Wanawake Ulimwenguni Pote
WANADAMU wawili wa kwanza walipoasi dhidi ya Mungu, Yehova alitabiri matokeo yenye msiba ambayo yangewapata wao na wazao wao pia. Yehova alimwambia Hawa hivi: “Tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” (Mwanzo 3:16) Biblia hutia moyo kwa mkazo sana heshima ya kina kwa wanawake, na mamilioni ya wanawake hufurahia maisha yenye furaha, yenye kuridhisha zaidi kwa sababu wao na familia zao hutumia kanuni za Biblia.
Hata hivyo, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya haki za kibinadamu, wanawake wengine wengi ulimwenguni pote wanaonewa, wananyanyaswa, na kushushwa. Likitoa maelezo juu ya ripoti hiyo, International Herald Tribune lasema hivi: “Katika maelezo yenye kuhuzunisha, ripoti ya nchi 193 . . . inaeleza mambo ya kusikitisha ya kuwaonea na kuwatendea vibaya wanawake siku kwa siku.”
Hapa kuna vielelezo vichache: Katika Afrika ya kati, ni lazima wasichana wafanye nyingi ya kazi ngumu ya kulima, na theluthi moja tu ndio huenda shule ikilinganishwa na wavulana. Katika nchi moja huko, uzinzi ni kinyume cha sheria kwa wanawake lakini si kwa wanaume. Sheria ya nchi nyingine ya Afrika inamwachilia mume anayemuua mkeye akipatikana akifanya uasherati, lakini sheria hiyo haimwachilii mke anayemuua mumeye akipatikana akifanya tendo hilohilo.
Ripoti yasema kwamba katika sehemu fulani ya Amerika Kusini, polisi hawawahurumii wanawake ambao wamepigwa. Na ni lazima wanawake walioajiriwa mara nyingi waridhike na mshahara mdogo wa asilimia 30 hadi 40 kuliko wanaume.
Katika sehemu za Asia, wanawake hulazimishwa kufunga uzazi na kutoa mimba. Katika nchi moja, kuna makahaba wapatao 500,000, wengi wao wakiwa wameuzwa na wazazi wao wafanye hivyo kwa kusudi la pesa za kununua nyumba mpya. Polisi katika nchi nyingine lazima wakabili visa vyenye kuenea vya “vifo vya mahari”—mke huuawa na mumeye au na familia yake kwa sababu mahari yake haikufikia ile waliyotazamia.
Kuhusu Yesu Kristo, Biblia hutuhakikishia hivi: “Atamwokoa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, na damu yao ina thamani machoni pake.” (Zaburi 72:12-14) Hivyo tuna sababu nzuri ya kuwa na maoni yanayofaa; wanawake ulimwenguni pote wanaweza kutazamia mbele kwenye hali zilizoboreka zitakazokuwapo wakati huo.