Wanaweza Kujifunza Kutoka kwa Nyuki
“Katika miaka ya karibuni, wahandisi na wabuni wa vitu wametambua jambo ambalo yaelekea nyuki wamejua wakati wote: kugeuza kifaa hata kile kilicho chembamba sana kuwa umbo la sega lenye pande sita hufanya sega liwe na nguvu zaidi ya vile linavyoweza kuwa kwa namna nyingineyo.”—The New York Times, Oktoba 6, 1991.
HAISHANGAZI kwamba wanadamu wanaweza kufaidika na uchunguzi wa makini wa wadudu. Mtu mmoja wa kale mwenye imani, Ayubu, alisema hivi: “Lakini sasa waulize hao wanyama, nao watakufundisha; na nyuni wa angani, nao watakuambia . . . Katika hawa wote ni yupi asiyejua, kwamba ni mkono wa BWANA [Yehova, NW] uliofanya haya?” (Ayubu 12:7-9) Naam, hekima ya Muumba imedhihirishwa wazi na vitu vya kawaida kama vile vijumba vya sega la nyuki vyenye pande sita.
Ingawa kuta za nta za vijumba hivyo huwa na unene wa sehemu moja kwa tatu ya milimeta, ni zenye nguvu sana. Kwa hakika, zinaweza kustahimili uzito ulio mara 30 zaidi yao.
Nguvu hiyo yaweza kutumiwa katika matumizi ya kawaida, kama vile kulinda vifaa dhidi ya kugongwa na kuharibika. Hata hiyo hutumika kulinda vifaa vya kijeshi vinavyoangushwa chini kutoka kwa ndege. The New York Times husema juu ya hilo: “Vitu vyenye uzito wa gari la jip hufungamanishwa na mbao zenye vipande vya sega la asali chini yayo ili kukinza dhidi ya pigo la kuanguka.”
Vitu vilivyotengenezwa na mwanadamu vikiwa na muundo huo vyaweza kufanyizwa kutoka kwa vifaa vingi. Inaonekana kuwa ile iliyo ya kawaida sana ni karatasi. Karatasi ya nailoni na utomvu wa miti hutumiwa kufanyiza sega ambalo hutumiwa kwenye viunzi vya ndege kubwa. Nguvu nyingi hupatikana kwa uzito ulio mdogo sana kwa kulinganisha. Kwa nini? Hewa ndio huchukua nafasi kubwa kati ya vibao, kwa hiyo kuna uzito mdogo. Hewa ina uwezo mzuri wa kuhami pia.
Nyuki wa kawaida ‘hajui’ kikweli juu ya hayo yote, kwani hana shahada ya uhandisi. Na bado, kila siku yeye hufanya kazi yake akiwa na hekima ya kisilika aliyopewa na Muumba, Yehova.