Aliyekuwa Hakimu Hapo Awali Aomba Radhi—Baada ya Miaka 45
MAHAKAMANI katika Berlin, mwezi wa Agosti 1995, aliyekuwa hakimu wa Mahakama Kuu Zaidi hapo awali alimweleza mmoja wa Mashahidi wa Yehova majuto yake kwa sababu ya kosa alilokuwa amefanya miaka 45 iliyopita.
Mwezi wa Oktoba 1950, Mahakama Kuu Zaidi ya Jamhuri ya Demokrasi ya Ujerumani (GDR) iliwatangaza Mashahidi wa Yehova tisa kuwa na hatia ya machocheo dhidi ya serikali na upelelezi. Wawili walihukumiwa kifungo cha maisha, na wale wengine saba—kutia na Lothar Hörnig mwenye umri wa miaka 22, mshtakiwa wa nne kutoka kushoto katika picha—walipewa vifungo vya muda mrefu.
Miaka 40 baadaye, GDR ikawa sehemu ya Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani. Tangu wakati huu maofisa wamechunguza baadhi ya ukosefu mbalimbali wa haki katika ile iliyokuwa GDR hapo awali na wamejaribu kuhukumu wale wenye lawama. Mmojapo ukosefu wa haki wa aina hiyo ulikuwa ile kesi ya Mahakama Kuu Zaidi ya wale Mashahidi katika 1950.
A. T., ambaye sasa ni mwenye umri wa miaka 80, alikuwa mmoja wa wale mahakimu watatu waliotoa hukumu wakati wale Mashahidi tisa walipofikishwa mahakamani. Sasa akiwa ameshtakiwa kupotosha haki, alikuja mbele ya Mahakama ya Kimkoa katika Berlin ili kueleza juu ya hukumu aliyokuwa ametoa.
Katika taarifa yake kwa mahakama, huyo aliyekuwa hakimu hapo awali alikiri kwamba alikuwa amepigia kura hukumu ya hatia miaka 45 mapema, ingawa alikuwa amependelea kutoa hukumu zisizokuwa kali hivyo. Lakini kesi hii ilikuwa imemfanya afikirie tena. Kwa nini? Mashahidi wa Yehova walinyanyaswa na Wanazi wakati wa vita ya ulimwengu ya pili kwa sababu walikataa kumuunga mkono Hitler. Baada ya hiyo vita Mashahidi walinyanyaswa tena, wakati huo na utawala wa Kikomunisti. Hilo lilimfanya hakimu “asononeke sana.”
Lothar Hörnig aliiambia mahakama kwamba alitumia miaka mitano na nusu akiwa amefungwa peke yake naye hakuachiliwa kutoka gereza la Brandenburg hadi 1959. Baada ya kusikia taarifa ya Hörnig, yule aliyekuwa hakimu hapo awali alitoa machozi. “Nasikitika sana,” akalia machozi kwi kwi kwi. “Tafadhali nisamehe.” Hörnig alikubali hilo ombi la msamaha.—Linganisha Luka 23:34.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Neue Berliner Illustrierte