Mfalme Mwenye Mali na Hekima
Je, wafikiri kwamba mali zaweza kukufanya uwe mwenye furaha? Kama mtu angekupatia fedha nyingi mno, je, hungefurahi? Labda ungefurahi. Yaelekea ungefikiria njia za kuzitumia.
KWA wazi, kuna vitu vingi vya kununua ili kufanya maisha yawe yenye kustarehesha na yenye kufurahisha. Pia fedha zaweza kutumika kuwa “ulinzi” dhidi ya matatizo yasiyotazamiwa, kama vile maradhi au ukosefu wa kazi ya kuajiriwa.—Mhubiri 7:12.
Lakini kuna uhusiano gani kati ya fedha na furaha? Wafikiri, kama wengi wafikirivyo, kwamba furaha ni pato la ziada la mali? Kupata majibu ya maswali hayo kwaweza kutokeza ugumu kwa sababu fedha zaweza kupimwa kwa urahisi, au kuhesabiwa, ilhali furaha haiwezi. Huwezi kuiweka furaha kwenye mizani na kuipima.
Kisha pia, matajiri fulani huonekana kuwa wenye furaha, ilhali wengine ni wenye taabu. Ndivyo ilivyo kwa walio maskini. Ingawa hivyo, watu wengi, hata wale ambao tayari ni wenye mali, huamini kwamba fedha zaidi zitawaletea furaha nyingi zaidi.
Mtu mmoja aliyeandika kuhusu mambo hayo alikuwa Mfalme Solomoni wa Israeli ya kale. Alikuwa mmoja wa watu walio matajiri waliopata kuishi. Waweza kusoma ufafanuzi wa utajiri wake katika sura ya 10 ya kitabu cha Biblia cha Wafalme wa Kwanza. Kwa mfano, ona kwamba, mstari wa 14 husema: “Uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani [“Solomoni,” NW] mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita.” (Italiki ni zetu.) Tarakimu hiyo ni sawa na tani 25 za dhahabu. Leo, kiwango hicho cha dhahabu kingekuwa na thamani ya dola zaidi ya 200,000,000, za Marekani!
Na bado, Solomoni hakuwa tajiri tu; alibarikiwa na Mungu kuwa na hekima. Biblia husimulia hivi: “Mfalme Sulemani [“Solomoni,” NW] akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima. Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani [“Solomoni,” NW] uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.” (1 Wafalme 10:23, 24) Sisi pia twaweza kunufaika kutokana na hekima ya Solomoni, kwa kuwa maandishi yake ni sehemu ya Biblia. Acheni tuone yale yaliyombidi kusema kuhusu uhusiano kati ya mali na furaha.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Reproduced from Die Heilige Schrift - Übersetzt von Dr. Joseph Franz von Allioli. Druck und Verlag von Eduard Hallberger, Stuttgart