Jihadhari Usije Ukawakwaza Wengine
Watu wanaodai kuwa wanampenda Mungu na Kristo wanahitaji kuangalia maneno na matendo yao. La sivyo, huenda wakawa na hatia ya kumkwaza mmoja wa “wadogo” wa Yesu au wafuasi wake. Yesu mwenyewe alilieleza jambo ili hili katika njia ya kitamasha aliposema hivi:
“Ye yote atakayemkwaza mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari.”—Marko 9:42; Mt. 18:6, HNWW.
Mawe ya kusagia kama hilo linaloonyeshwa hapa huyafanya maneno ya Yesu yawe yenye kukazia sana maana. Kuzungusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia kulihitaji nguvu za mnyama kwa kuwa lilikuwa na upana wa futi nne mpaka tano (1.2 mpaka 1.5 m). Kwa sababu ya ukubwa wa jiwe kama hilo, hakungekuwa na tumaini la kuokoka kwa mtu ambaye angezamishwa baharini akiwa amefungiwa uzito mkubwa kama huo shingoni mwake. Bila shaka, hicho ni kitia-moyo chenye nguvu cha kutufanya tujihadhari katika maneno na matendo yetu!