Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 4/8 kur. 14-16
  • Upaswalo Kujua Kuhusu Chawa wa Kichwani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Upaswalo Kujua Kuhusu Chawa wa Kichwani
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Namna Tatu
  • Ni Tatizo Lililoenea kwa Mapana Gani?
  • Wao Hupitishwaje?
  • Kulinda Jamaa Yako
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1991
  • Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu Yanaongezeka
    Amkeni!—2003
  • Kuchunguza Nywele Zako
    Amkeni!—2001
  • Je, Nywele Zako Zinakuhangaisha?
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 4/8 kur. 14-16

Upaswalo Kujua Kuhusu Chawa wa Kichwani

MSHTUKO, aibu, na hatia ni vitendo-miitikio vya wazazi ambao watoto wao huwa na chawa wa kichwani. “Inatia aibu,” akasema mama mmoja, “kwa sababu wahisi kwamba watu wafikiria kuwa wewe si mtu safi.”

Lakini je! kuna sababu ya kuona aibu watu wa nyumba yako wakiwa na chawa?

Namna Tatu

Chawa wa kichwani ni wadudu wadogo sana wasio na mabawa, ambao kwa ujumla urefu wao huwa ni inchi moja ikiwa imepunguzwa mara kumi na sita (1/16), ukubwa ambao ni karibu ule wa mbegu ya ufuta (simsim). Wana rangi ambazo huanzia kijivujivu hadi hudhurungi. Ile aibu kubwa ambayo hutokana na kuwa na chawa hutokana na wazo baya la kwamba chawa husumbua watu ambao hawazoei kufuata kibinafsi kanuni nzuri za afya. Lakini, kwa kweli, chawa wa kichwani hupendelea mazingira safi, kwa hiyo hata wale ambao huoga kwa ukawaida waweza kuwapata.

Zaidi ya chawa wa kichwani, namna nyingine mbili za chawa wa kichwani ni za kawaida kwa mwanadamu: chawa wa mwilini na chawa wa kinenani (mbeleni). Yule chawa wa kinenani, ambaye hupitishwa kupitia mgusano wa kingono, hupatikana katika nywele ngumu-ngumu katika eneo hilo la kinena, chini ya makwapa, katika ndevu na masharubu, na pindi kwa pindi katika kope. Huwa ni mfupi zaidi na mwenye umbo kama la kaa mdogo, na ndiyo sababu amebandikwa jina la chanjagaa.

Chawa wa mwilini, ambaye ni tofauti na chawa wa kichwani na chawa wa kinenani, haishi katika miili ya watu. Huishi katika mavazi yaliyo karibu na ngozi ya mwili na hutambaa na kuupanda mwili ili ajilishe. Chawa wa mwilini ameenea kwa mapana miongoni mwa watu walio katika hali za msongamano na zisizo safi. Nyakati zilizopita amekuwa mbebaji wa magonjwa kadhaa, kutia na homa kali ya chawa, homa kali ya mahandakini, na homa kali yenye kurudirudi, lakini ni mara haba ambapo magonjwa haya ya kipuku huenezwa na chawa leo.

Ni Tatizo Lililoenea kwa Mapana Gani?

Jarida la kitiba Archives of Dermatology lilisema hivi: “Kuvamiwa na chawa wa kichwani kumekuwa tatizo lenye kuenea kwa mapana katika United States, likifikia kadiri ya kuenea sana katika maeneo fulani.” Wenye mamlaka katika mambo ya afya wakadiria kwamba watu milioni sita hadi kumi katika United States huathiriwa kila mwaka.

Ikitegemea msingi wa uchunguzi ulioendeshwa na Vitovu vya Kudhibiti Magonjwa United States, hesabu kubwa ya wanafunzi waliochunguzwa walipatwa wakiwa na chawa wa kichwani. Kwa uhakika, Profesa David Taplin, wa Chuo Kikuu cha Shule ya Tiba ya Miami asema hivi: “Katika maeneo fulani tukio hilo ni kubwa kufikia asilimia 40.”

Hata hivyo, hangaiko kuhusu tukio kubwa la kuvamiwa halimo katika United States tu. Gazeti la kisayansi Discover laripoti hivi: “Kutoka Kanada na Chile, kutoka Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujeremani Mashariki, Urusi, hata Australia, zaja ripoti za chawa wa kichwani wakiambukia watoto ambao hesabu yao yafikia asilimia 50 au zaidi katika shule fulani.”

Wao Hupitishwaje?

Kwa kuwa chawa hawawezi kuruka kwa mabawa au miguu, wao hupitishwa hasa kwa mgusano wa moja kwa moja na mtu aliyevamiwa, kwa kawaida mgusano wa kichwa kwa kichwa. Utafiti ulioendeshwa katika madarasa ya Pennyslvania ulifunua kwamba asilimia 73 ya visa vyote vya kuvamiwa ilitukia kwa njia hii. Watu fulani wahisi tarakimu hiyo ni ya juu zaidi. Dennis White, mkurugenzi wa Programu ya Magonjwa Yaletwayo na Wadudu Watambaaji, Idara ya Afya Katika Mkoa wa New York, asema hivi: “Mgusano wa moja kwa moja ndio husababisha karibu asilimia 90 ya visa vyote vya kuvamiwa.”

Njia nyinginezo ambavyo wewe waweza kupata chawa wa kichwani kutoka kwa mtu aliye nao ni kwa kushirikiana kichana, vibano vya nywele, skafu, kofia, ukanda wa kichwani, taulo, hedifoni za stirio, kofia ya kuogelea, au vitu vingine vya kibinafsi. Hiyo ni kwa sababu chawa wana uwezo wa kuendelea hai kufikia saa 20 (watu fulani hudai kuwa ni 48) wakiwa mbali na mwenye kuwapa makao.

Sababu nyingine ambayo hufanya chawa wawe wameenea kwa mapana sana leo ni kwamba wazazi wengi hawashughulikii tatizo hilo. Deborah Altschuler, mkurugenzi mtekelezi wa Shirika la Kitaifa la Uvamizi wa Chawa, asema kwamba “mara nyingi watu huwa wenye shughuli mno hata wasikumbuke kuchukua wakati na kufanya jitihada ya kuchunguza nywele za watoto wao waone kama zina mayai ya chawa.” Ukweli wenye kusikitisha ni kwamba katika miaka ya 1980 kuvamiwa na chawa hutokana na kukosa maarifa na kutojali mambo.

Kulinda Jamaa Yako

Dalili ya kwanza ya kuvamiwa na chawa ni mnyeo (kuwashwa-washwa na kutaka kujikuna). Umo la chawa wa kichwani huwashawasha ngozi ya kichwani, ikisababisha mnyeo na wekundu pindi kwa pindi. Uwe na shuku kuna kitu ikiwa waona mtoto wako akijikunakuna kichwa mara nyingi. Ili kukagua kwa uangalifu watakiwa uwe na nuru nyangavu na kioo cha kukuza ukubwa. Kwa kuwa chawa ni mtembeaji sana na huwa tayari kuepuka kugunduliwa, tafuta mayai yake, ambayo huwa yameshikamana imara na nywele karibu na ngozi ya kichwani. Mayai hayo hutofautiana rangi kuanzia manjano-nyepesi hadi hudhurungi. Madaktari wa ngozi wametambua angalau hali 12 ambazo hudhaniwa kimakosa kuwa ni kuvamiwa na mayai ya chawa. Kwa hiyo, tumia kioo cha kukuza ukubwa ili ufanye jitihada ya juu-chini kukagua kichwa. Kaza fikira kandokando ya masikio na ukosi wa shingo.

Ikiwa chawa ama mayai yao yapatikana, matibabu ya kutumia mafuta maalumu ya shampuu, krimu, au losheni (dawa ya kuua chawa) yataua chawa hao. Ili kuwazuia wasienee, kila mmoja aliyevamiwa apaswa kupokea matibabu wakati ule ule mmoja. Kwa hiyo chunguza jamaa nzima kabla ya kuanza matibabu.

Si sikuzote ambapo dawa ya kuua chawa huua mayai yaliyoshikamana na nywele. Mayai yoyote yaliyobakia yataanguliwa katika muda wa siku saba hadi kumi, kwa hiyo huenda yakahitajiwa matibabu ya pili ya kuua chawa wowote waliobaki hai. Hata hivyo, tahadhari: Dawa zote za kuua chawa zina kiasi kidogo cha sumu ya kuua wadudu ambayo ikitumiwa isivyofaa, huenda ikatokeza athari nzito za kando. Kwa hiyo, fuata kwa uangalifu maagizo ya mfanyizaji.

Ikiwa dawa za kuua chawa hazimo katika eneo lako, njia tofauti za utibabu zaweza kutumiwa. Wenye mamlaka wengi hupendekeza kuyaondoa mayai kwa kichana maalumu chenye meno membamba. Kuongezea hiyo, kitabu cha masomo ya tiba Clinical Dermatology: A Color Guide to Diagnosis and Therapy chadokeza hivi: “Ule mnato wenye kushikamanisha mayai na unywele waweza kuyeyushwa kwa kukanda nywele kwa dakika 15 kwa kutumia siki [vinegari].”

Jambo lenye matokeo hata zaidi ni kunyoa nywele. Watu fulani wamepata pia kwamba kupaka kiasi kidogo cha mafuta-taa kwenye ngozi ya kichwa kwa dakika 15 hadi 20 kutawaua chawa na mayai. Hata hivyo, uangalifu wapasa kutumiwa, kwa kuwa huenda mafuta-taa yakasababisha mwasho wa ngozi mahali hapo, na yakiingia machoni, yaweza kuleta umivu. Pia mafuta-taa yaweza kuwa sumu yakivutwa ndani kwa kupumua, na yatawaka moto yakiwa karibu na mwali wa moto.

Ni jambo la maana pia kutibu matandiko, nguo, na vitu vingine vya kibinafsi. Yaoshe kisha uyakaushe katika kikaushaji chenye joto kwa angalau dakika 20 ili uwaue chawa wale pamoja na mayai yaliyopo. Kwatua-kwatua magodoro, viti vyenye mito, na vitu vingine ambavyo haviosheki ili uondolee mbali mayai yote yenye uhai au chawa wote. Kutibu vitu ni utaratibu wenye kazi nyingi, lakini kwahitajiwa kabisa ili kuwazuia chawa wasiendelee kukaa daima katika jamaa yako.

Ingawa haiwezekani kukaa kabisa bila kuvamiwa na chawa, wewe waweza kupunguza sana uelekeo wa kupatwa nao kwa kufuata miongozo michache iliyo sahili. Watie moyo watoto wako waepuke kushirikiana vichana, brashi, na vitu vingine vya kibinafsi ambavyo vingeweza kwa urahisi kupitisha chawa. Ikiwezekana, fanya watoto wako walale katika vitanda vilivyotengana. Suka nywele ndefu iwe misokoto au iunganike mkiani ikiwa kishungi kimoja ili kusaidia kupunguza mgusano wa kichwa kwa kichwa. Na mwisho, mtoto wako akipata chawa, usibabaike. Ni mara haba ambapo vamio la chawa huwa taabu nzito. Pia hilo ni jambo la kawaida sana na ni moja ya siri ambazo watu hutunza sana mjini.

[Sanduku katika ukurasa wa 15]

Tatizo la Tangu Zamani

Chawa wa kichwani wamekuwa pigo lenye kukumba wanadamu kwa maelfu ya miaka. The Medical Post la Novemba 15, 1988, yaripoti hivi: “Chawa wamepatikana wakiwa wameshikamana na nywele za maiti za Kimisri zenye kuhifadhiwa, kwenye Wahindi wa kutoka Peru wa kabla ya wakati wa Columbia na Wahindi wa kutoka kusini-magharibi ya Amerika.

“Wakati huo kama ilivyo sasa, chawa hawakuchagua kuheshimu mtu eti kwa sababu ya cheo chake cha kifalme, daraja lake au uchaji wake wa kidini.

“Walipatikana kwa wingi katika vichana na sampuli za nywele zilizotolewa katika jumba la kifalme la Herode, kutoka kwenye makao ya kale ya ulowezi kandokando ya Masada, na kutoka kwenye mapango kule Qumran ambako ziligunduliwa zile hatikunjo za Bahari ya Ufu (ya Chumvi), ambazo ndizo hati za kibiblia zijulikanazo kuwa za zamani zaidi.”

Vichana vilivyotumiwa kuondoa mayai ya chawa maelfu ya miaka iliyopita vyafanana ajabu na vile vyenye kutumiwa leo. Kwa kawaida vichana hivyo vilifanyizwa kwa mti, lakini vichana vya pembe vilipatikana katika lile jumba la kifalme la kale kuliko Megido. Vichana vya kuondoa mayai ya chawa vilipochunguzwa kwa ukaribu, vilipatikana vikiwa na chawa wengi na mayai ya chawa juu yavyo.

Dakt. Kosta Mumcuoglu, wa shule ya kitiba ya Chuo Kikuu cha Hadassah, alionelea hivi: “Kwa kufikiria hesabu ya chawa na mayai yaliyo juu ya vichana, yaonekana hivi vilikuwa vifaa vyenye matokeo sana katika kuondoa chawa.”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Chawa wa kichwani (ukubwa wake ukiwa umeongezwa sana na darubini)

[Hisani]

Foto ni kwa hisani ya Beecham Products U.S.A.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki