Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 10/8 kur. 24-26
  • Filipi—Sehemu ya Mabubujiko ya Maji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Filipi—Sehemu ya Mabubujiko ya Maji
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mabubujiko ya Maji
  • Mabubujiko ya Mawe ya Thamani
  • Mabubujiko ya Damu
  • Mabubujiko ya Uhai
  • Mabubujiko ya Ukarimu
  • Kuondoka Kwetu
  • “Vuka Uingie Makedonia”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Kitabu Cha Biblia Namba 50—Wafilipi
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • ‘Amani ya Mungu Ni Yenye Ubora Unaozidi Fikira Zote’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2017
  • Lidia—Mwabudu wa Mungu Mkaribishaji-Wageni
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 10/8 kur. 24-26

Filipi—Sehemu ya Mabubujiko ya Maji

TULIKUWA tunaambaa juu tu kidogo ya mawimbi ya Aegean tulipokuwa tunakaribia Thesalonike. Kwa ghafula, kiwanja cha ndege kikaonekana kikitokeza kwenye ukingo wa maji na kikapitilia chini yetu—karibu sana ya ndege hivi kwamba mke wangu akafikiri kwamba tayari tumetua. “Huo ndio mtuo mwororo zaidi tulioweza kuupata!” yeye akasema. Halafu, magurudumu yakagusa chini kwa kishindo.

Makedonia, Ugiriki! Nilifikiri juu ya ulimwengu wa Aleksanda Mkuu na vita ya baadaye katika uwanda wa Filipi ambayo iliamua wakati ujao wa Rumi. Na nikawazia juu ya athiri ambayo huenda hilo lilileta kwa maisha na huduma ya mtume Mkristo Paulo. Akiwa “mtume wa watu wa mataifa,” Paulo alijulisha Ukristo katika Ulaya huko Filipi. (Warumi 11:13) Je, tungeweza kuona kitu chochote huko ambacho kingetuangazia zaidi? Au historia ilikuwa imepitilia kwenye uwanda huo bila kuacha alama yoyote?

Saa mbili kuelekea kaskazini mwa Thesalonika, basi letu lilipanda kwenye barabara ya mlima juu ya bandari ya Kaválla. Ingawa Kaválla inajulikana kimsingi kwa kuuza nje tumbaku, wavuvi wenye kutengeza nyavu kwenye fuo walifanyiza mandhari ambayo tuliwazia Paulo aliiona wakati Kaválla ilipokuwa inaitwa Neapolis.—Matendo 16:11.

Ingawa Paulo hakukaa Neapolis, hatua chache chini yetu tungeweza kuona barabara ya mawemawe ambayo alisafiria. Halafu tukapitia kipitio chembamba chenye mitimiti na kuona ono la kwanza la ule uliokuwa mji wa Filipi. Tungeweza kutambua mwamba mkubwa unaotia alama mahali penyewe, karibu na katikati ya bonde. Tulikuwa tunatazama chini kwenye mashamba ya tumbaku iliyokuwa ikiiva. Paulo alikuwa ametazama mabwawa, na wahamiaji wa zamani wa misitu mizito. Mtume huenda alisimama kupunga hewa muda baada ya muda alipokuwa akiteremka. Bado, ni lazima awe aliharakisha kusonga mbele labda akiwa amesisimuka kama sisi tulivyokuwa.

Mabubujiko ya Maji

Filipi ilikuwapo kabla ya Filipo 2 kuja katika 356 B.C.E. kufyeka misitu, kueneza mji, na kuuita kwa jina lake. Miaka mitano mapema, wahamiaji kutoka Thásos walikuja kufanya kazi kwenye migodi tajiri ya Asyla na Mount Pangaeus. Waliita kijiji chao Crenides, ‘mahali pa vibubujiko vidogo.’ Kwa nini? Kwa sababu chemchemi za maji zinajitokeza kila mahali, zikifanya bonde hilo kuwa bwawa kwa sehemu kubwa.

Ni karibuni tu ambapo ardhi hiyo ilikaushwa kwa mafanikio. Lakini chemchemi hizo ziko hapo, na bado vijito vinatiririka. Katika mahali pamoja, barabara ya zamani ya Rumi inavuka Mto Gangite. Mto huo ulikuwa wa maana kwa Paulo, na tulitaka tuuone.

Mabubujiko ya Mawe ya Thamani

Filipo aliizingira Crenides ili kuokoa wachimba migodi wa Thásos waliotishwa na Thrace. Alitaka Crenides iwe kituo cha kijeshi. Lakini zaidi ya yote, alihitaji dhahabu kulipia mipango yake ya kivita. Migodi hiyo ya dhahabu ilitajirisha Filipo na Aleksanda Mkuu kwa zaidi ya talanta elfu moja kila mwaka. Dhahabu ilipokwisha, Filipo akawa mnyonge.

Mabubujiko ya Damu

Zaidi ya karne moja ilipita. Ugiriki ukaanguka chini ya uwezo wa Rumi. Milki ya Rumi ilitaka barabara, na Via Egnatia ilijengwa kupitia Makedonia. Kilomita kumi na nne unusu, kutoka pwani, ilipitia katikati ya Filipi, ikiipa usitawi wa biashara na miendo ya kijeshi.

Filipi ilikuwa imekuwa na umaana mkubwa. Katika 42 B.C.E., kulikuwa na damu nyingi iliyomwagwa hapo katika mapigano mawili makubwa kati ya Rumi na wanyang’anyi wa ufalme waliotaka kuongoza milki hiyo. Lakini njama hiyo ya kijamhuri ilikosa kufanikiwa na milki ya Kikaisari iliweza kuokolewa. Ili iwe ukumbusho, Octavio mwenye ushindi aliifanya Filipi kuwa koloni ya Rumi.—Matendo 16:12.

Mabubujiko ya Uhai

Hakuna mtu anayeishi Filipi leo. Sehemu hiyo ni ya kiakiolojia tu. Tulipokuwa tunatembea kwenye njia ya Via Egnatia, tulichunguza alama za magurudumu kwenye barabara. Tulizurura kwenye sehemu ya soko na tukatazama choo cha umma chenye visehemu 50. Kwenye maktaba ya vitabu, hakukuwa na vitabu, kama ambavyo hakukuwa na wacheza mweleka kwenye uwanja wa michezo (Palaestra hasa, au shule ya mieleka). Tuliona mabaki ya mahekalu ya Kirumi, vidirisha vya Kigiriki, na hata sehemu takatifu za Kimisri nusu ya mwendo tulipokuwa tukielekea akropoli. Tulipokuwa tumeketi katika jumba lililo wazi la michezo, tulishangazwa na uwezo walo wa kukuza sauti. Tulisimama kwenye baraza na tukawazia juu ya mahakimu wenye mamlaka wakiwa wanatoka kwenye vyumba vyao, wakitanguliwa na maofisa wa mahakama wanaobeba vifurushi vya fito zilizofunwa kuzunguka shoka—ishara ya mamlaka yao. Kwa jicho la akilini mwetu, tulijaribu kufanyiza Filipi ya mwaka 50 C.E. ambayo ilikuwa na tamaduni ya Kirumi.

Kulingana na Biblia, Paulo na washiriki wenzake ‘wakawa katika mji huu, wakikaa siku kadha wa kadha.’ (Matendo 16:12) Hakuna mapambano yoyote yenye kusisimua yanayoripotiwa. Halafu siku moja Paulo alisikia juu ya kikundi kidogo kimoja ambacho hakikufuata ama miungu ya zamani au mipya na bado kilisemwa kuwa chamcha Mungu. Kikundi hicho kilikuwa kinakutania ng’ambo ya tao la koloni, nje ya mji karibu na mahali ambapo barabara inavuka kijito.

“Hata siku ya sabato” akaandika Luka, “tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.” Mazungumzo hayo yalitia ndani tumaini la wokovu na uhai wa milele kupitia Yesu Kristo. Na hasa “mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, . . . akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.”—Matendo 16:13, 14; linganisha Wafilipi 2:12, 16; 3:14.

Baada ya siku kadhaa, kukaa kwa Paulo katika Filipi kukawa na mwisho wenye tamasha. Akitembea kilomita moja unusu hivi akielekea sehemu ya maombi, alikutana na msichana mwenye kusumbua aliye pagawa na roho mwovu. Wakati Paulo alipofukuza yule shetani, waajiri wa yule msichana walighadhabishwa walipoona kwamba biashara yao ya uaguzi imeharibiwa. Kukiwa na tokeo gani?

“Wakawakamata Paulo na Sila wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji.” ‘Wao ni Wayahudi,’ wao wakashitaki. (Kila mtu alijua kwamba Claudius alikuwa amewafukuza Wayahudi wote kutoka Rumi.) “Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi,” wao wakaongeza. Umati huo ukapiga makelele; wakadhi wakatoa hukumu. Baada ya hilo maofisa wa mahakama wakafungua fito zao na ‘kuwapiga Paulo na Sila mapigo mengi.’ Halafu wakawatupa gerezani, huku wakitokwa na damu na wakiwa dhaifu, na wakawafunga miguu yao kwa mikatale. Usiku uo huo tetemeko kubwa la ardhi liliongoza kwenye kuachiliwa kwa Paulo na sila na kwenye ukubali wa Ukristo kwa yule mlinzi wa gereza na nyumba yake.—Matendo 16:16-34.

Asubuhi iliyofuata, wakadhi walisikitika sana kwa kutokuelewana kokote kulikotokea, lakini je, wale wageni wangeondoka mjini? Paulo na Sila kwanza walienda kwa nyumba ya Lidia ili kutia moyo waamini wenzi kabla ya wao kuelekea Thesalonike. Luka alibaki nyuma ili kulichunga kundi hilo changa.—Matendo 16:35-40.

Mabubujiko ya Ukarimu

“Akatushurutisha” tuingie nyumbani mwake, Luka akaandika juu ya Lidia. Hata yule mlinzi wa Paulo katika gereza alikuwa mkarimu sana punde tu alipoielewa hali. (Matendo 16:15, 33, 34) Marafiki wa Paulo wafilipi walimtumia mara mbili vitu alivyohitaji wakati wa kukaa kwake Thesalonike.

Baadaye, alipokuwa akimtumikia Mungu kwa ushujaa katika Korintho, Wafilipi tena walimtafuta. Hata miaka mingi baadaye, wakati Paulo alipokuwa gerezani Roma, mjumbe kutoka Filipi alikuja pamoja na zawadi na toleo la utumishi wa kibinafsi kwa niaba ya mtume huyo. Paulo aliguswa moyo. Alijua kwamba Wafilipi hawakuwa na mali nyingi. Hivyo akaandika: “Wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongeza utajiri wa ukarimu wao.”—2 Wakorintho 8:1, 2; 11:8, 9; Wafilipi 2:25; 4:16-18.

Kuondoka Kwetu

Tulikawia kando ya Gangite, na nikachovya mkono wangu kwenye maji. Kwa kushangaza, yalikuwa baridi. Tukatazama huku na huku. Mahali fulani karibu na hapa palikuwa “mahali pa sala” ambapo Paulo na wengine walikutana ili kuabudu.

Lakini nikauliza, ni nini kinachofanya Filipi iwe ya pekee sana kwangu? Je, ni hii sehemu iliyo kando ya mto? Au ni sehemu ya soko pamoja na maktaba yake yaliyo tupu, kiwanja kitupu cha michezo, hekalu zisizo na miungu, na maduka yasiyo na bidhaa?

Je, ni mabubujiko yake? Kwa kweli, Filipi kweli kweli ni “mahali pa mabubujiko.” Bado panatiririka kwa maji. Wakati mmoja palitiririka kwa dhahabu na, katika kipindi kibaya, kwa damu. Lakini pia kulikuwako na kipindi kizuri wakati mabubujiko ya uhai, upendo, na ukarimu yalipotiririka kutoka kwa watu wa kipekee sana kama Paulo, Lidia, yule mlinzi wa gereza, na wengine. Ni watu wenyewe sivyo? Watu hao wa kipekee wanafanya Filipe iwe ya maana kwangu. Wananifanya niwe na mawazo mengi. Wananifanya nifikiri. Ninatamani—mke wangu akagusa mkono wangu. “Njoo,” akasema kwa wororo. “Ni wakati wa kuenda”—Imechangwa.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 24]

Juu kushoto: “bema” (kiti cha hukumu) ya Filipi ya kale; juu kulia: mahali ambapo “Via Egnatia” inavuka Gangite; chini: Lile baraza

[Ramani of Greece/Philippi]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki