Dhuluma—Imeenea Kadiri Gani?
MAPEMA mwaka wa 1940 mwanamume mwenye umri wa miaka 34 jina lake Roi alikamatwa katika New Meksiko, Marekani, akashtakiwa unyang’anyi. Alidai alikuwa kilomita 1,600 kutoka mahali pa uhalifu huo ulipokuwa ukifanywa, lakini hakuweza kuleta mashahidi wo wote kuthibitisha hilo. Kwa hiyo akapatikana na hatia akafungwa gerezani. Miaka kumi na sita baadaye Roi alifunguliwa kutoka gerezani. Uchunguzi ulikuwa umefunua kwamba hakuwa na hatia!
Miaka kadha iliyopita mwanamke mmoja katika Kolombia aliandikia gazeti moja akieleza hadithi yenye kusikitisha. Mume wake alikuwa amemwacha yeye na wanaye wanne akamwendea mwanamke mwingine. Hata hivyo, kwa kujitahidi sana na kujinyima mwanamke huyo alikuwa amewapa wanaye elimu wakati huo, na kwa msaada wao, akaweka raslimali ili jamaa yake iishi kwa starehe. Halafu siku moja akapewa taarifa ya kumtaka aende mbele ya hakimu. Kwa sababu gani? Mume wake alikuwa ameleta mashtaka. Mke huyo akaambiwa kwamba nusu ya kila kitu alichokuwa nacho kilikuwa ni mali ya mume wake. “Nashindwa kuelewa dhuluma hiyo,” akasema kwa kustaajabu.
Miaka mingi iliyopita mwanamume mmoja mwenye hekima alieleza kwa muhtasari mengi yanayowapata wanadamu aliposema: “Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.” (Mhubiri 8:9) Mamlaka hiyo imefanya watu mmoja mmoja wateseke, kama inavyoonyeshwa na mifano hiyo miwili. Pia imetokeza kudhulumiwa kwa jamii nzima nzima za watu. Ebu fikiria mifano michache tu.
Uchumi: Kulingana na kitabu The World Almanac & Book of Facts 1984, mapato ya India kwa wastani yalikuwa shilingi (za Kenya) kama 1,950 kwa mwaka—ambapo wakati huo katika nchi nyingi za Ulaya mapato ya wastani yalikuwa shilingi (za Kenya) kama 130,000 kwa mwaka. Wanauchumi wanasema kwamba tofauti hizo zimetilia shaka mafaa na haki ya utaratibu wa kiuchumi uliopo.”
Afya: “Kuelekea Haki ya Afya” ndicho kilichokuwa kichwa cha hivi majuzi cha gazeti moja la afya la umoja wa Mataifa. Kuna dhuluma gani katika afya? Mfano mmoja ni kwamba muda usio mrefu uliopita kijana mmoja mwanamume katika Kenya alikufa kwa sababu alihitaji dawa ya sumu ya nyoka. Hakukuweko dawa ya sumu ya nyoka katika eneo lote aliloishi! Je! ni haki kwamba watu wafe katika nchi fulani kwa sababu ya maradhi ambayo kwa kawaida yanaponywa au kuzuiwa katika nchi nyingine? Watu milioni 25 wanakufa kila mwaka kwa sababu ya maradhi yanayosababishwa na maji machafu na uchafu wa afya. Hata hivyo haingekuwa vigumu kuwapa maji masafi, na ingegharimu theluthi moja (sehemu moja kwa tatu) tu ya pesa ambazo ulimwengu unatumia kwa sigara au sehemu moja kwa kumi na nane (1/18) ya pesa ambazo ulimwengu unatumia kwa silaha. Je! hiyo ni haki?
Chakula: Katika mwaka wa 1980 watu kama milioni 50 waliuawa na njaa. Hata hivyo, kuna chakula kumtosha kila mtu na kusaza—kama kingegawanywa vizuri. Tatizo ni kwamba nchi nyingine zinatumia chakula kinachozidi posho lao. Mara nyingi, hata wakati chakula kinapatikana, maskini hawawezi kukinunua. Afisa mmoja mkuu wa Shirika la Kusaidia Watoto la Umoja wa Mataifa alisema kwamba hali hiyo ni ya ‘dhuluma, isiyokubalika na ambayo karibu haiwezi kuepukika.’
Ubaguzi: Likieleza ghasia yenye jeuri ya ubaguzi wa rangi katika Marekani, gazeti moja la habari lilisema: “Kisababishi kikubwa zaidi cha ghasia hiyo kati ya visababishi vingi kilikuwa ni hali ya kuona dhuluma.” Ndiyo, vikundi fulani vya rangi mara nyingi vinabaguliwa. Wanawake pia wanabaguliwa. Maskini wanabaguliwa pia, wawe ni wa jinsia gani au rangi gani.
Kwa sababu gani ulimwengu umejawa na dhuluma?