Mahakama Kuu Zaidi ya Connecticut Yategemeza Haki za Mgonjwa
Katika Aprili 8, 1996, Mahakama Kuu Zaidi ya Connecticut, Marekani, ilitegemeza haki ya Mashahidi wa Yehova ya kukataa utiaji-damu mishipani. Uamuzi huo uligeuza hukumu ya mahakama ya hapo awali.
Katika Agosti 1994, Nelly Vega, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alianza kutokwa na damu sana baada ya kuzaa mtoto wake wa kwanza. Jitihada za kukomesha kuvuja kwake damu hazikuwa na matokeo. Hali ya Bi. Vega ilipoendelea kuwa mbaya zaidi, hospitali ilijaribu kupata amri ya mahakama ya kuidhinisha utiaji-damu mishipani. Bi. Vega alikuwa tayari ametia sahihi hati ya ondoleo la hatia la kitiba yenye kuagiza kwamba hapasi kutiwa damu au vifanyizo vinavyohusiana na damu anapokuwa hospitalini, hivyo akiiweka hospitali huru na daraka lolote la matokeo ya uamuzi wake. Hata hivyo, hospitali ilijadili kwamba kulazimisha utiaji-damu mishipani ungefanywa kwa manufaa bora ya kitoto kilichozaliwa karibuni, ambacho hospitali ilijadili kwamba, kilihitaji mama yake. Mahakama ya kesi pia ilisikitika kwamba, mbali na kupoteza damu yake, Bi. Vega alikuwa mwanamke mchanga, mwenye afya nzuri. Hivyo, licha ya kuteta kwa mume wa Bi. Vega na wakili wake, mahakama ilitoa amri naye akatiwa damu mishipani.
Baada ya muda fulani, kesi ilipelekwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Connecticut. Huko, iliamuliwa kwa kauli moja kwamba tendo la hospitali lilikiuka haki za Bi. Vega. Huo uamuzi ulisema hivi: “Kusikizwa kwa kesi hiyo mbele ya mahakama kulitokea usiku wa manane, katika hali za dharura kabisa ambazo hazikufaa kwa pande zote mbili kuwa na uwezo wa kufafanua majibizano yao.”
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu Zaidi ya Connecticut ni wa maana kwa watu wasio Mashahidi wa Yehova. “Ni wa maana kwa wagonjwa wote ambao huenda wasikubaliane na maamuzi ya madaktari wao,” asema Donald T. Ridley, wakili wa Bi. Vega. “Uamuzi huo utazuia hospitali kusonga viwango vya wagonjwa, iwe ni vya kidini au visivyo vya kidini.”