Mwongozo Katika Kuchagua Washirika Wema
VIJANA huwategemea marika wao badala ya wazazi wao ili kupata mwongozo juu ya mavazi na muziki, yataarifu ripoti moja katika Reader’s Digest. Kwa hiyo ni muhimu wazazi wajue watoto wao hushirikiana na nani na wapi.
“Ni daraka lenu kufanya uchunguzi,” asema Esmé van Rensburg, mhadhiri mkuu katika idara ya saikolojia katika chuo kikuu cha Afrika Kusini. Aongeza kusema hivi: “Yaelekea kwamba mtoto wenu atakasirishwa nanyi, lakini atapoa.” Kisha apendekezea wazazi mambo yafuatayo. Sheria zapaswa kupatana na akili na ziwe na kanuni hususa; msikilizeni mtoto wenu; msikasirike, tulieni, na mjue jambo mnalotaka kusema. Ikiwa mtoto wenu tayari amesitawisha urafiki na mshirika asiyependeza, kazieni tabia isiyokubalika ambayo urafiki huo umetokeza badala ya kumkataza tu asishirikiane naye tena.
Shauri zuri kwa wazazi limekuwepo kwa muda mrefu katika Neno la Mungu, Biblia. Mathalani, yataarifu hivi: “[U]we mwepesi sana juu ya kusikia, wa polepole juu ya kusema, wa polepole juu ya hasira ya kisasi.” (Yakobo 1:19) Maandiko pia hutoa shauri zuri juu ya kuchagua washirika: “Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.” (Mithali 13:20) Vielelezo hivyo vyaonyesha hekima iliyopo kwa wale waisomao Biblia kwa kuithamini na kutumia mambo isemayo katika maisha yao ya kila siku.