“Tangu Utoto Sana Umeyajua”
KULINGANA na uchunguzi wa kisayansi wa majuzi, kuzungumza na watoto wachanga huathiri sana ukuzi wa akili zao, kukiuimarisha uwezo wao wa kufikiri, kusababu, na kutatua matatizo. Hivyo ndivyo ilivyo hasa wakati wa mwaka wa kwanza wa maisha ya mtoto mchanga. Gazeti la International Herald Tribune laripoti kwamba watafiti fulani sasa waamini kwamba “idadi ya maneno ambayo mtoto mchanga husikia kila siku ndiyo mtabiri wa pekee na wa maana zaidi wa vile akili, mafanikio shuleni na uhodari wake katika jamii utakavyokuwa baadaye.”
Hata hivyo, lazima hayo maneno yasemwe na mtu. Yaonekana televisheni au redio, haiwezi kuwa kibadala.
Mtaalamu wa sayansi ya neva kwenye Chuo Kikuu cha Washington Seattle, Marekani alitaarifu hivi: “Twajua kwamba kuunganishwa kwa neva hufanyika mapema sana maishani na kwamba akili ya mtoto mchanga inangojea kihalisi kupatwa na mambo ili kuamua jinsi kuunganishwa kwa neva kufanywavyo. Tulitambua majuzi sana jinsi utaratibu huo uanzavyo. Kwa mfano, watoto wachanga wamejifunza sauti za lugha yao ya kienyeji kufikia umri wa miezi sita.”
Utafiti hupinga oni lililoenea pote kwamba watoto wachanga watasitawi kiakili wakipewa tu upendo mwingi. Utafiti huo pia wakazia umaana wa wazazi katika ukuzi wa mtoto.
Jambo hilo latukumbusha maneno ya barua iliyopuliziwa ya mtume Paulo kwa Timotheo: “Tangu utoto sana umeyajua maandishi matakatifu, yawezayo kukufanya uwe mwenye hekima kwa ajili ya wokovu.” Yaelekea kwamba maandishi matakatifu, ambayo mtoto mchanga Timotheo aliambiwa na mama na nyanya yake waliokuwa waamini, yalitimiza fungu kubwa katika ukuzi wake akiwa mtumishi mwenye kutokeza wa Mungu.—2 Timotheo 1:5; 3:15.