Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 12/15 kur. 21-23
  • Kufika kwa “Msaidizi,” Roho Takatifu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kufika kwa “Msaidizi,” Roho Takatifu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 12/15 kur. 21-23

Kufika kwa “Msaidizi,” Roho Takatifu

(Funzo la Kitabu)

1. “Msaidizi” aliyeahidiwa angetolewa katika jina la nani, na kwa walioamini jina la nani?

MIAKA isiyozidi mia tano kabla Yesu Kristo hajatoa ahadi hiyo kwa mitume wake, Liwali Nehemia huko Yerusalemu aliandika sala juu ya namna Mungu alivyowatendea Waisraeli: “Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako.” (Neh. 9:30) Na sasa, wakati ambapo Yesu Masihi angekuwa hayupo pamoja na wanafunzi wake, roho ile ile ya Yehova Mungu ingekuja kuwasaidia. Wangepewa roho hiyo kupitia kwa jina la Yesu peke yake. Ingetolewa kwa watu wale tu ambao wangeamini kwamba Yesu ndilo jina la Masihi wa kweli. Ilitolewa lini kwa mara ya kwanza?

2, 3. (a) Yesu alifikia upeo wa siku zake 40 baada ya kufufuliwa kwa kuwaahidi wanafunzi wake jambo gani lililokuwa tofauti na ubatizo wa Yohana? (b) Ni ulizo gani lingetokea juu ya ubatizo huu ulioahidiwa?

2 Kwa muda wa siku 40 baada ya kufufuliwa kwake Yesu kutoka kwa wafu katika Nisani 16, 33 W.K., aliendelea kukaa hapa duniani, walakini kwa kutokuonekana. Nyakati nyingine, alifanya kama vile malaika wa nyakati zilizopita, akachukua umbo la kibinadamu, ili kuwapa wanafunzi wake ushuhuda wa kwamba kwa kweli alikuwa amefufuka kutoka kwa wafu, walakini kama roho. Nyakati hizo alizowatokea aliendelea “[kuwafundisha] mambo yaliyohusu ufalme wa Mungu.” (Matendo 1:1-3) Wengine wa hao mitume walikuwa wamekuwa wanafunzi wa Yohana Mbatizaji. Na sasa wakati wa siku ya 40, siku ya kupaa kwake mbinguni, Yesu Kristo aliwapa wanafunzi wake matazamio zaidi alipowaambia: “Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika [roho takatifu] baada ya siku hizi chache.” (Matendo 1:4, 5) Wayahudi waliotubu waliobatizwa na Yohana walibatizwa ili kuonyesha toba yao juu ya makosa yao waliyofanya kwa kuvunja sheria ya Mungu kupitia kwa Musa.

3 Huenda ubatizo huo katika maji ukawa uliwapa faraja pamoja na dhamiri njema. Lakini matokeo yangekuwaje juu ya wanafunzi wa Yesu ‘wakiisha batizwa [zamishwa] katika roho takatifu’? Ilipaswa iwatie nguvu, kwa sababu roho takatifu ya Mungu, ni nguvu takatifu ya utendaji isiyoonekana.​—Mt. 3:11.

4. Kulingana na maneno ya Yesu katika Matendo 1:6-8, wangetiwa nguvu kwa roho takatifu wafanye jambo gani?

4 Wakati ingefika, roho takatifu ya Mungu ingewatia nguvu wenye kuipokea wafanye nini? Muda mfupi kabla ya kupaa kwake mbinguni, Yesu alisema hivi kwa wanafunzi wake: “Mtapokea nguvu, [ikiisha kuwajilia juu yenu roho takatifu]; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” (Matendo 1:6-8) Katika maneno hayo mna jibu la ulizo letu: Kuwatia nguvu wapokeaji wa roho takatifu ili watoe ushuhuda kwamba Yesu ndiye Masihi, Kristo.

5. Ahadi ya Yesu kwa wanafunzi wake ilitimizwa chini ya hali gani katika siku ya 50 ya kufufuliwa kwake?

5 Yesu Kristo apaa mbinguni. Siku kumi zapita. Siku ya 50 tangu kufufuka kwake yafika! Huko Yerusalemu sikukuu ya Kiyahudi ya Majuma au Pentekoste (inayomaanisha “ya hamsini” ikihusu siku) yaanza. Asubuhi na mapema wanafunzi wapatao 120 wamekusanyika pamoja, si kwenye hekalu lenye sherehe, bali katika chumba cha orofa, wakingojea, “kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa [roho takatifu], wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama [roho i]livyowajalia kutamka.”​—Matendo 1:2-4.

6, 7. Kama alivyoeleza Petro, ni unabii gani ulioanza kutimizwa katika siku hiyo ya Pentekoste, nao ulitimizwa baada ya muda gani kupita tangu utolewe?

6 Aha, mwishowe, baada ya zaidi ya miaka mia nane tangu ulipotolewa, unabii wa Yoeli 2:28-32 ukawa umeanza kutimizwa. Wayahudi walioshtuka wakakusanyika ili kutazama jambo hili la ajabu. Wengine wakawashtaki wanafunzi kuwa walikuwa wamelewa. Kwa ujasiri mtume Petro akawaambia hivi:

7 “Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, itakuwa siku za mwisho, asema [Yehova], nitamwagia watu wote roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake [r]oho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu kabla ya kuja ile siku ya [ajabu ya Yehova] iliyo kuu na iliyo dhahiri. Na itakuwa kila atakayeliitia jina la [Yehova] ataokolewa.”​—Matendo 2:16-21.

8. Ni ubatizo gani uliotukia wakati huo, naye Petro alionyesha kwamba ni nani aliyetumiwa kufanya ubatizo huo?

8 Ubatizo katika roho takatifu ulikuwa umetokea, kama vile Yesu alivyokuwa ameahidi. Kusemwa kwamba roho ‘ingemwagwa’ kungepatana na uhakika wa kwamba roho ni kama kitu chenye umajimaji chenye kumwagika kwa ajili ya ubatizo au uzamisho. Twakumbuka kwamba Mungu alimpa Yohana Mbatizaji ishara kuhusu Yesu, ili kuonyesha kwamba “ndiye abatizaye kwa [roho takatifu].” (Yohana 1:33) Kupatana na uhakika huu, mtume Petro alimtambulisha Yesu Kristo aliyetukuzwa kuwa wakili wa Mungu katika kumwaga roho takatifu juu ya Wakristo hawa wa kwanza. Kuongezea hayo, Petro alisema hivi kwa washerehekeaji hao wa Pentekoste wa Kiyahudi: “Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake. Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya [roho takatifu], amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia.”​—Matendo 2:32, 33.

9. Petro angewezaje kusema kwamba waliona na kusikia kile ambacho Yesu aliyetukuzwa alikuwa amekimwaga?

9 Wao waliona na kusikia utendaji wa roho takatifu, kwa maana waliona ndimi kama za moto juu ya vichwa vya wanafunzi hao na kuzisikia lugha za kigeni zilizozungumzwa kimwujiza na wanafunzi hao.

10. Ni jambo gani jingine lililotukia kwa wanafunzi wakati huo, ili lilingane na lile lililotukia kwa Yesu baada ya kubatizwa kwake katika maji?

10 Walakini, jambo lililo zaidi ya kubatizwa tu kwa wanafunzi hao wa Yesu katika roho takatifu lilikuwa limetukia vilevile. Kama vile Yesu alivyotiwa mafuta kwa roho takatifu baada ya kubatizwa katika maji na hivyo akawa Kristo au Mtiwa Mafuta, ndivyo na wanafunzi wake. Walitiwa mafuta kwa kile alichobatizwa kwacho.

11. Vilevile, wanafunzi hao walitiwa muhuri kwa kitu gani, kama alivyoeleza Paulo katika 2 Wakorintho 1:21, 22?

11 Zaidi ya hayo, walitiwa muhuri kwa roho hiyo kama wonyesho wa urithi wao wa kiroho utakaokuja. Hii inapatana na yale ambayo mtume Paulo aliliambia kundi la Kikristo katika Korintho wa kale, katika Ugiriki: “Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo na kututia mafuta, ni Mungu naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa [wonyesho wa kile kitakachokuja, yaani, hiyo roho,] mioyoni mwetu.”​—2 Kor. 1:21, 22.

12. Baadaye mtume Yohana aliandika nini juu ya kupakwa mafuta katika 1 Yohana 2:20, 27?

12 Mtume Yohana, ambaye alikuwapo wakati huo wa Pentekoste wa kumwagwa kwa roho takatifu, alifahamu jambo lililokuwa limetukia. Kwa hiyo aliwaandikia waamini wenzake hivi: “Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.”​—1 Yohana 2:20, 27.

​—Kutoka Holy Spirit​—the Force Behind the Coming New Order, Sura ya 6.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki