Je, Muungano wa Kidini Wakaribia?
“Twashuhudia siku ya maana katika historia ya makanisa yetu,” akasema Christian Krause, msimamizi wa shirikisho la Lutheran World Federation. Naye Papa John Paul wa Pili vilevile akasema juu ya “hatua muhimu na isiyo rahisi ya kurejesha tena muungano kamili miongoni mwa Wakristo.”
Matangazo hayo yenye kusisimua yalitolewa baada ya kutiwa sahihi kwa Taarifa Rasmi ya Pamoja Oktoba 31, 1999, huko Augsburg, Ujerumani, kuthibitisha Azimio la Pamoja kuhusu Fundisho la Haki. Wakati na mahali pa kufanyia mkutano huo palichaguliwa ifaavyo. Inasemekana kwamba Oktoba 31, 1517, Martin Luther alipigilia hoja zake 95 kwenye mlango wa kanisa huko Wittenberg, na hivyo kuanzisha Marekebisho ya Kiprotestanti. Bila shaka, Augusburg ni mahali ambapo katika mwaka wa 1530, Walutheri waliwasilisha itikadi zao za msingi, ziitwazo Augsburg Confession, ambazo zilikataliwa na Kanisa Katoliki, na hivyo kutokeza pengo lisiloweza kuzibwa kati ya Waprotestanti na Wakatoliki.
Je, Azimio hilo la Pamoja litakuwa hatua ya kukata maneno katika kumaliza mgawanyiko wa kanisa, kama inavyodaiwa? Si washiriki wote waliokuwa na matazamio mema. Zaidi ya waǹatheolojia 250 Waprotestanti walitia sahihi ombi la kupinga, wakionya dhidi ya kutawaliwa na Kanisa Katoliki. Waprotestanti waliudhika pia wakati Kanisa Katoliki lilipotangaza rehema ya pekee kwa mwaka wa 2000, zoea lilelile lililosababisha mgawanyiko yapata miaka 500 iliyopita. Na kwa kuwa Augsburg Confession na hoja ya Kikatoliki ya kupinga iliyotolewa na Baraza la Trent bado inatumika, itakuwa vigumu sana kupata muungano.
Mgawanyiko na kutoafikiana ndani ya Jumuiya ya Wakristo ni mkubwa sana kuliko marekebisho yoyote yanayoweza kuletwa na kutiwa sahihi kwa azimio lolote la pamoja. Isitoshe, muungano katika imani hutegemea itikadi zinazotegemea hasa Neno la Mungu, Biblia. (Waefeso 4:3-6) Muungano wa kweli hautokani na kuridhiana bali hutokana na kujifunza na kufanya yale ambayo Mungu anataka. “Mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake,” akatangaza nabii mwaminifu Mika, “na sisi tutakwenda kwa jina la BWANA, Mungu wetu, milele na milele.”—Mika 4:5.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
© Ralph Orlowski/REUTERS/Archive Photos