Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w76 5/15 kur. 222-225
  • Matendo ya Kinyama Yatakwisha Lini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Matendo ya Kinyama Yatakwisha Lini?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MATUMIZI MABAYA SANA YA VIUNGO VYA UZAZI
  • WASONGAMANISHWA KATIKA KAMBI ZA UZUIZI
  • MAMBO HAYO YA KISHENZI YATAKWISHA LINI?
  • Watu Wakaidi Wapuza Katiba ya Malawi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Yehova Hutujali Sikuzote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Nilibarikiwa ‘Katika Majira Yanayofaa na Majira Yenye Taabu’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Nimemruhusu Yehova Aongoze Njia Yangu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2022
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
w76 5/15 kur. 222-225

Matendo ya Kinyama Yatakwisha Lini?

BAADA ya kuondolewa Msumbiji walikokuwa wamekimbilia, maelfu ya mashahidi wa Yehova walianza kumiminika katika barabara kuu za kaskazini na kati ya Malawi wakirudi vijijini kwao. Wengi walisumbuliwa-sumbuliwa sana.

Kikundi kimoja cha Mashahidi 40, wanaume na wanawake, kilifika katika soko la Mzimba, kikielekea makwao kaskazini ya nchi. Watu walikusanyika kuwafanyia mzaha wasafiri hao wachovu, halafu washiriki wa Ushirika wa Vijana wa Malawi wakawashambulia. Walipigwa vikali tangu saa 2:30 asubuhi mpaka saa 8:00 alasiri. Mapolisi walisimama kando wakitazama. Mmoja wa wenye kupigwa alikuwa mwanamume wa zaidi ya miaka 80. Bado walikuwa na maili 70 za kutembea na hawakuwa na chakula, maana pesa chache walizokuwa nazo walinyang’anywa na washiriki wa Ushirika wa Vijana.

Walipofika vijijini kwao, nyakati nyingine Mashahidi kwanza waliruhusiwa kukaa tena katika nyumba zao. Lakini kwa ujumla muda mwingi haukupita bila ya washiriki wa Ushirika wa Vijana kuja kudai wanunue kadi za kuwa katika chama cha kisiasa. Walipokataa walitendewa namna zote za ukatili. Angalia mifano michache:

Kijiji cha Sosola, Jimbo la Kati; Agosti 26, 1975: Kikundi cha wanaume na wanawake, kutia na Mjumbe wa Bunge wa hapo, Bw. Elson Muluzi, na Mwenyekiti wa Chama wa hapo, Stuart Maere, wazingira nyumba za mashahidi wa Yehova na kuwauliza kama wana nia ya kununua kadi za uanachama. Mashahidi wajibu hawawezi, kisha wanachama wanyang’anya nyumba zao na kuwafukuza kijijini, wakisema: “Ondokeni hapa! Nendeni kwenye nchi isiyo na kadi zo zote!”

Jimbo la Kasonjola; Septemba 4, 5, 1975: Vijana wa Malawi Congress Party waenda kwenye nyumba za Mashahidi wa vijiji vya Nsambe, Kampini, Tanga, Mbalame I, Mbuziyamwana na Mselela. Wadai kadi za chama zinunuliwe. Mashahidi wakataapo, wanachama waingia nyumbani mwao na kuiba mali zao zote: pesa, baiskeli, saa za mkono, sahani, vikombe na vyombo vingine vya nyumbani. Akina ndugu wapigwa sana, mmoja azimia kwa saa moja na nusu. Mahali pawili, washiriki wa Ushirika wa Vijana (ambao mwenyekiti wake ni Mozangwila) wakojolea unga wa mahindi katika nyumba hizo, kuufanya usifae kuliwa. Wakati Shahidi mmoja aendapo kwa polisi akaripoti juu ya mashambulio hayo na kurudi, apigwa tena.

Kijiji cha Makambale, Jimbo la Kati: Mashahidi watano, wanaume na wanawake, wavuliwa nguo, wapigwa-pigwa na kufukuzwa maili saba. Wanaohusika na tendo hilo: Mjumbe wa Bunge wa eneo la Mangochi, Bw. Abidabilu, na washiriki wa Ushirika wa Vijana na Mapainia Vijana. (Mapainia Vijana ni chama cha huko wala si wale mapainia wa Sosaiti.)

Mazonda, Muso na Mingola; Septemba 2, 3, 1975: Zaidi ya wanaume na wanawake 20 washambuliwa na kupigwa vibaya sana na wanachama wa Malawi Congress Party wa wilaya ya Ncheu. Shahidi mmoja azimia kwa saa mbili kwa sababu ya kupigwa. Kisha washambuliaji wasugua maganda yenye kuwasha ya mbegu kama maharagwe katika vidonda vya wanaume na wanawake pia. Septemba 4, 1975: Mapainia Vijana Maduka na Samora waongoza kikundi cha vijana kushambulia Mashahidi katika kijiji cha Beni Chauya. Wanaume na wanawake wapigwa hata wazimia.

Lingadzi, eneo la Lilongwe; Septemba 29, 1975: Saa 12:000 asubuhi kundi la wakuu wa Malawi Congress Party na Ushirika wa Vijana wapeleka Mashahidi kumi na wanne, wanaume na wanawake, kwenye makao makuu ya tawi la Chama katika kijiji cha Tsoka. Huko wapigwa vibaya sana. Washambuliaji wavua Shahidi mmoja nguo, naye alikuwa anaendelea kutokwa na damu mdomoni na masikioni, wamfunga mikono kwa nyuma kisha wasugua matope katika nywele na macho yake. Wanaohusika na tendo hilo: Mwenyekiti wa Eneo Ng’ambe, Naibu wa Mwenyekiti Syawa, na Mwenyekiti wa Tawi la Ushirika wa Vijana Mchezo na Naibu wa Mwenyekiti Mchenga.

MATUMIZI MABAYA SANA YA VIUNGO VYA UZAZI

Ripoti nyingi zinaeleza matumizi mabaya sana ya viungo vya uzazi. Haya ni mengine kati ya hayo:

Eneo la Mponela, kaskazini ya Malawi: Mashahidi wapelekwa na headman wa kijiji chao, Bw. Kwindanguwo, kwenye kituo cha polisi cha Mponela. Wawekwa huko siku tano bila chakula. Kisha wapewa barua waende kituo cha polisi katika Dowa, ambalo ndilo eneo kuu. Wafikapo kituo cha polisi cha Dowa, afisa mwenye kusimamia mambo awapeleka kwenye afisi ya eneo ya Malawi Congress Party. Wakuta Mashahidi wengine wakiwa huko tayari. Wote wapigwa vibaya sana. Kabla hawajaanza kushambuliwa, mwenyekiti wa eneo la Dowa wa Malawi Congress Party, Bw. Kamtepa, apaza sauti akisema, “Yesu Kristo na ashuke sasa hivi atuzuie tusiwapige ninyi nyote, kabla hatujaanza kuwapiga!” Mwenyekiti na wasaidizi wa Ushirika wa Vijana ndipo waanzapo kupiga wanaume na wanawake. Wawavua nguo zao zote na kusugua mchanganyiko wa pilipili na manyoya ya maganda ya mbegu kama maharagwe zenye kuwashaa katika uchi wao wote. Wafinya mchanganyiko huo huo katika viungo vya uzazi vya wanaume na kuuingiza ndani ya viungo vya uzazi vya wanawake. Kisha wasukuma wanaume kuwaweka juu ya wanawake wakijaribu kuwalazimisha wafanye uasherati, wakati huo wote wakiwapiga. Hakuna hata mmoja wa Mashahidi alegeaye katika mateso hayo ya ukatili.

Vijiji vya Bunda, Nyanga na Phatha, kusini ya Lilongwe; Septemba 4 mpaka 9: Mashahidi wote wafukuzwa katika nyumba zao na kuvuliwa nguo kisha wapigwa na makundi yenye ghasia yakiongozwa na mwenyekiti wa hapo wa Malawi Congress Party, na mmoja wao aitwa Jeke. Kikundi kimoja cha washambuliaji kina watu zaidi ya mia moja ambao waja wakiwa tayari na silaha walizochagua kupigia Mashahidi. Wajaribu kusihi wanaume Mashahidi wafanye uasherati na wanawake Mashahidi. Wale wa kutoka Bunda wapelekwa kwa polisi nao polisi wajiunga kuwapiga. Polisi wawaambia Mashahidi: “Serikali ni yetu. Nendeni kwa Mungu, ikiwa yeye yuko, mkamwombe aje kuwasaidia.” Polisi waambiwapo habari za matendo mengine mabaya mno ya ukatili, wajibu hivi: “Nendeni mkamwambie Mungu. Mwacheni awasaidie. Asipofanya hivyo, mwaka huu mtakwisha.”

Bila shaka maneno hayo yanakumbusha mtu juu ya huko nyuma kabla ya utawala wa kichaa wa Nazi katika Ujeremani​—huko nyuma katika karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida ambapo Kristo Yesu alishtakiwa kwa uongo kuwa mfitini juu ya serikali akapigiliwa misumari kwenye mti wa mateso. Soma katika Biblia yako mwenyewe juu ya vile wakuu wa makuhani na waandishi na wazee wa taifa walivyoanza kumdhihaki “wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”​—Mt. 27:41-43.

Leo, maneno yanayoelekea kufanana na hayo yanasemwa kwa mashahidi wa Yehova Malawi kwa sababu wao pia wanaendelea kuwa waaminifu kwa Mungu kama Mwanawe Yesu Kristo, aliyekuwa amemwambia Pontio Pilato hivi mapema: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu.”​—Yohana 18:36.

Kanchenche, magharibi ya kaskazini ya Lilongwe; Agosti 31, 1975: Washiriki wa Ushirika wa Vijana washambulia mashahidi wa Yehova. Wanaume wapigwa na kuangushwa chini kisha washiriki wa Ushirika wa Vijana wawakanyaga shingoni. Wanawake wavuliwa nguo na kupigwa kisha washiriki wa Ushirika wa Vijana watumia mienge (tochi) kuchoma nywele (mavuzi) za sehemu zao za uzazi. Wanawake wa hapo washiriki kuwapiga. Wanawake watano walioolewa wa Mashahidi wanajisiwa. Kisichana kimoja cha miaka kumi na saba chanajisiwa na wanaume watatu mbalimbali. Wanaoongoza katika mateso haya: Mwenyekiti wa Eneo wa Malawi Congress Party Yowase Kapulula wa kijiji cha Lundu; Kanjaye, mwana wa Biliyati wa kijiji cha Thandaza; Asedi Chavesi, mwana wa Magadi wa kijiji cha Chilomba, na Benala Mtsukwa wa kijiji cha Msanda.

Kijiji cha Chimasongwe, eneo la Lilongwe; Septemba 7, 1975: Kikundi cha Mashahidi chapelekwa kwenye tawi la eneo la Malawi Congress Party, ambako wapinzani wao wavua nguo wanaume na wanawake pia. Kisha wawafunganisha pamoja na kujaribu kuwalazimisha wafanye ngono na hivyo wafanye uzinzi. Shahidi mmoja wa miaka 60 afunganishwa hivyo na kisichana kidogo Shahidi; kijana mwingine afunganishwa na dada yake mwenyewe; hata mwanamke aliye mwezini afunganishwa hivyo na mmoja wa Mashahidi wanaume. Mwenyekiti wa hapo wa Ushirika wa Vijana, Chipukupuku, achukua pia mwenge (tochi) na kuchoma nywele (mavuzi) za sehemu za siri, za kifua na za makwapa ya wanaume kumi Mashahidi. Kwa kusihiwa na wanawake wa hapo ambao ni washiriki wa Ushirika wa Wanawake wa Malawi, washambuliaji wachukua Shahidi mmoja mwanamke​—aliyevuliwa nguo akawa uchi​—nao waruka-ruka juu ya miguu na tumbo lake huku wakimpiga kwa makonge mpaka azimia. Mwanamke aliye mwezini apigwa mpaka atoa damu mdomoni na puani.

Chilinde, katika Lilongwe; Septemba 8: Washiriki wa Ushirika wa Vijana wapiga Mashahidi vibaya sana wakati wa usiku. Mmoja wa wanawake anajisiwa na wanaume wanne; mwingine afungiwa nyumbani mwake kwa kufuli, kisha wanaume watatu wamnajisi. Mashahidi waripotipo visa hivi kwa polisi, wapewa jibu hili: “Mwambieni Mungu wenu. Yeye ndiye anayefanya mnyang’anywe. Kwani yeye amekufa, hata macho yake yasione?”

Lumbadzi, kaskazini ya Lilongwe; Septemba 24: Mashahidi watoro warudi makwao, naye headman wa kijiji awaruhusu waingie kijijini. Lakini, usiku huo mwenyekiti wa eneo wa Malawi Congress Party pamoja na kundi la washiriki wa Ushirika wa Vijana waja na kupeleka Mashahidi kwenye afisi ya chama katika Dowa. Washambuliaji wao wawapiga kisha wachukua wanaume wawili Mashahidi na kufunganisha viungo vyao vya uzazi pamoja. Wawapiga katika viungo vyao vya uzazi ili mmoja akijaribu kujivuta asipigwe amwumize yule mwingine. Wafungilia matofali mazito juu ya viungo vya uzazi vya Mashahidi wengine na kuwatembeza wakiwa nayo. Kati ya wanaohusika katika tendo hilo yuko mwanamume anayeitwa Chilunje, wa Lumbadzi. Matendo mabaya mno hayo ya ukatili yaripotiwapo kwa polisi, wao wajibu: “Hata mwuawe, hamtasaidiwa.”

Kijiji cha Chindamba, magharibi ya Zomba; Oktoba 2: Mashahidi kumi na watano wakamatwa na polisi wa Zomba na kuteswa kikatili. Zaidi ya kuwanyima chakula na kuwapiga vibaya sana, watesi wao wafinya viungo vya uzazi vya wanaume na wanawake kwa koleo (vibano au plais) za mbao kujaribu kuwalazimisha wanunue kadi za chama cha kisiasa.

Bado ripoti nyingine zaeleza habari za vijana wa Chama wakisukuma-sukuma vijiti ndani ya viungo vya uzazi vya wanawake Mashahidi. Kweli mambo hayo kwa ujumla ni yenye kuhuzunisha sana na yanachafua moyo. Lakini hayajaisha bado.

WASONGAMANISHWA KATIKA KAMBI ZA UZUIZI

Mwanzoni mwa Oktoba serikali ya Malawi ilitoa barua ya kuzunguka kila mahali kwa vituo vyote vya polisi​—si kukomesha mashambulio ya uvunjaji wa sheria na kurudisha sheria na utengemano​—bali kuzingira mashahidi wa Yehova na kuwaingiza katika kambi za uzuizi, kama vile katika Dzaleka, Kanjedza na Malaku. Katika maeneo mengine kambi hizo za uzuizi ni kubwa; nyingine zinakuwa katika maeneo yenye kuzungushiwa seng’enge ya miiba karibu na vituo vya polisi.

Lakini lililo baya zaidi kwa Mashahidi ni kwamba, watu wazima peke yao ndio wanaotakiwa waingizwe humo. Kwa hiyo wazazi wametenganishwa na watoto wao, kutia na vitoto vichanga vyenye kunyonya. Inaonekana kwamba agizo la serikali limekusudiwa kuzuia Mashahidi wasijaribu kutoroka kwenda nchi nyingine, maana hawawezi kwenda na watoto wao hata wakijaribu kutoroka; au pengine limekusudiwa kuwatia mama Mashahidi katika huzuni nyingi sana ndio watende tofauti na dhamiri yao ya Kikristo na kujiunga na chama cha kisiasa. Sasa makundi mazima ya mashahidi wa Yehova yamezingirwa na kutiwa katika kambi hizo za uzuizi. Yaliyotendwa kwa mashahidi wa Yehova katika Ujeremani ya Nazi yanarudiwa​—na wakati huu yanarudiwa Afrika.

Hivyo Mashahidi wanaachwa bila ya kuweza kuomba serikali yo yote iwafanyie haki au kuwalinda na kufanyiwa jeuri. Wao wala si washambuliaji wao ndio wanaokamatwa. Wanapotafuta ulinzi wa polisi, wanarudishiwa-rudishiwa maneno kama haya, “Sisi hatuna wakati wa kupoteza juu yenu, maana hamshirikiani na Chama. Hata mtaabishwe, hamna haja ya kutujia mripoti, maana sisi hatupo hapa kwa ajili yenu. Wakati tu mtakapotuonyesha kadi ya Chama ndipo tutakapowasaidia. Mwaweza kutuletea ripoti mtu akifa tu, na hata iwapo hivyo tutakachoandika ni statement tu.”

Katika maeneo mengine mahali pa pekee ambako Mashahidi Wamalawi wanaweza kupata usalama ni vichakani na porini tu​—ambako wanyama halisi wala si wanadamu wa kinyama ndio wanaishi. Orodha ya kutoka eneo la Lilongwe inaonyesha makundi kumi na matano ya mashahidi wa Yehova wamekimbilia Msitu wa Dzalanyama katika mpaka wa kati ya Malawi na Msumbiji. Washiriki wa makundi mengine mengi wanashinda nyakati za mchana wakiwa mjini lakini usiku wanaingia vichakani wakalale huko, ama kwa sababu sasa hawana makao au kwa sababu ya kuepuka kushambuliwa usiku.

MAMBO HAYO YA KISHENZI YATAKWISHA LINI?

Ingawa wametaabishwa sana na mateso hayo ya kishenzi, mashahidi wa Yehova katika Malawi na katika sehemu nyingine zote za ulimwengu hawatikisiki katika imani yao wala katika uamuzi wao wa kushikamana kwa uthabiti na kanuni za Kikristo. Wao wanayakumbuka maneno ya mtume Petro ya wakati ambao Wakristo wa karne ya kwanza walikuwa wakipatwa na mateso kama hayo kwa sababu wao pia ‘hawakuwa wa ulimwengu’ bali waliendeleza uaminifu usiogawanyika kwa ufalme wa Mungu kupitia kwa Kristo Yesu. Mtume aliwaandikia hivi: “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini.”​—Yohana 17:16; 1 Pet. 4:12, 13.

Lakini, maneno hayo hayapunguzi hata kidogo lawama linalokalia wale wanaoleta mateso hayo juu ya watu wasio na hatia. Ikiwa hataleta ukombozi na faraja mapema, basi wakati wa kufikiliza kwake hukumu juu ya ulimwengu adui, Yehova Mungu anaahidi kuleta ukombozi na faraja kwa wote wale wanaomtumaini na kuendelea kuwa waaminifu kwake wakiwa chini ya majaribu makali. Wakati huo na umilele wote ujao, dunia hii haitaaibishwa tena na matendo ya kishenzi, ukatili na upotovu wa hali ya chini sana wenye kutendwa juu ya wasio na ulinzi. Wakati huo, katika dunia yote, “wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.”​—⁠Zab. 37:11.

Lakini je! matendo mabaya mno ya ukatili katika Malawi yanaweza kukomeshwa kabla ya wakati huo? Naam, yanaweza. Wenye mamlaka wakiheshimu katiba ya Malawi, mashambulio hayo yasiyosameheka yanaweza kukomeshwa sasa hivi. Sababu gani wakuu hao Wamalawi waache wavunja sheria, ingawa wamo katika chama chao wenyewe, wapuze katiba ya Malawi na kuliaibisha taifa machoni pa ulimwengu?

Je! kwani katika Malawi hamna hata mwanamume mmoja mwenye mamlaka aliye na hekima na ushujaa kama Gamalieli? Ikiwa yumo, bila shaka huu ndio wakati wa mwanamume wa kadiri hiyo kushauri wenzake, akisema, kama alivyosema Gamalieli juu ya mitume wa Kikristo waliokuwa wamekamatwa: “Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”​—Matendo 5:38, 39.

Kwa kweli wale wanaoteswa sasa katika Malawi wanastahili kuombewa na wote wale wanaomwamini Mungu na haki. (Linganisha Matendo 12:5.) Zaidi ya hilo, ikiwa kuteswa kwa watu hawa wasio na hatia kunakufanya uwahurumie, mbona usiandike barua sasa kwa mjumbe wa Malawi aliye katika nchi yako au kwa wakuu wo wote wa serikali ya Malawi? Wasihi wafanye wawezayo kukomesha matendo mabaya mno ya ukatili yanayoendelea katika nchi yao.

[Maelezo ya Chini]

a Mbegu hizo zenye kuwasha zilizo kama maharagwe zinaitwa chitedze kwa Cinyanja. Scott and Hetherwick Chinyanja Dictionary yasema: “Aina ya haragwe, lenye kujikunja kama herufi “S,” lenye maganda laini ya rangi ya hudhurungi (brown), ambalo likiiva na kutikiswa huwasha kweli kweli; manyoya yake yakikushika shingoni utakuwa kama una kichaa, na utajisikia kama kuna umeme unaokuwasha.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki