Balaamu—Ni Historia Au Ni Hadithi ya Kutungwa Tu?
KULINGANA na kitabu cha Biblia cha Hesabu, Balaamu mwana wa Beori alikuwa nabii wa kukodiwa. (Hesabu Sura 22-24) Kwa kweli, jina lake linaonekana katika vitabu vinane mbalimbali vya Biblia, kutia na barua zilizoandikwa na waandikaji wa Kikristo Petro na Yuda. Balaamu aliishi katika karne ya 15 K.W.K katika bonde la juu la Mto Eufrati. Yeye alijitokeza akodiwe na Balaki, mfalme wa Moabu, aliyemtaka atamke laana nyingi juu ya taifa la Israeli. Sasa, je! Balaamu alikuwa mtu wa kihistoria au wa kutungwa tu katika hadithi za Kiyahudi?
Kama ilivyoripotiwa katika kichapo Biblical Archaeology Review (Septemba/Oktoba 1985), wachimbuzi wa vitu vya kale wenye kufanya kazi katika Bonde la Yordani la katikati wamepata uthibitisho fulani wa kustaajabisha unaoonyesha kwamba Balaamu alikuwako kweli kweli. Wao walikuwa wakichimbua kwenye eneo la Tell Deir Alla, mwendo mfupi tu kaskazini mwa mto unaojulikana katika Biblia kuwa Yaboki, wakati walipogundua vipande fulani vya mkandiko ulioandikwa maandishi ya kale ya kisemitiki. Katika muda wa miaka michache iliyopita vipande hivyo vimeandikwa tarehe kwa uangalifu, vikaunganishwa pamoja, na maana ikafumbuliwa.
Mchunguzi Mfaransa Andre Lemaire anaeleza kwamba vipande hivyo vilipelekwa vikachunguzwe kwa njia ya rediokaboni vionekane ni vya tarehe gani na anasema: “Kulingana na uchunguzi huo, maandishi yaliyoandikwa juu yavyo yangepewa tarehe ya karibu na 800 K.W.K., kuongeza au kuondoa miaka 70.” Na maandishi hayo yanasema nini? Kulingana na yalivyoonekana baada ya Lemaire kuyaunganisha pamoja, maandishi hayo yanasema hivi kwa sehemu (herufi zilizo katika vifungo vya mraba zimewekwa ili kujazia vipande ambavyo havikuwapo):
“1. Mwandiko wa [Ba]laamu [mwana wa Beojri, mtu aliyekuwa mwonaji wa miungu. Tazama, miungu ilimjia yeye usiku na [ikasema] naye
2. kulingana na ma[n]eno hayo, nao wakamwambia [Balaa]mu, mwana wa Beori . . . naye akalia machozi
4. Kwa bidii nyingi na watu wake wakaja kwake na ku[mwambia] Balaamu, mwana wa Beori: ‘Mbona wewe unafunga na mbona unalia machozi?’ “
Inaonekana kwamba maandishi hayo yalipatikana yaweze kusomwa na watu wote yapata miaka 2,800 iliyopita, kwa sababu yalikuwa sehemu ya mwandiko wa ukutani ulio mrefu kiasi cha kutosha. Pia, ingawa kuna mapengo katika maandishi hayo, Balaamu anatajwa jina waziwazi. Hata ingawa mwandiko huo uliandikwa yapata miaka mia saba baada ya matukio yenyewe, ni wazi kwamba Balaamu alikubaliwa kuwa mtu wa kihistoria na nabii.
Maandishi hayo ya ukutani ni ya miaka mia kadha karibu zaidi na wakati wa matukio yanayosimuliwa katika Biblia kuliko zile hati za zamani zaidi zinazopatikana kwa sasa. Hayo ni kisehemu kingine kinachoongezea ushuhuda wa kuthibitisha kwamba Biblia inatoa habari yenye kutegemeka juu ya historia ya kale.—2 Timotheo 3:16, 17.