Jina la Mungu Larudishwa
“IMECHUKUA karibu muda wa miaka 60 ili jina la Mungu, ‘YHWH,’ ambaye ndiye Mungu si wa Wayahudi tu bali pia wa Wakristo, lirudishwe mahali ambapo mpakaji rangi aliliweka awali.” Hivyo ndivyo gazeti la Kijerumani Schwarzwälder Bote linavyoeleza juu ya kurudishwa kwa jina la Mungu kwenye upande wa mbele wa jumba la baraza la mji katika Horb, kusini mwa Ujerumani. Lakini ni kwa nini jina hilo liliondolewa?
Gazeti hilo laripoti kwamba upande wa nje wa jumba la baraza la mji ulikuwa umepakwa rangi kwa urembo kukiwa na mandhari za picha zikipamba upande wa mbele. Tetragramatoni ilikuwa imetiwa ndani pia, zile herufi nne za Kiebrania zinazoonyesha jina la Mungu.
“Jina hilo linalotokea mara zaidi ya 6,000 katika Biblia,” gazeti hilo laendelea, “ni ‘Yehova’ au jambo sawa na hilo katika Kijerumani. Matamshi sahihi hayajulikani wazi kwa sababu Kiebrania cha kuandika kilikuwa chenye konsonanti tu. Irabu ziliongezwa na msomaji.”
Hata hivyo, katika 1934 wawakilishi wa Chama cha Nazi waliamua kwamba Tetragramatoni “haikupatana na itikadi iliopo” na kwa hiyo yapasa kupakwa rangi juu yayo. Kwa furaha, sasa Tetragramatoni imerudishwa. Gazeti hilo laeleza hivi: “Leo upande wa mbele [wa jumba la baraza la mji], wenye kupambwa kwa mandhari za kihistoria, alama za mji, na picha za watu, ni mahali papasapo kuonwa katika Horb.”