Wakati wa Kumtafuta Mungu
PICHA iliyoko kwenye ukurasa huu ni ya Akropoli (sehemu ya mji yenye kuta) ya Athene, iliyokuwa wakati mmoja kitovu cha ibada ya miungu na miungu-wake wengi. Areopago, iliyosemwa kuwa ndipo mahali mahakama ya haki ilipokuwa katika nyakati za kale, iko kwenye sehemu ya chini ya Akropoli hiyo. Hapo ndipo mahali mtume Paulo aliposimama na kutoa hotuba yenye kutokeza kweli kweli, miaka 2,000 hivi iliyopita. Yafuatayo ni baadhi ya mambo aliyosema:
“[Mungu] alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu.”—Matendo 17:26-28.
Historia ingalikuwa tofauti kama nini ikiwa ainabinadamu kwa ujumla ingalitii maneno ya Paulo! Ni vita vingi kadiri gani, ni kuteseka kwingi kadiri gani, kungezuiwa ikiwa wanadamu wangalitambua masilahi yao wakiwa wazao wa mwanadamu mmoja aliyeumbwa na Bwana Mwenye Enzi Kuu, Yehova.
Leo, ainabinadamu imejawa na utaifa, migawanyiko ya kijamii, chuki za kirangi, na uonevu wa kijamii. Hata hivyo maneno ya Paulo bado hutumika. Sisi sote tu wazao wa yule mtu mmoja aliyeumbwa na Mungu. Sisi sote, kwa maana hiyo, ni ndugu na dada. Na bado hakujawa kuchelewa mno kumtafuta Mungu akiwa bado aweza kupatikana.
Maneno ya Paulo huwa na maana yenye uzito hata zaidi tunapofikiria maneno ya mwisho ya hotuba yake. Alisema hivi: “[Mungu] ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.”
Ufufuo wa Yesu ni jambo hakika la kihistoria, na kama Paulo aonyeshavyo, huo ni uthibitisho kwamba kutakuwa siku ya hukumu kwa ainabinadamu. Wakati gani? Twajua kwamba wakati huo ni miaka 2,000 hivi karibu zaidi ya wakati ambapo Paulo alisimama kwenye Areopago na kutamka maneno hayo. Kwa kweli, utimizo wa unabii wa Biblia huonyesha kwamba wakati huo u karibu sana. Hilo ni wazo lenye kuleta fikira nzito kama nini? Ni jambo la hima kama nini kwamba tumtafute Mungu kwa unyofu wote, kwa kuwa, kama Paulo alivyowaambia Waathene, “sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu”!—Matendo 17:30, 31.