya michongoma utamea msunobari, na badala ya mibigili, mhadesi; jambo hili litakuwa la kumpatia [Yehova] jina, litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali.”​—Hagai 1:1.

10. Kama inavyoonyeshwa katika unabii, sifa ingekuwa ya nani kwa sababu ya mgeuzo wa nchi hiyo, na kwa sababu gani kwa kufaa hivyo?

10 Kweli kweli ungekuwako mgeuzo wenye kupendeza wa nchi isiyotunzwa, isiyolimwa kwa muda mrefu! Walakini, jambo hili halingetukia bila kwanza watu waliorudishwa kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo. Hata hivyo, sifa imepaswa na ingemwendea Yehova kwa mgeuzo huo wa ajabu, kwa maana Yeye Ndiye angezibariki jitihada zao za unyofu. Kubariki kwake jitihada zao lilikuwa ndilo jambo la lazima, na wangepata baraka yake mradi wangeitanguliza ibada Yake na kulitimiza kusudi ambalo kwa hilo alikuwa amewafungua kutoka katika Babeli yenye kuonea akawarudisha kwenye nchi ya kwao, waliyopenda.

11. Ni nini lililotoa ushuhuda kwamba nchi ya Yuda ilikuwa imekuwa kama ardhi iliyolaaniwa, wakati wa miaka yake ya ukiwa?

11 Bila shaka walipoirudia nchi yao michongoma ilikuwa mingi, na mibigili ilisitawi juu ya nchi iliyoachwa bila kulimwa kwa muda mrefu. Mimea hiyo haikuwa sehemu yenye kutokeza, yenye kuvutia ya paradiso ya kwanza ya wanadamu. Badala yake, Mungu alipohukumu mwanamume na mwanamke wa kwanza kama wafanya dhambi waishi nje ya Bustani ya Edeni, alimwambia mwanamume huyo hivi: “Ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia.” (Mwa. 3:17, 18) Hivyo nchi ya Yuda, ilikuwa imekuwa kama ardhi iliyolaaniwa wakati wa miaka yake 70 ya ukiwa: “Ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.”​—Ebr. 6:8; linganisha Kumbukumbu la Torati 28:15-18; Isa. 24:6.

​—Kutoka Kitabu Man’s Salvation Out of World Distress at Hand!, sura ya 7.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki