“Sasa Sisi Tuna Jumba la Ufalme Letu Wenyewe”
MENGI yamechapishwa juu ya Majumba ya Ufalme yenye kujengwa haraka katika nchi kama vile Uingereza, Kanada, na United States. Hata hivyo, usiojulikana sana ni uhakika wa kwamba mahali palipojengwa kwa haraka pa ibada ya Mashahidi wa Yehova pamesimamishwa kwa makumi ya miaka katika zile zenye kuitwa nchi zinazositawi.
Katika mabara ya Kiafrika Mashahidi wa mahali hujenga mara nyingi majengo ya muda tu kwa ajili ya mikusanyiko ya wilaya kwa muda wa majuma machache tu. Haya yametumika si kuwa mahali pa mikutano na kinga ya jua kali la kitropiki tu bali pia yamekuwa malazi ya wajumbe. Maono kama hayo yaweza kusimuliwa juu ya Amerika ya Kati.
Kwa kielelezo, katika Jiji la Guatemala, Guatemala, mchango wa dola 200 ulipelekwa kwenye Kundi la Vivibien la Mashahidi wa Yehova. Shahidi wa huko alipotoa kipande cha ardhi katika eneo la mashambani, Mashahidi waliamua kutumia mchango huo kujenga jengo la kiasi ambalo lingeweza kutumiwa kwa ajili ya mikutano yao.
Mianzi ingetumiwa kwa ua wa kuzungushia boma hadi kimo cha meta 1.5; juu ya hapo ilikuwako nafasi wazi ya kuingizia hewa. Iliamuliwa kwamba jengo hilo liwe na ukubwa wa meta 4 kwa meta 6. Wazee wa kundi walipozuru uwanja huo, walishangaa kupata mbele ya kipande cha ardhi hiyo vichaka kadhaa vya mianzi, yenye kimo cha meta 6 hadi meta 9 na yenye kipenyo-duara cha kuanzia sentimeta 8 hadi sentimeta 13. ‘Kwa nini tusilijenge Jumamosi ijayo?’ wakauliza.
Usiku wa Jumatano iliyofuata, mipango ya ujenzi ilifanyizwa. Alhamisi ndugu mmoja akanunua mabati, mwingine akanunua mbao, na mwingine misumari. Kufikia alasiri ya Alhamisi mbao zilikatwa mapema ziwe za urefu wenye kutakiwa, nao wakaanza kufanyiza maboriti ya fremu ya muundo wa A pamoja na mabamba ya chuma yaliyochangwa. Kufikia usiku wa Ijumaa maboriti yalikuwa tayari.
Mapema asubuhi ya Jumamosi, lori liliburuta maboriti hayo na mbao nyinginezo, vifaa vya paani, na misumari hadi kijijini. Magari manne yalisafirisha wanaume, wanawake, na watoto 50 hivi kwenda kijijini. Kufikia saa 2:00 asubuhi wote wakawa wamewasili.
Mashimo yaliyotobolewa katika mwamba mgumu wa kivolkeno ndiyo yaliyoingizwa nguzo zile kubwa zenye kusimamishwa wima. Kabla ya hapo, kutoka kwa mwenye mianzi Mashahidi walinunua mashina 50 ya mianzi kwa senti 12 kila mmoja [za United States]—malipo ya jumla ya dola 6. Kwa haraka, panga zikaiangusha chini mianzi hiyo. Mianzi hii ilikatwa kwa misumeno ya mkono iwe na urefu wa meta 1.5 na ikapasuliwa katikati hadi chini.
Maboriti yalipokuwa yakiwekwa mahali payo, mikono mingine ilikuwa ikipigilia misumari kwenye papi zilizokingama, nusu moja kwa nje na nusu moja kwa ndani, hivi kwamba hiyo mianzi mviringo ya kuvutia ipambe kuta za ndani na pia za nje. Halafu, paa ikawekwa huku wengine wakianza kuleta mawe na udongo wa kutandaza sakafu ile ya udongo. Jengo hilo lililofanywa kwa saa 12 lilimalizwa kabla haijawa giza, na akina ndugu wakarudi nyumbani kwao jijini wakiwa na mioyo yenye shangwe.
Baadaye, majani-sindano ya msunobari yalitandazwa kila mahali kwenye sakafu ya udongo, na viti fulani vya kukunja na vikalio virefu vilivyofanyizwa kwa mianzi ambayo haikutumiwa vikasimamishwa. Sasa Jumba la Ufalme likawa tayari kwa mkutano wa kwanza.
Katika mabara mengi ya zile tropiki—Afrika, visiwa vya Pasifiki na Karibea, Esia, Meksiko, Amerika ya Kati na ya Kusini—ambako labda huishi Mashahidi wa Yehova milioni moja, majengo hayo sahili yamewaletea shangwe Mashahidi wa huko kwa sababu wangeweza kusema: “Sasa sisi tuna Jumba la Ufalme letu wenyewe.”