Wakati Moto Utishapo Umati
MOTO ni neno lisilopendwa na watengenezi wa sherehe za umma. Kila mwaka, mioto husababisha maelfu ya vifo na majeraha mabaya sana. Hatari huwa nzito hasa wakati masongamano ya watu yakusanyikapo katika nafasi iliyozungushiwa ua. Wasimamizi wa maonyesho ya tafrija, tamthilia, makongamano, na makusanyiko mengine makubwa waweza kufanya nini ili wapunguze hatari ya moto? Wale walio sehemu ya umati huo waweza kufanya nini ili kuwe na usalama? Na moto ukitokea kwa kweli, yaweza kufanywa nini ili kuongezea fursa za kuokoka?
Ili kupata habari fulani juu ya mambo haya, Amkeni! lilihoji ofisa mmoja wa moto katika Ailandi. Yeye huzoeza wazima-moto na ameona mengi kuhusiana na mioto.
Umati wa watu utarajiwapo kwa sherehe fulani, wasimamizi waweza kufanya nini ili kuwe na usalama?
Hatua ya kwanza ni kuhakikisha kwamba jengo ambalo mwatarajia kutumia ni salama. Ni lazima kuwe na milango ya kutokea inayotosha wote jengoni kutoka haraka uhitaji ukizuka. Pia, ni lazima kila mlango wa kutokea uwe umeandikwa wazi na usiwe na vizuizi vyovyote. Ni lazima vijia na ngazi zote viwe bila vipingamizi nyakati zote. Milango ya dharura yapasa kufunguka nje-nje na ifanye hivyo kwa urahisi sana.
Huenda mipango ya kuketi ikawa tatizo katika majengo yasiyo na viti vya daima. Ni jambo muhimu kupanga viti kupatana na kanuni zinazohusiana na moto katika eneo lenu. Hakikisheni kwamba wakaribishaji na wangojezi wote wajua la kufanya kukitokea dharura. Wale walio na daraka la usalama wapaswa kujua mahali vilipo vizima-moto vyote na jinsi ya kuvitumia. Ni kuchelewa mno kusoma maagizo baada ya moto kutokea. Kumbuka, pia, jambo la kwanza kabisa baada ya kuanzisha hatua za kuondoka ni kuipasha habari idara ya moto.
Je! kuna lolote ambalo wenye kuhudhuria sherehe hizo waweza kufanya ili kuendeleza usalama?
Naam! Watu hubabaika kwa urahisi zaidi katika mazingira wasiyozoeleana nayo. Kwa hiyo uzoeleane na mpangilio wa ujumla wa jengo ambamo kusanyiko litafanywa. Angalia mahali pa kutokea na mahali ilipo milango ya dharura. Usibabaike. Dumisha nidhamu. Sikiliza kwa uangalifu mielekezo yoyote itolewayo na uifuate. Katika kuliacha jengo, tembea haraka sana, lakini usikimbie wala usisukume watu.
Ni sharti nikazie sana uhitaji wa kuondoka haraka. Watu walio wengi hawang’amui jinsi moto uwezavyo kuenea kasi. Saidia wazee-wazee na wanyonge ukiona kwamba wanatatizwa. Ukiisha kutoka ndani ya jengo, ondoka kabisa kwenye milango ya kutokea ili usifunge njia ya wale wanaokuja nyuma yako, na baada ya wewe kuwa nje, usijaribu kamwe kuingia tena jengoni mpaka ijulishwe kuwa liko salama.
Una ushauri gani kwa wazazi?
Katika umati mkubwa wazazi wapaswa wakati wote kukaa pamoja na watoto wao wadogo au wahakikishe wanatunzwa na mtu mwenye umri mkubwa, mwenye kujali madaraka. Wakati wa dharura ya moto, wazazi wenye kufadhaika huku wakitafuta watoto wao waliopotea waweza kusababisha matatizo ya kila aina.
Je! moto ni hatari kwa sababu tu ya ukali wao mwingi?
Sivyo. Kwa kawaida moshi na gesi zenye sumu ndizo huua watu katika moto. Hata wakati ambapo gesi zilizopashwa moto mwingi sana huwa hazitoshi kuua, zitaingilia viungo vya upumuaji na mifumo ya fahamu ya wanaozipumua. Hiyo yaweza kusababisha watu watende kwa njia isiyo ya akili. Moshi uwapo mzito, funika pua na kinywa kwa kitambaa cha mfukoni. Hakitakulinda na gesi zenye sumu, lakini kitasaidia kuzuia visehemu vikubwa zaidi vya moshi ambao ungeweza kusababisha hali ya kutapika.
Ikiwa moshi ni mzito sana, jaribu kukaa karibu na ukuta ili uepuke kuvurugika fikira. Ikiwa huwezi kuona au kuhisi ukuta, tembea kuelekea upande mmoja mpaka ufikie mlango au dirisha. Pia, kumbuka kwamba katika chumba kilichojaa moshi, kuna hewa zaidi yenye kupumulika karibu na sakafu, na hapo pia utaona vizuri zaidi.
Ni jambo gani laweza kufanywa nguo za mtu zishikapo moto?
Jambo baya zaidi uwezalo kufanya ni kukimbia. Hiyo itaongezea tu kupepea miali ya moto. Badala ya hivyo, jiangushe chini na ubingirike. Hiyo itazuia miali ya moto isifikie uso wako na yatumainiwa itauzima moto.
Kuna neno lolote la mwisho kwa wasomaji?
Mimi natumaini kwamba hutakuwa kamwe motoni. Ni jambo la kutia hofu. Lakini ukishikwa katika mmoja, kanuni hizi chache zitakuwa zenye msaada. Na kumbuka, ichukue hatari ya moto kwa uzito. Usiichukue kimchezo wala kama mzaha. Si mzaha.
[Blabu katika ukurasa wa 15]
Unapokaa hoteli, je! sikuzote wewe hutafuta mahali ulipo mlango wa dharura ulio karibu zaidi kabla hujalala usiku huo?