Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w81 12/15 kur. 6-7
  • Kuendelea Kuwa Imara Katika Imani Nyakati za Magumu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuendelea Kuwa Imara Katika Imani Nyakati za Magumu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
w81 12/15 kur. 6-7

Kuendelea Kuwa Imara Katika Imani Nyakati za Magumu

KATIKA sehemu nyingi za dunia, Wakristo wa kweli wanateswa vikali sana, sawa na ilivyokuwa katika karne ya kwanza. Kama vile Wakristo wa siku hizo walivyoendelea kuwa imara katika imani, ndivyo wale wa siku hizi wanavyofanya. Kuelekea mwishoni mwa mwaka wa 1978, mwangalizi mmoja mwenye kusafiri wa Mashahidi wa Yehova aliliandikia tawi la nchi ambayo yeye anatumikia ikieleza habari za mateso mabaya sana yanayoletwa kwa wingi juu ya Mashahidi katika eneo hilo. Uthabiti wao unang’aa ukiwa mfano mwingine mzuri sana wa ukamilifu wa Kikristo.

Kulingana na ripoti ya mwangalizi huyo mwenye kusafiri, wafanya matata waliambia kikundi cha Mashahidi hivi:“Sisi hatutaki kuwasikia mkihubiri tena habari za Yesu.” Lakini Mashahidi wakajibu: “Sisi hatuoni ubaya wo wote juu ya mambo aliyofanya Yesu. Kwa hiyo kumhubiri kwetu hakuna ubaya wo wote.”

Wanaume hao walikasirika sana. Basi wakawaagiza Mashahidi—ndugu watatu na dada wawili—wachukue vitabu vyao vyote wavipeleke kilomita tano hivi (maili 3) kutoka hapo. Kufika huko wakavichoma vitabu. Halafu, baada ya kuwapeleka kina ndugu umbali mdogo kutoka hapo, wakaanza kuchapa mmoja wa kina dada—kisichana tu—huku kina ndugu wakitazama. Kwa kuwarudia kina ndugu, wakasema: “Msichana huyo amesema ninyi mlimlazimisha awe Shahidi.” Walakini, yule dada mdogo aliyekuwa ametoka kuchapwa saa iyo hiyo akasikia maneno hayo kwa mbali, naye akapaza sauti akisema: “Ni uongo!”

Halafu mikono ya ndugu mmoja ikafungwa kwa nyuma. Alipigwa akazimia. Baada ya kupiga kelele wakisema “Yesu chini,” wenye kuwatesa-tesa walipiga ndugu mwingine wakamkata sikio moja likang’oka. Ndugu wa tatu alipigwa kwa ukatili mwingi sana, hata jicho moja likakaribia kuwa na upofu. Lakini hakuna hata mmoja wa ndugu hao aliyeikana imani yake wajapokuwa wametendwa kinyama.

Mwishowe, wakawapeleka kina ndugu mtoni, wakikusudia kuwazamisha wafe maji. Wakiwa njiani kuelekea mtoni kina ndugu walisali kwa bidii nyingi. Halafu wale wenye kuwatesa-tesa wakabadili nia zao na kuwarudisha nyumbani kwao. Wakaambiwa wasirudi mjini kwenye Jumba la Ufalme kwa muda wa miezi mitatu itakayofuata. Hata hivyo Jumapili iliyofuata mmoja wa ndugu hao alikwenda mkutanoni mjini.

Baadaye, Mashahidi wale wale watano walifikiwa njiani na kikundi kingine cha wanaume. Wakaulizwa, “Ninyi mnamfikia Mungu kupita kwa nani?” Mmoja wa kina ndugu akajibu, “Kupita kwa Yesu.” Lakini akakatizwa kwa kuambiwa: “Sisi tunamfikia Mungu kupita kwa mizimu ya mababu waliokufa.” Kisha mwingine mwenye kuuliza-uliza maulizo akaongezea: “Kwa hiyo ninyi hamwaabudu mababu wenu waliokufa.” Mashahidi walibaki kimya.

Halafu mmoja wa watu hao akachukua fimbo kubwa akaanza kuwatandika kina ndugu. Wengine wakajiunga naye, wakawapiga ngumi kina ndugu na kuwapiga-piga mateke kwa viatu vyao. Baada ya kitambo, mmoja wa kina ndugu akatenganishwa na wale wengine akapelekwa mbali na kikundi kingine cha watu aulizwe-ulizwe maulizo. Akaambiwa arudie kuutaja usemi “Vita na iendelee.” Akapigwa tena kwa sababu ya kukataa. Mmoja wa wenye kuwatesa-tesa akasema: “Wewe tupe shavu lile jingine maana Yesu alisema mtu akikupiga shavu moja mpe na lile jingine.”

Ndugu huyo akatii, kisha akachekelea wakati wale wengine walipokuwa wakimfanyia mzaha (utani). Walakini, yule aliyemwambia ageuze shavu lile jingine hakumpiga tena, bali alisema hivi kwa dhihaka: “Wewe ni kama mwenda-wazimu. Sasa nenda zako!” Hata hivyo, wengine wakaanza kumpiga kwa matako ya bunduki zao na kwa ngumi zao, huku wengine zaidi wakimpiga-piga mateke kwa viatu vyao vizito. Kufikia wakati huo alikuwa ameharibiwa sana.

Waliposhindwa kumfanya akubaliane nao, walimrudisha ndugu mahali walipokuwa wale watesi wa kwanza. Nao wakaendelea kumbembeleza akubaliane nao na kuutaja usemi “Vita na iendelee.” “Kusema hivyo ni kajambo kadogo tu,” wakamwambia. Lakini ndugu alisimama imara, akakataa kukubaliana nao katika jambo hilo ijapokuwa aliendelea kupigwa-pigwa.

Karibu na wakati huo mke wa ndugu huyo akafika mahali hapo. Walipojua yeye ni nani, wanaume hao wakajaribu kumbembeleza amwambie mumewe arudie kuutaja usemi wao. Lakini dada akabaki kimya. Wakati huo usiku wa manane ulikuwa umekwisha kuingia na kupita—kina ndugu wakiwa wamevumilia mateso yote saa za mchana—kisha watesi wakachoka na kwenda zao.

Kesho yake, ndugu waliamua kutoroka kwa utulivu, wakaacha nyuma mali zao ili isijulike wanatoroka. Wakakuta baadhi ya Mashahidi, nao wamewatunza ndugu zao waliokuwa wamevumilia mambo mengi sana.

Nia ya Mashahidi hao walioteswa ni nini? ‘Kukiwa na uhitaji, sisi tumekaza nia tufe kwa ajili ya jina la Yehova,’ ndivyo wanavyosema. Na ivyo hivyo ndivyo walivyowaambia watesi wao macho kwa macho. Matokeo yamekuwa nini kwa sababu ya kushika ukamilifu kwa njia hiyo? Jambo moja ni kwamba, wengine kati ya waliowaona wakivumilia ukatili huo wa kinyama walisikiwa wakisema hivi baadaye: “Yehova ndiye Mungu wa kweli.”

“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi [kuwatesa, NW] na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”​—Mt. 5:11, 12.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki