Kutabiri Juu ya Wakati Ujao wa Uchumi wa Ulimwengu
UKOSEFU wa uthabiti wa masoko ya kiuchumi na ukosefu wa uhakika katika wachanganuzi walioshindwa kutabiri lile anguko la soko la hisa katika 1987 umewafanya baadhi ya wafanya biashara wageukie unajimu ili kutabiri wakati ujao wao wa kifedha, ladai gazeti la London Accountancy Age. Gazeti hilo lasema kwamba “Wanajimu wa kifedha wanazidi kupata wateja wengi mashuhuri wanaotaka utabiri mbalimbali wenye kutia mambo mengi kuhusu mauzaji.”
Mnajimu mmoja alinganisha zile kawaida anazopata katika miaka 30 ya data ya kifedha ya kila siku na mwendo wa sayari. Yeye hutoa utabiri wake kwa msingi huo. Ingawa wateja wengi walisita kufuata shauri lake kabla ya 1987, sasa aona kwamba hata wafanya biashara washupavu wako tayari kusikiliza.
Mnajimu mwingine wa kifedha hutoa chati zenye kutegemea tarehe za kuzaliwa ili kuchanganua tabia ya mtu na pia ili kujaribu kupata “vidokezo vya wakati unaoelekea kuwa wa maendeleo ya kibiashara.” Mwingine bado huamini kwamba kubadilika-badilika kwa mauzaji ya fedha hufuata kawaida za mwezi. Lakini anapolinganishwa na wachanganuzi wa kifedha wa kawaida, mnajimu huyo aona kwamba wateja wake “humpatia nafasi ndogo sana ya kutokuwa sahihi.”
Hata hivyo, kuna utabiri mmoja wa kifedha utakaotimizwa kwa hakika, na hauhusiki hata kidogo na unajimu. Utabiri huo umeandikwa katika Biblia na kupuliziwa na Yehova, Mungu ambaye hajipatii nafasi yoyote “ya kutokuwa sahihi.” Yeye ndiye Mungu “asiyeweza kusema uongo.” (Tito 1:2) Alimwamuru nabii wake Ezekieli ajulishe rasmi hivi: “Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa.”—Ezekieli 7:19.
Hilo litatukia wakati gani? Wakati wa ile “dhiki kubwa” inayokuja iliyotabiriwa na Yesu Kristo, ambayo Ezekieli aliita “siku ya ghadhabu ya BWANA [Yehova, NW].” (Mathayo 24:21; Ezekieli 7:19) Ufanisi wa kifedha hautathibitisha wokovu, yajapokuwa yale ambayo huenda wanajimu wakatabiri. Ni kutumaini tu katika Yehova Mungu, yule Mkombozi Mkuu, kutakakohakikisha usalama wakati wa msukosuko huo wa ulimwengu ambao katika huo ufisadi wote utaondolewa—wa kisiasa, wa kidini, na wa kibiashara.—Mithali 3:5, 6; Sefania 2:3; 2 Petro 2:9.