Jihadhari na Usimoni!
SIMONI wa Samaria aliheshimiwa sana katika jumuiya yake. Aliishi katika karne ya kwanza W.K., nao ufundi wake wa kimzungu ulivutia watu sana hivi kwamba walikuwa wakisema hivi kumhusu: “Mtu huyu ndiye Nguvu ya Mungu, iwezayo kuitwa Kubwa.”—Matendo 8:9-11.
Hata hivyo, baada ya Simoni kuwa Mkristo aliyebatizwa, alitambua nguvu kubwa zaidi kuliko zile alizoonyesha hapo awali. Hizo nguvu zilikuwa zimepewa mitume wa Yesu, zikiwawezesha kuwapa wengine zawadi za kimuujiza za roho takatifu. Simoni alivutiwa sana hivi kwamba aliwatolea mitume fedha na kuwasihi hivi: “Nipeni mimi pia mamlaka hii, ili yeyote ambaye mimi naweka mikono yangu juu yake apate kupokea roho takatifu.”—Matendo 8:13-19.
Mtume Petro alimkemea Simoni, akisema: “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu kupitia fedha ulifikiri kupata umiliki wa zawadi ya bure ya Mungu. Wewe huna sehemu wala fungu katika jambo hili, kwa maana moyo wako si mnyoofu mbele ya macho ya Mungu.”—Matendo 8:20, 21.
Neno “usimoni” latokana na simulizi hilo la Biblia, nalo limefasiliwa kuwa “dhambi ya kununua na kuuza nyadhifa au upandishwaji vyeo kanisani.” Kichapo New Catholic Encyclopedia chaonyesha kwamba hasa kuanzia karne ya 9 hadi ya 11, “usimoni ulikuwa umeenea sana katika nyumba za watawa, miongoni mwa makasisi wa vyeo vya chini, maaskofu na hata mapapa.” Chapa ya tisa ya The Encyclopædia Britannica (ya 1878) yasema: “Uchunguzi wa historia ya mabaraza ya siri ya Mapapa humsadikisha mwanafunzi kwamba hakujawahi kuwa na uchaguzi wa kanisa usiokuwa na usimoni, ingawa katika visa vilivyo vingi, ule uliozoewa katika mabaraza hayo ya siri umekuwa usimoni mbaya zaidi, wenye kuaibisha zaidi, na ulio wazi zaidi.”
Wakristo wa kweli leo wapaswa kujihadhari na usimoni. Kwa kielelezo, huenda wengine wakawarai au kuwapa zawadi kwa wingi wale wawezao kuwapa mapendeleo zaidi. Kwa upande ule mwingine, huenda wale wawezao kuwapa mapendeleo hayo wakawapendelea wale wenye uwezo—na mara nyingi wenye hamu—ya kuwapa zawadi kwa wingi. Hali zote mbili zahusisha usimoni, nayo Maandiko hushutumu waziwazi mwenendo kama huo. “Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu,” Petro akamhimiza Simoni, “na omba dua kwa Yehova ili, ikiwezekana, upate kusamehewa mbinu ya moyo wako [“hila hiyo yako,” New Jerusalem Bible]; kwa maana naona wewe ni nyongo yenye sumu na kifungo cha ukosefu wa uadilifu.”—Matendo 8:22, 23.
Kwa furaha, Simoni alielewa uzito wa tamaa yake mbaya. Aliwasihi mitume hivi: “Nyinyi watu, fanyeni ombi la dua kwa Yehova kwa ajili yangu ili hata moja kati ya mambo mliyosema lisipate kuja juu yangu.” (Matendo 8:24) Kwa kuzingatia somo muhimu lipatikanalo katika simulizi hili, Wakristo wa kweli hujitahidi kuepuka kutiwa doa lolote na usimoni.