Maji ya Uhai
“NAYE asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima [uhai, NW] bure.” (Ufunuo 22:17) ‘Maji ya uhai’—hayo yanamaanisha maandalizi yote ya Mungu kwa ajili ya wokovu wetu kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo. Maandalizi hayo yanapatikana, na ni ya bure. Huo ni ukarimu wa ajabu kama nini kwa upande wa Mungu! Lakini, kwa nini yanafananishwa na maji?
Maji halisi huwezesha ukuzi wa mimea udongoni, na hilo huwezesha uhai wa kibinadamu. Bila maji, uhai wa mimea, na hivyo uhai wa kibinadamu, hauwezi kuwako. Zaidi ya hayo, asilimia 65 ya mwili wako ni maji. Wastadi wengine wa afya hudokeza kudumisha uwiano huo kwa kunywa lita 2.4 za maji kwa siku. Taratibu zako zote za uhai mwilini—kutoka kusaga chakula hadi kuondosha takataka mwilini—zinahitaji maji. Usipokunywa maji kwa juma moja, utakufa.
Vivyo hivyo, ‘maji ya uhai’ huwezesha na kutegemeza uhai wa kiroho. Tukikatalia mbali maji ya uhai, hatuna wakati ujao wenye kudumu. (Yohana 3:36) Tukiyakubali, tunaweza kupata uhai wa milele. Haishangazi kwamba yule mwanamke Msamaria aliitikia kwa kupendezwa wakati Yesu alipomwambia hivi: “Ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima [uhai, NW] wa milele”! (Yohana 4:14) Na tujitahidi kwa bidii tufikie kuyatwaa maji ya uhai bure.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Garo Nalbandian