Matumizi Mabaya Sana ya Kisasa ya Uwezo
KATIKA sheria iliyotolewa kupitia Musa, Muumba alikataza kwa uthabiti upokeaji rushwa kwa upande wa mahakimu (Kutoka 23:8; Kumbukumbu la Torati 10:17; 16:19) Tunaweza kuona jinsi maagizo hayo yalivyokuwa ya hekima sana kwa kuangalia visa fulani vya kisasa vyenye kuonyesha jinsi maafisa wa serikali wanavyotumia vibaya uwezo wao.
Kisa kimoja kama hicho kilihusu Hakimu Martin T. Manton. Kule nyuma mwaka 1918 yeye alizuia jitihada za wanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, za kuwatafutia dhamana J. F Rutherford na washirika wenzake saba Wahudumu hao wanane Wakristo walishtakiwa juu ya kuzuia jitihada ya vita na wakapelekwa kwenye gereza kuu la serikali katika Atlanta, Georgia. Mahakama ya rufani yenye kusikia kesi yao ilikuwa na mahakimu watatu, kutia na Manton. Yeye alikataa, lakini mahakimu wale wawili wengine wakakubali kutoa rufani, na hukumu hiyo isiyofaa ikageuzwa
Manton alikuwa hakimu wa aina gani? Magazeti yenye kuchapisha habari yalimwita “afisa mwenye daraja la juu zaidi katika mahakama [katika United States] kufuata wale Mahakimu tisa wa Mahakama Iliyo Kuu Zaidi.” Alikuwa pia mmoja wa washiriki wa kanisa walio mashuhuri zaidi katika Amerika, hata papa akampa daraja la kuwa “Mtawa wa Mtakatifu Gregory.” Anguko la Manton lilikuja wakati alipopatikana na hatia na kuhukumiwa kutozwa faini ya dola 10,000 na miaka miwili gerezani. Kwa kufanya nini? Kwa kuuza maamuzi ya hukumu. Zaidi ya hilo, yeye alikuwa na ujasiri mno wa kudai hongo kutoka kwa wale waliosimama mbele yake, akiwaogopesha kwamba kama wao hawangemlipa pesa nyingi angewapa hukumu mbaya. Gazeti The New York Times lilisema hivi juu yake: “Hongo zilikuwa zikitoka katika nyumba ya mahakama ya Serikali.” Loo! matumizi mabaya kama nini ya uwezo wa kuhukumu!
Miaka mingi baadaye kesi nyingine mbaya sana ilitokea yenye kumhusu Spiro Agnew, aliyekuwa makamu wa rais wa United States kuanzia mwaka wa 1969 mpaka 1973. Yeye alishtakiwa kuwa akiipunja serikali maelfu ya dola, na kwa hiyo akajiuzulu. Na hivi juzi tu mwaka 1983, yeye alilipa mkoa wa Maryland dola zaidi ya 250,000 kwa sababu ya rushwa alizokuwa amepokea.
Halafu alikuwako Richard M. Nixon, aliyekuwa amechagua Agnew awe makamu wa rais. Halmashauri ya Seneti ya United States yenye kushughulikia kesi iliyohusu kashifa ya Watergate ilipendekeza kwamba Nixon ashtakiwe juu ya mambo matatu: kwamba alikuwa ametumia vibaya uwezo wake wa kirais; kwamba alizuia haki isitendwe; na kwamba alikataa kufika mahakamani alipopelekewa taarifa ya kufika mahakamani. Inaelekea wewe unajua kwamba yeye alijiuzulu Agosti 9, 1974, ikiwa imebaki miaka miwili na nusu ya urais wake.
Matumizi hayo mabaya ya uwezo yapo ulimwenguni pote. Kwa mfano, gazeti Maclean’s la Kanada la Julai 15, 1985, liliripoti juu ya “karamu zenye makelele-makelele na matendo ya ngono katika Kilima cha Bunge . . . na rushwa haramu.” Lilisimulia kwamba kwenye karamu moja afisa wa cheo cha juu wa kiserikali mwenye kusimamia wafanya kazi wengi alimwambia mwanamke mmoja wa miaka 30, hivi: “usipovua mavazi yako, hutapata kazi.”
Karibu na wakati ule ule, gazeti la habari za kimataifa lilichapisha makala “Ufisadi Wapunguza Mwendo wa Mgeuko wa Msimamo wa China.” Liliripoti hivi: “Karibu kila siku hivi majuzi, magazeti ya kiserikali yalikuwa na masimulizi yanayohusu matumizi mabaya ya fedha, mengine yakihusu maafisa wenye vyeo vya juu.”
Hivi majuzi zaidi, kichapo New Zealand Herald, chini ya kichwa: “Laana ya Ufisadi ni Tisho Kubwa Katika ‘Nchi Yenye Bahati,”’ kiliyaripoti hivi maoni ya hakimu mmoja aliyestaafu kazi: “Australia, katika miaka ya katikati ya 1980 ni tajiri, yenye uhakika na ufisadi.” Kichapo hicho kilitaja “mfumo wa hukumu ambao katika mwaka uliopita uliona hakimu mmoja wa kutoka mahakama iliyo juu zaidi nchini akitiwa korokoroni na ambao karibu kila siku unatoa ushuhuda wenye kugutusha juu ya polisi wenye ufisadi.”
Ni wazi kwamba watu hao wenye kutumia uwezo vibaya wanaipuuza kanuni hii iliyotajwa na Yesu Kristo: “Hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana.”—Mathayo 10:26