Kutoka Kuwa Hospitali ya Kihistoria Hadi Kuwa Jumba la Ufalme la Aina Yalo
KATIKA 1770 mvumbuaji wa nchi Mwingereza Luteni James Kuk alikuwa akiendesha ile meli yenye uzani wa tani 369 iitwayo Endeavour karibu na pwani ya mashariki mwa Australia isiyokuwa imetembelewa na wavumbuaji wa nchi. Katika jioni ya Juni 11, chombo hicho kilikwama kwenye miamba ya matumbawe katika eneo la mbali kuelekea kaskazini mwa bara hilo. Chombo hicho kilichofanyizwa kwa mti wa oaki kilikuwa kimeharibika vibaya sana. Kilihitaji kutengenezwa kwa hima ikiwa mabaharia hao wangeokoka. Mwingilio wa mto uliokuwa karibu ulithibitika kuwa mahali pafaapo pa kufanyia marekebisho hayo, yaliyochukua majuma sita. Miaka mia moja na tatu baadaye, dhahabu ilivumbuliwa katika eneo hilo. Wengi wakaanza kuhamia kwa haraka eneo hilo lenye dhahabu! Makumi ya maelfu walikuja kutafuta utajiri wao. Mji Kuktauni ukazaliwa.
Katika 1879 ruhusa ya serikali ilitolewa ya kujenga hospitali yenye kudumu ili kuwatunza wagonjwa na wale waliojeruhiwa katika aksidenti zilizotokea wakati wa kuchimba dhahabu. Katika mwaka uo huo, kwa upande ule mwingine wa ulimwengu, chapa ya kwanza ya Zion’s Watch Tower ilitokea Julai 1. Tangu wakati huo, gazeti hilo limeandaa programu kwa ajili ya afya ya kiroho ya mamilioni ya watu wanaomcha Mungu. Wakati huo haikujulikana kwamba ujenzi wa hospitali ya Kuktauni ungehusika kwa ukaribu na gazeti hilo.
Baada ya karne zaidi ya moja, Hospitali ya Kuktauni ilihitaji kujengwa upya. Fedha za serikali zilikuwako za kujenga jengo jipya, kwa hiyo mwaliko ulitolewa kwa wowote waliotaka kuhamisha jengo hilo la kale la hospitali hiyo. Lile shirika la Kwinzlandi, Australia linalohifadhi majengo ya zamani lilionyesha kupendezwa sana na jengo hilo la kihistoria. Hata hivyo, gharama iliyohusika katika kulihamisha jengo hilo mahali penginepo na kulirekebisha ilithibitika kuwa kubwa mno. Hakuna wowote waliojitolea kufanya hivyo.
Karibu na wakati huo, lile kundi dogo la Mashahidi wa Yehova katika Kuktauni lilikuwa likitafuta mahali pa kudumu pa kufanyia mikutano ya Kikristo. Halikuwa na shamba lolote nalo lilikuwa na dola za Australia 800 tu. Lingeweza kujengaje Jumba la Ufalme? Wawakilishi wa kundi la mahali hapo walijitolea kuhamisha jengo hilo la hospitali na hawakutoa malipo yoyote. Yehova angeelekezaje mambo? Habari zenye kusisimua! Toleo lao lilikubaliwa!
Sasa kwa jambo lililofuata—shamba la kuwekea jengo hilo. Naam, waliambiwa kwamba ilionekana kana kwamba shamba la serikali huenda likapatikana bila gharama yoyote, maadamu jengo hilo lilihifadhiwa na kurekebishwa. Hata hivyo, kufikia wakati huo upinzani dhidi ya mradi huo ulikuwa ukiongezeka katika sehemu ya jumuiya yenye chuki. Lalamiko lilitayarishwa lililokusudiwa kukomesha mipango ya Mashahidi. Uvumi ulienezwa kwamba Mashahidi wa Yehova wangetwaa uongozi wa Kuktauni, wangefunga mahoteli yote na mahali-mahali pa kuchezea kamari, na wangekataza uuzaji wa tumbaku. Bila shaka, hilo halikutukia, lakini kulizidi kuwa vigumu kupata ugawanyaji upya wa mashamba na kupata vibali vilivyohitajiwa kwa ajili ya ujenzi. Tarehe ya mwisho ya kuondoa jengo hilo ilikuwa ikikaribia kwa haraka. Walitafuta msaada kutoka kwa Serikali ya Majimbo ya Kwinzlandi. (Linganisha Warumi 13:2) Ruhusa ya kutumia shamba la serikali wakapewa kwa haraka, na idhini ya ujenzi ikatolewa. Wakiwa na shamba na jengo pia, ni jambo gani linalofuata?
Kikundi chawasili cha mamia ya Mashahidi, mafundi wenye ujuzi na wasaidizi kutoka sehemu mbalimbali za Jimbo la Kwinzlandi, wanaotoa wakati wao kwa hiari na ambao wamesitawisha ustadi wa kujenga Majumba ya Ufalme kwa haraka. Mradi huo ulikuwa na matatizo ya pekee: kuhamisha sehemu mbalimbali za hospitali hiyo yenye orofa mbili hadi mahali papya na kisha kuijenga tena. Majira ya kusi yalikuwa yakikaribia kwa haraka, yakitisha kuleta mvua nyingi sana. Je! kazi ingekamilishwa kabla ya wakati huo? Baadhi ya wakazi wa mji huo walishuku hilo. Hata hivyo, jambo lililoonekana kutowezekana kwa wengine lilitimizwa upesi. Katika Aprili 1986 jengo hilo lilihamishwa na baadaye kurekebishwa kwenye uzuri walo wa awali.
Utendaji huo wote haukupita bila kutazamwa, kama ilivyo wazi kutokana na maelezo katika Anglican Newsletter katika Kuktauni. Ilitaarifu hivi kwa sehemu: “Bila shaka nitachambuliwa, lakini . . . ebu angalia kotekote Kanisani na uone jinsi isivyojaa na ebu kiangalie kile kikundi kingine cha watu [Mashahidi wa Yehova] na uone jinsi kinavyozidi kujaa . . . , kinajazwa Waanglikana na Wakatoliki wa Kiroma . . . Je! ulijua kwamba tengenezo fulani . . . [lime]nunua ile Hospitali ya zamani ili kuijenga upya kuwa jengo liwezalo kuitwa kanisa kwa sababu ile Shule walimokutania ni ndogo mno kwao wote? . . . Tumekuwa dhaifu kama nini, kuruhusu jambo hilo litukie.”
Maelfu ya watalii huzuru Kuktauni kila mwaka. Wao huja ili kuona ile mandhari yenye kupendeza ya msitu wa mvua na ile Miamba Mikubwa ya Kizingiti na kujifunza juu ya historia ya eneo hilo. Jumba la Kuhifadhi la Kapteni Kuk ni mahali panapovutia wageni wengi. Tangu 1989 Hospitali ya Kihistoria ya Kuktauni ikiwa sasa Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova imekuwa pia mahali panapovutia watalii wengi. Maduka yanayouza vitu vya ukumbusho huuza vitambaa vya kupanguzia vyombo na T-shati zenye picha ya Hospitali-Jumba la Ufalme la Kuktauni juu yazo. Wakati wa majira ya watalii, watu kati ya mia sita na elfu moja huzuru jengo hilo kila juma na kujionea wenyewe ujenzi walo wa pekee wa 1879.
Gazeti linalojulikana sasa kuwa Mnara wa Mlinzi hupatikana kwa wageni kwa wingi. Tangu 1879 mweneo wa gazeti hili limeongezeka kufikia nakala zaidi ya milioni 15 mara mbili kwa mwezi katika lugha 111. Linaelekeza watu kwenye ahadi ya Biblia kwamba wengine katika kile kizazi cha 1914 watakuwa hai kuona afya njema ya kimwili na ya kiroho ikirudishiwa ainabinadamu. (Isaya 33:24) Dunia nzima itageuzwa kuwa paradiso na mamilioni ya watu wenye kujitolea kwa hiari. (Zaburi 37:29) Kwa nini usitembelee Jumba la Ufalme moja lililo karibu na wewe? Utapata kitu chenye thamani kubwa zaidi kuliko ile dhahabu yote iliyochimbwa katika eneo la Kuktauni.—Mithali 16:16.