Kuufikia Moyo wa Mtoto
JE, UMEWAHI kusikitika kuona mtoto akicheza michezo ya vita? Kwa kuwa jeuri imejipenyeza katika tafrija, michezo kama hiyo imekuwa ya kawaida hata miongoni mwa walio wachanga sana. Unaweza kumsaidiaje mtoto aache kucheza michezo ya vita na badala yake acheze michezo isiyo ya vita? Waltraud, ambaye amekuwa mmishonari Shahidi wa Yehova kwa muda mrefu barani Afrika, alipata njia ya kumsaidia mvulana mmoja kuacha michezo kama hiyo.
Kwa sababu ya vita, Waltraud alitoka nchi alimokuwa akiishi na kuhamia nchi nyingine ya Afrika. Akiwa huko alianzisha funzo la Biblia pamoja na mama ya mvulana mmoja mwenye umri wa miaka mitano. Kila mara Waltraud alipomtembelea mama huyo, mvulana huyo alikuwa akicheza na bunduki ndogo ya plastiki. Mvulana huyo hakuwa na chombo kingine cha kuchezea ila bunduki hiyo. Waltraud hakuwahi kumwona mvulana huyo akilenga bunduki hiyo kwenye kitu fulani, lakini sikuzote alipenda sana kuifungua na kuifunga, kana kwamba alikuwa akiijaza risasi.
Waltraud alimwuliza hivi mvulana huyo: “Werner, je, unajua ni kwa nini ninaishi katika nchi yenu? Ni kwa sababu ya vita. Nilikimbia nchi yetu ili kuepuka watu hatari waliokuwa wakiwaua watu kwa kutumia bunduki kama hiyo yako. Je, unafikiri ni vizuri kuua watu?”
“Hapana,” Werner akajibu kwa kusikitika.
“Umesema kweli,” akamjibu Waltraud. Kisha, Waltraud akamwuliza: “Je, unajua ni kwa nini ninawatembelea wewe na mama yako kila juma? Ni kwa sababu Mashahidi wa Yehova wanataka kuwasaidia wengine kuwa na amani pamoja na Mungu na majirani wao.” Baada ya mama ya Werner kukubali, Waltraud alimwambia Werner hivi: “Ukinipa hiyo bunduki yako, nitaitupa, kisha nitakuletea kigari cha kuchezea chenye magurudumu manne.”
Werner akampa Waltraud bunduki hiyo ya plastiki. Ilibidi Werner asubiri kwa majuma manne, hata hivyo, kigari chake kipya kilifika. Werner alifurahi sana alipopokea kigari hicho kilichotengenezwa kwa mbao.
Je, unapanga wakati wa kuzungumza na watoto wako, huku ukijaribu kugusa mioyo yao ili watupe vyombo vya kuchezea vinavyofanana na silaha? Ikiwa unafanya hivyo, utakuwa umewafundisha jambo ambalo litawafaidi katika maisha yao yote.