Zaidi ya Kuwa Nguzo Zenye Kuchochea Udadisi
Wageni huchochewa na nguzo katika Bahari ya Mediterania kule Kaisaria, bandari ya kale kwenye pwani ya Israeli. Herode Mkuu alijenga bandari hiyo na kuupa mji huo jina kwa heshima ya Kaisari Augusto.
Wanaakiolojia wamefukua sehemu kubwa ya mji huo, kutia na jumba lao la michezo lililokubwa sana. Wameingia majini pia ili kupata mwono-ndani kuhusu jinsi majengo ya bandari yalivyojengwa ukingoni mwa mchanga.
The New York Times (Januari 8, 1991) liliripoti uvumbuzi wa nguzo katika mabaki ya jumba la mfalme ambalo zamani lilitokeza kuelekea baharini. Hizo ni za kipekee katika njia ya kwamba maandishi juu yazo hutaja magavana wa Roma ambao hawakujulikana kabla ya hapo. “Mwangalizi” wa meli atajwa pia, huo ukiwa “mwandiko wa kwanza unaohusika na bandari.”
Wanafunzi wa Biblia wajua kwamba mtume Paulo alisafiri kwa meli hadi bandari hiyo mwisho-mwisho wa safari mbili za umishonari. Huko alikaa pamoja ya Filipo mwevanjeli, na ni lazima maono yake yawe yaliwatia moyo sana wanafunzi. (Matendo 18:21, 22; 21:7, 8, 16) Twaweza kusoma mengi ya hayo maono yenye kusisimua katika kitabu cha Biblia cha Matendo ya Mitume.
Kwa hiyo nguzo hizo zilizo ukingoni mwa bahari si mabaki tu ya historia yasiyo na thamani. Zinawakumbusha Wakristo juu ya ndugu zao wa mapema, walioeneza habari njema kwa bidii katika bandari mbalimbali na kuelekea “mifikio ya mbali sana ya dunia.”—Matendo 1:8, NW.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Garo Nalbandian