Kitabu cha Nyimbo Akipendacho Zaidi Irina
MUDA usio mrefu uliopita, Irina, msichana mwenye umri wa miaka tisa kutoka Sofia, Bulgaria, alibatizwa akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Yeye hupenda kuimba na hasa yeye hufurahia nyimbo zilizo katika kitabu Mwimbieni Yehova Sifa. Basi Irina aliweka mradi wa kukariri moyoni nyimbo chache kila mwezi.
Mojawapo masomo Irina ayapendayo shuleni ni muziki. Kwa hiyo mwalimu wake wa muziki alishangaa Irina alipokataa mwaliko wa kuimba katika kwaya ya shule. Kwa nini Irina alikataa? Yeye alitambua kwamba nyimbo nyingi ambazo angetakiwa kuimba hutukuza mashujaa wa kitaifa na sikukuu ambazo ni zenye asili ya kipagani. Nyimbo nyingine hata huunga mkono uasi na ujeuri ili kuendeleza mapendezi ya kitaifa. Yule mwalimu hakuweza kuelewa msimamo wa Irina juu ya suala hili. Irina akaamua kumwandikia mwalimu wake barua akimtajia itikadi zake za kidini—lakini bila kufanikiwa.
Baba ya Irina akawa na wazo. Akampa mwalimu nakala ya kitabu Mwimbieni Yehova Sifa, chenye nyimbo ambazo Irina hupenda kuimba. Siku chache baadaye, yule mwalimu akamwita Irina ndani ya chumba cha muziki. Akamwomba Irina aimbe baadhi ya nyimbo azipendazo kutoka hicho kitabu—wanadarasa wenzake wakiwepo—huku mwalimu akifuatisha kwa kupiga piano. Wonyesho huo ukaendelea kwa muda uzidio saa moja! Yule mwalimu alilazimika kukiri kwamba kitabu cha nyimbo Irina akipendacho zaidi kilikuwa na melodia fulani zilizo tamu sana.