Hekaya ya Furiko Yategemeza Simulizi la Biblia
GHARIKA ya tufeni pote ya siku ya Noa ni jambo la hakika la kihistoria. Aina mbalimbali za masimulizi zapatikana katika historia ya mdomo ya staarabu nyingi tofauti-tofauti ulimwenguni pote. Katika nchi ya Afrika, Chad, kabila la Moussaye hueleza Furiko hilo hivi:
‘Hapo zamani za kale, mahali palipo mbali sana, paliishi familia moja. Siku moja, mama wa familia hiyo alitaka kuwatayarishia wapendwa wake mlo mzuri sana. Kwa hiyo akachukua kinu chake na mchi wake ili atwange nafaka iwe unga. Wakati huo anga-hewa lilikuwa karibu zaidi kuliko lilivyo sasa. Kwa kweli, ikiwa ungeunyosha mkono wako, ungeweza kuligusa. Akatwanga nafaka kwa nguvu zake zote, na mtama alioutwanga upesi ukawa unga. Lakini alipokuwa akitwanga, bila kuwa mwangalifu mwanamke huyo aliuinua mchi juu sana, naye akatoboa shimo kwenye anga-hewa! Mara moja, maji mengi sana yakaanza kumwagika duniani. Hiyo haikuwa mvua ya kawaida. Ilinyesha siku saba mchana na usiku mpaka dunia yote ikafunikwa kwa maji. Mvua ilipokuwa ikinyesha, anga-hewa lilianza kuinuka hata likafika lilipo sasa—juu lisiweze kufikiwa. Ni msiba ulioje kwa wanadamu! Tangu wakati huo, tumepoteza pendeleo la kuligusa anga-hewa kwa mikono yetu.’
Kwa kupendeza, masimulizi ya kale yanayoeleza juu ya furiko la tufeni pote yaweza kupatikana ulimwenguni pote. Staarabu za wenyeji wa Amerika na zile za Wenyeji wa Australia zote zina hadithi juu yalo. Mambo madogo-madogo huenda yakatofautiana, lakini masimulizi yaliyo mengi yana lile wazo la kwamba dunia ilifunikwa kwa maji na ni watu wachache tu waliosalimika wakiwa ndani ya chombo kilichofanyizwa na mwanadamu. Kuenea sana kwa habari hiyo huongezea utegemezo wa lile jambo la hakika kwamba Gharika ya ulimwenguni pote ilitukia, kama ilivyoripotiwa katika Biblia.—Mwanzo 7:11-20.