Ubuni—Zawadi ya Ukarimu Kutoka kwa Mungu
YEHOVA hupata shangwe katika kazi zake za ubuni. (Zaburi 104:31) Uradhi wenye kina apatao kutokana na tendo la kuumba unaonyeshwa katika Mwanzo 1:31: “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.”
Yehova hakujiwekea shangwe hii. Alimpa Yesu pendeleo la kuwa mjumbe, au chombo, ambacho kukipitia vitu vingine vyote viliumbwa. (Yohana 1:3; Wakolosai 1:16, 17) Akiwa “stadi wa kazi,” Yesu pia alikuwa “furaha sikuzote mbele ya [Yehova].”—Mithali 8:30, 31, NW.
Lakini uwezo wa kubuni haupo mbinguni pekee. “Umewekwa ndani ya jamii ya binadamu,” aandika Eugene Raudsepp katika kitabu chake How Creative Are You? Hili si tukio lisilotazamiwa, maana mtu aliumbwa kwa sura ya Mungu. (Mwanzo 1:26) Hivyo Yehova amewapa wanadamu uwezo wenye kuridhisha wa ubuni.—Yakobo 1:17.
Basi, si ajabu kwamba Biblia husifu sana kuimba, kucheza dansi, kusokota, upishi, ufundi stadi, na jitihada nyinginezo za ubuni. (Kutoka 35:25, 26; 1 Samweli 8:13; 18:6, 7; 2 Mambo ya Nyakati 2:13, 14) Bezaleli, fundi stadi, alitumia kipawa chake katika ‘kubuni kazi za ustadi’ ili asaidie katika kujenga tabenakulo. (Kutoka 31:3, 4) Yule mchungaji Jabali huenda ndiye aliyebuni hema, ubuni unaofaa kwa maisha ya kuhama-hama. (Mwanzo 4:20) Daudi hakuwa mwana-muziki na mtungaji tu, bali pia mtengenezaji wa vinanda vipya vya muziki. (2 Mambo ya Nyakati 7:6; Zaburi 7:17; Amosi 6:5) Miriamu huenda akawa ndiye aliyetunga dansi ya shangwe iliyoadhimisha kuokolewa kwa Waisraeli kimuujiza kupita Bahari Nyekundu.—Kutoka 15:20.
Ubuni mara nyingi ni kipawa kinachoendeleza ibada ya kweli. Kwa ubuni Yesu alitoa vielezi na mifano ya vitu vinavyoonekana ili kuwasilisha ujumbe wake. Wafuasi wake vilevile wanahimizwa ‘wafanye kazi kwa bidii katika kusema na kufundisha.’ (1 Timotheo 5:17, NW) Ndiyo, kazi yao ya kuhubiri si jambo la kawaida tu. Ni ufundi unaohitaji njia za ubuni za kufundisha. (Wakolosai 4:6) Hili ni muhimu hasa mmoja anapofundisha watoto wake.—Kumbukumbu la Torati 6:6, 7; Waefeso 6:4.
Hivyo, Yehova hushiriki na wengine shangwe ambayo kubuni humletea. Zawadi ya ukarimu kama nini!