Wataalamu Wafikiria Njia Nyingine Badala ya Damu
WATAALAMU wapatao 200 kutoka kotekote Marekani walikutana Cleveland, Ohio, Jumamosi, Oktoba 7, 1995, kuzungumzia suala lenye upendezi wenye kuongezeka katika uwanja wa tiba: utabibu na upasuaji bila damu.
Hali ngumu kadhaa zilizungumzwa. Kwa kielelezo, iweje mgonjwa apatwapo na upungufu mkubwa wa damu? Mtoto azaliwaye kabla sana ya wakati wake atatibiwaje bila damu? Je, upasuaji wa moyo waweza kufanywa kwa mafanikio bila ya utiaji-damu mishipani? Kwa kupendeza, upasuaji bila damu—mara nyingi hutumia mbinu ambazo husaidia mwili kujitengenezea akiba yake ya damu—mbinu hizo tayari zimejaribiwa katika hali hizo zote kukiwa na matokeo mazuri.a
Kwa nini kuna uhitaji wa njia nyingine badala ya utiaji-damu mishipani? “Tumejifunza kwamba kutia damu mishipani mara nyingi hupitisha magonjwa, hasa mchochota wa ini,” asema Sharon Vernon, mkurugenzi wa Center for Bloodless Medicine and Surgery kwenye St. Vincent Charity Hospital katika Cleveland. Yeye aendelea kusema: “Hata damu ikosapo kupitisha ambukizo, inaweza kupunguza uwezo wa mfumo wa kujikinga wa mgonjwa.” Ingawa kupitishwa kwa UKIMWI kumepunguzwa kupitia uchunguzi wa damu, bado kuna magonjwa mengi ambayo hayagunduliwi kupitia uchunguzi huo. Na licha ya ule uhitaji wa matayarisho makubwa zaidi, upasuaji bila damu huthibitika kuwa na gharama nafuu kwa hospitali, kwani huondoa kabisa matatizo ya kisheria ambayo yanaweza kutokea mgonjwa apokeapo damu iliyochafuliwa.
Kwa Mashahidi wa Yehova, kuna sababu ya maana zaidi ya kuepuka kutumia damu: sheria ya Mungu hupinga kutumia damu. (Matendo 15:29) Hata hivyo, wao hutaka kupata matibabu bora kabisa yanayowezekana. Hivyo, wao wameshirikiana na madaktari ambao wameongoza utafiti katika utibabu bila damu. Utibabu huo hunufaisha si Mashahidi wa Yehova tu bali pia wengine wengi ambao wanahangaikia hatari za kutiwa damu mishipani.
[Maelezo ya Chini]
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Picha ya WHO iliyopigwa na P. Almasy