Sala Yajibiwa
KATIIKA visiwa vya South Pacific vya Samoa, wakuu wa huko wana uwezo mwingi sana. Wanaheshimu sana vyeo vyao nao wanaheshimiwa sana na watu. Kwa hiyo, lazima kuwe na sababu kubwa sana ya kumfanya mkuu aachilie cheo chake.
Kwa hiyo, wakati mmoja wa wanaume hawa kutoka kisiwa cha Savaii katika Samoa ya Magharibi alipoacha kazi yake, akisema kwamba alitaka asiwemo kabisa katika mambo ya siasa ili amtumikie Mungu, lilikuwa jambo la kushangaza sana. Sana-sana lilishangaza kwa sababu, mwanamume huyu ndiye mara nyingi aliyekuwa mnenaji wa Malietoa, mmojawapo wa wafalme. Wakati wo wote wakuu na wafalme wa Samoa walipokutana, mara nyingi mwanamume huyu ndiye aliyetangulia kusema.
Mkuu huyu alikuwa amejiunga na mojawapo la makanisa ya Jumuiya ya Wakristo, na kwa kuwa alikuwa anapendezwa na kujifunza mengi juu ya Mungu, alikuwa amechunguza mafundisho ya makanisa mengi. Walakini, hakujisikia ameridhika kiroho. Siku moja alifumbua kwamba mchungaji wa kanisa lao alikuwa akitumia fedha za kanisa kwa makusudi yake mwenyewe, akijinunulia vitu vingi vya anasa. Aliwajulisha washiriki wa kanisa jambo hilo, wakamchagua aseme na mchungaji huyo. Mchungaji alijibu: “Nifanyalo na fedha hizo si shauri lako; hilo ni juu yangu na Kristo.” Aliposikia hivyo, mkuu huyo alijiuzulu kanisa hilo, asirudi humo tena.
Wakati huo mkuu huyu alimwomba Mungu faraghani amsaidie kujua kweli. Siku moja, alipokwisha kuomba namna hiyo, mmoja wa Mashahidi wa Yehova alimtembelea na funzo likaanzishwa. Baada ya kupita muda fulani, mwanamume huyu alitaka kutoa maisha yake kwa Yehova, asiwe tena sehemu ya taratibu ya kisiasa ya ulimwengu huu. Ijapokuwa cheo chake kilimletea heshima na mali, yeye aliona inafaa zaidi awe huru na uhusiano wo wote na siasa za ulimwengu. (Yak. 4:4) Sasa, akiwa shahidi wa Yehova aliyebatizwa, anajitahidi awezavyo kusaidia wengine wajifunze kweli.