“Madhara Yaliyofanywa Yatakuwa Makubwa Mno”
VITA ya Ulimwengu ya Kwanza ilileta hasara kubwa mno katika maisha za binadamu na mali. Hata hivyo, jambo lisilojulikana sana ni madhara ambayo vita hiyo ilifanya kwa sifa ya wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo katika Afrika. Kulingana na mmisionari Mkatoliki Francis Schimlek katika kitabu chake Medicine Versus Witchcraft, habari za moto mkubwa wa duniani pote “ulikuwa kama tetemeko la dunia, mtetemo ambao ulihisiwa mbali sana kufikia kituo cha mwisho cha misheni katika msitu wa Afrika. . . . Wajumbe wa Kristo walitahayarika, na Wakristo Wenyeji walitatizika.”
Sababu gani hivyo? Schimlek ananakili mmisionari Albert Schweitzer kuwa akieleza hivi “Sisi sote, tunafahamu kwamba wenyeji walio wengi wanatatizika juu ya swali la jinsi gani ingewezekana kwamba weupe, walioleta Gospeli ya Upendo, sasa wanauana makusudi, na kutupilia mbali amri za Bwana Yesu. Wanapotuuliza swali hilo sisi tunakuwa hoi. . . . Mimi naogopa kwamba madhara yaliyofanywa yatakuwa makubwa mno.”