“Maua ya Mashamba”
UKOSEFU wa kazi za kuajiriwa. Bei zenye kupanda. Umaskini. Mshuko wa hali ya kiuchumi. Maneno hayo hutokea mara nyingi zaidi katika taarifa za habari. Nayo huonyesha magumu ambayo mamilioni hukabili wanapojaribu kulisha na kuvika familia zao nguo na kuwa na mahali pa kuishi.
Waamini na wasioamini pia huathiriwa. Lakini waamini hawaachwi peke yao wakabili matatizo hayo. Yesu, alipokuwa akisema na watu wanyenyekevu wa karne ya kwanza, alisema hivi: “Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! si bora kupita hao?”—Mathayo 6:26.
Yesu alisema hivi pia: “Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, . . . je! hatazidi sana kuwavika ninyi?”—Mathayo 6:28-30.
Je! hilo lamaanisha kwamba Mkristo hahitaji kufanya kazi ili ajiruzuku? Hasha! Mkristo hufanya kazi kwa bidii iwezekanavyo ili kuzilipa gharama zake. Mtume Paulo alisema hivi: “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.” (2 Wathesalonike 3:10) Hata hivyo, Mkristo hutambua utunzaji wa Mungu wenye upendo na ana imani kwamba Baba yake wa kimbingu humwangalia. Hivyo, haondoshwi kwenye usawaziko na mahangaiko ya maisha. Hata katika nyakati ngumu, yeye huweka mambo ya kwanza—mambo ya kiroho—kwanza. Anaamini maneno haya ya Yesu: “Utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”—Mathayo 6:33.