Sambamba kwa Muda wa Miaka Kumi!
ALIPOULIZWA jinsi alivyohisi miaka kumi iliyopita wakati chapa ya Kihispania ya Mnara wa Mlinzi ilipoanza kuchapishwa sambamba na chapa ya Kiingereza, dada mmoja mpendwa Mhispania aliitikia hivi: ‘Twahisi ni baraka kwa sababu sasa tulikuwa, mwasemaje, sambamba na Kiingereza. Nisemapo Kiingereza, sikuzote mimi hufikira juu ya tengenezo. Sisi hurejezea tengenezo hilo kuwa “Mama.” Twahisi tukiwa na ushirika wa karibu sana. Ni wenye kupendeza. Ni mzuri ajabu!’
Dada huyo mwaminifu alieleza hisia za wasomaji wengi ambao hawasomi Kiingereza. Katika miaka iliyopita, makala zilitokea katika chapa ya Kihispania ya Mnara wa Mlinzi karibu miezi sita baada yazo kuchapishwa katika Kiingereza. Lugha nyinginezo zilikuwa zimechelewa vivyo hivyo. Kwa kueleweka, katika lugha nyingi kulikuwa na tamaa kubwa sana ya kuchapisha habari ileile, kwa wakati uleule.
Kwa hiyo kuanzia na toleo la Aprili 1, 1984, chapa ya Kihispania ilikuwa ya kwanza kuchapishwa sambamba na chapa ya Kiingereza. Lugha nyinginezo zilifuata upesi. Kuanzia mwanzo wa 1985, chapa katika lugha 23 zilikuwa sambamba. Watafsiri walipopatikana na kuzoezwa, chapa katika lugha nyingine zaidi zilianza kuwa sambamba na Kiingereza.
Toleo hili la Mnara wa Mlinzi latia alama mwaka wa kumi tangu uchapishaji wa sambamba. Sasa Mnara wa Mlinzi linachapishwa katika lugha 116, kati ya hizo 85 huchapishwa sambamba. Hilo lamaanisha kwamba asilimia 99.3 ya wastani wa ujumla wa nakala 16,100,000 za Mnara wa Mlinzi zinazochapishwa zina picha ya jalada na makala zilezile. Kati ya wale wanaohudhuria Funzo la Mnara wa Mlinzi la kila juma, zaidi ya asilimia 95 huzungumzia habari ileile kwa wakati uleule.
Amkeni!, gazeti jenzilo la Mnara wa Mlinzi, huchapishwa sambamba katika lugha 37 kati ya lugha zalo 74. Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova kinachapishwa katika lugha 18. Uchapishaji wa sambamba hutumikia kuunganisha watu wa Mungu “katika nia moja na shauri moja.”—1 Wakorintho 1:10.