Vijana Wauliza...
Je! Unywaji Waweza Kunifanya Niwe Mzoevu Kweli?
YOTE yalianza Jerome alipokuwa mwenye miaka tisa tu. “Nilionja vileo vilivyobaki katika karamu iliyofanyiwa nyumbani, nikalewa, na nikapendezwa na jinsi nilivyohisi,” yeye aeleza. Upesi ikawa kawaida kwa Jerome kununua, kuficha, na kunywa kileo. Na bado, anakiri hivi: “Sikujua nilikuwa na tatizo hadi nilipokuwa wa miaka 17. Wengine walipokuwa wakila kiamshakinywa, mimi nilikuwa nikinywa robo lita ya vodka!”
Utumizi ufaao na usiofaa wa kileo unaongezeka kwa kiwango cha kugutusha miongoni mwa vijana ulimwenguni pote. Katika United States pekee, zaidi ya milioni kumi—nusu—ya wanafunzi Waamerika wa kati ya miaka 13 hadi 18 wamekunywa kileo angalau mara moja mwaka uliopita. Karibu milioni nane hunywa kila juma. Kwa kweli, matineja wa U.S. hunywa zaidi ya mikebe bilioni moja ya pombe na chupa za divai baridi yenye kaboni zaidi ya milioni 300 kwa mwaka!
Biblia husema hivi kuhusu kileo: “Kila mtu anayepotoshwa nacho si mwenye hekima.” (Mithali 20:1, NW) Na bado, mamilioni ya vijana, kama Jerome, hukengeushwa na kileo. Kuna hatari gani za kutumia kileo isivyofaa? Unaweza kujuaje kwamba unakuwa mzoevu?
Kileo na Ulevi
Kileo kinapopakiwa kikiwa divai baridi inayovutia au pombe yenye povu, hicho huonekana kuwa hakina madhara. Hata hivyo, ladha na sura zaweza kudanganya. Kileo ni dawa ya kulevya—yenye nguvu.
Madaktari husema kwamba kileo ni kishushaji kinachoathiri ubongo, kikiathiri mfumo wa neva ya kati. Mtu mzima akitumia kileo kwa kiasi, chaweza kuwa na matokeo mazuri, yasiyodhuru. ‘Divai hufurahisha moyo wa mtu,’ yasema Zaburi 104:15. Hata hivyo, kiasi kingi cha kileo chaweza kulewesha—hali ambapo udhibiti wa kimwili na kiakili unaathiriwa sana. Kama Jerome, mtu anaweza kuwa mzoevu, akivuka mpaka wa kutaka kileo hadi kukihitaji au kukitamani. Kwa nini hilo hutukia? Mwili unaweza kukuza hali ya kukubali kileo ikiwa kinatumiwa kupita kiasi. Basi lazima mnywaji anywe kiasi kinachozidi kuongezeka ili kuhisi athari yacho. Hata hivyo, kabla hajang’amua, amekuwa mzoevu. Mtu anapokuwa mzoevu, maisha yake yanabadilika vibaya. Vijana wa U.S. karibu milioni tano wana tatizo la unywaji.
Sababu ya Wao Kunywa
Katika miaka ya 1930, tineja wa wastani wa U.S. alionja kileo kwa mara ya kwanza akiwa mwenye miaka 18 hivi. Leo, yeye hufanya hivyo kabla ya kufikia miaka 13. Wengine huanza wakiwa wachanga hata zaidi. “Nilikuwa mwenye miaka sita, . . . na nilikonga pombe kidogo katika glasi ya babu yangu. . . . nilikuwa nikipata kuzunguzungu sana!” Ndivyo anavyokumbuka Carlotta—anayeacha ulevi. Kadiri unavyoanza mapema, ndivyo inavyoelekea kwamba utakuwa mzoevu.
Bila shaka, kuhusu habari hiyo, mara nyingi marika huwa na uvutano mwingi. Lakini nyakati nyingine wazazi pia ni wa kulaumiwa. Wengine wao hunywa kupindukia, wakitumia kileo kuwa utegemezo wa kihisiamoyo, au hata hujivuna juu ya kiasi cha kileo wanachoweza kunywa. Kijitabu kimoja kuhusu ulevi kinasema: “Watoto wanaokuwa watu wazima wenye kunywa kwa kiasi huelekea kutoka katika familia ambamo kileo huonwa kuwa kitu cha kawaida bila kuwa utegemezo wa kihisiamoyo . . . , ambamo unywaji una mahali pao pafaapo.”a
Televisheni ni uvutano mwingine wenye nguvu juu ya vijana. Kijana wa kawaida Mwamerika anapofikia miaka 18 anakuwa ameona tamasha 75,000 za unywaji katika TV—11 kwa siku. Matangazo yanayovutia, yaliyofanyizwa kwa ustadi ili kufanya unywaji uonekane kuwa njia ya kupata furaha na mahaba, huonyesha violezo wanaovutia kingono wakinywa katika vikao vya karamu zenye kelele. Vileo hupewa majina ya aina ya matunda na bidhaa zinazopendwa. Matangazo hayo hufanikiwa. Kila mwisho-juma, vijana 454,000 katika United States hunywa kupindukia, ikifanya daktari mkuu wa U.S. aseme kwamba wengi wao “tayari ni walevi, na wale wengine wanaelekea kuwa walevi.”
Hata hivyo, vijana wengine husukumwa kunywa kwa sababu ya mahangaiko ya kindani. Kim alifunua kwa nini yeye alikunywa pombe sana: “Nilikuwa nikitumia [kileo] ili nibadilishe hali yangu ya moyo tena ili nihisi vizuri.” Ikiwa kijana ni mwenye haya au hajiheshimu mwenyewe, huenda kunywa kukaonekana kuwa utatuzi unaofaa. Na bado wengine hunywa ili kusahau mambo hakika ya maisha yenye kuwaumiza, kama vile kutendwa vibaya na wazazi au kupuuzwa. Kwa nini Ana alianza kunywa? “Sikuonyeshwa kamwe shauku niliyohitaji.”
Hata sababu ya kuanza kunywa iwe ipi, baada ya muda huenda kijana akapata kwamba inazidi kuwa vigumu kudhibiti unywaji wake. Ndipo huenda akakabiliana uso kwa uso na ulevi. Je! umeanza kunywa? Basi fanya mtihani uitwao “Tangu Ulipoanza Kunywa.” Huenda ukapata matokeo kuwa yenye kufunua mambo sana.
Kileo—Hatari kwa Vijana!
“Wale wakaao sana kwenye mvinyo” wanaonywa na Biblia kwamba “mwisho wake [mvinyo] huuma kama nyoka.” (Mithali 23:29-32) Sumu iliyotiwa na nyoka mwenye sumu yaweza kumjeruhi au kumwua mtu polepole na kwa uchungu. (Linganisha Matendo 28:3, 6.) Vivyo hivyo, utumizi wa kileo kupindukia na kwa muda mrefu kwaweza kukuua polepole. Kwaweza kudhuru au kuharibu viungo muhimu, kama vile ini, kongosho, ubongo, na moyo wako. Hasa miili na akili changa zinazokua zinaweza kupata madhara hayo kwa urahisi zaidi, ambayo nyakati nyingine hayaponyeki.
Utumizi mbaya wa kileo waweza kuharibu hisiamoyo zako zaidi ya mwili wako. Huenda kinywaji kikaongeza uhakika wako kwa muda. Lakini uhakika unaopata ni wa bandia—na kileo wakati wote huisha mwilini. Wakati uo huo, unarudisha nyuma ukuzi wako wa kihisiamoyo na kiakili. Badala ya kulevuka na kukabili mambo hakika, unazidi kunywa kileo. Peter mwenye miaka 18 asema hivi baada ya kuepuka kileo kwa miezi 11: “Ninalazimika kujifunza jinsi ya kukabili hisi zangu na kutafuta njia mpya za kuwezana na hali zile ambazo kileo kilinisaidia kukabili hapo mbeleni. Ninafikiri kwamba kihisiamoyo na kijamii nina umri wa miaka kumi na mitatu hivi.”
Kisha kuna hatari za kunywa na kuendesha gari. Vifo vya barabarani vinavyotokana na kileo ndivyo namba moja katika kuua vijana katika United States. Unywaji pia hushirikishwa na uuaji, ujiuaji, na kufa maji—visababishi vingine vya vifo kwa vijana.
Isitoshe, utumizi mbaya wa kileo waweza kuwa na matokeo mabaya sana kwa maisha yako ya familia, marafiki, masomo ya shule, na hali ya kiroho. Hivi ndivyo Biblia inavyosema: “Nionyeshe mtu anayekunywa sana, . . . na nitakuonyesha mtu mwenye huzuni na majisikitikio, nyakati zote akizusha matatizo na manung’uniko. Macho yake ni mekundu, na ana machubuko ambayo angaliweza kuyaepuka. . . . Utahisi kana kwamba umo baharini, mgonjwa, ukibembea juu kwenye mlingoti wa meli inayosukasuka.” (Mithali 23:29-34, Today’s English Version) Huo ndio upande wa unywaji ambao hauonyeshwi kamwe kwenye matangazo yanayovutia ya TV.
Mbona Uanze Kunywa?
Kwa hiyo nchi nyingi huzuia vijana wasinywe kileo. Ikiwa wewe ni Mkristo, una sababu yenye kushurutisha ya kutii sheria hizo, kwa kuwa Mungu akuamuru ‘utii mamlaka zilizo kuu.’ (Warumi 13:1, 2) Hata ikiwa utumizi wa kileo miongoni mwa vijana ni halali kwa sababu ya utamaduni wa mahali, je kweli ni kwa faida yako kuanza kunywa wakati huu wa maisha yako? Kama vile 1 Wakorintho 6:12 isemavyo, “vitu vyote ni halali . . . lakini si vyote vifaavyo.” Je! kwa kweli uko tayari kunywa kileo kwa njia ya ukomavu?
Ni kweli, marika wanapokupa divai baridi inayovutia, huenda ikashawishi kuionja. Hata hivyo, ng’amua kwamba unapewa dawa ya kulevya inayoweza kukufanya uwe mzoevu. Vijana wenye kumhofu Mungu katika nyakati za Biblia, kama vile Danieli, Shadraki, Meshaki, na Abednego, walikuwa na ujasiri wa kubaki imara dhidi ya mamlaka ya Kibabuloni na kukataa kujichafua kwa vyakula na divai waliyopewa na mfalme mpagani wa Babuloni. Wewe pia waweza kuwa na ujasiri wa kusema la!—Danieli 1:3-17.
Utakuja kuwa mkubwa vya kutosha—kisheria, kiakili, kihisiamoyo, na kimwili—kunywa kileo ikiwa huo ndio uchaguzi wako. Hata iwe ni hivyo, utakuwa mwenye hekima kuwa na kiasi na kuepuka kuwa mzoevu. Vijana wengi tayari wamekuwa wazoevu, na makala ya wakati ujao itazungumza juu ya yale wanayoweza kufanya ili kushinda uzoevu.
[Maelezo ya Chini]
a Katika tamaduni nyinginezo, kwa kawaida vijana huruhusiwa kunywa vileo pamoja na chakula. Hata hali iwe hivyo, wazazi watakuwa wenye hekima kufikiri kwa uzito yale yanayofaa zaidi watoto wao na wasiruhusu desturi zinazopendwa na wengi ziongoze maamuzi yao yote.
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
TANGU ULIPOANZA KUNYWA:
◻ Je! una marafiki tofauti au wachache zaidi?
◻ Je! maisha nyumbani ni magumu zaidi?
◻ Je! unaona vigumu kulala, au unahisi umeshuka moyo au mwenye wasiwasi?
◻ Je! unahitaji kileo ili uhisi umestarehe miongoni mwa wengine?
◻ Je! unakosa furaha au kutamauka baada ya kunywa?
◻ Je! wewe hudanganya au kuficha kwamba unakunywa?
◻ Je! wewe huona aibu au kukasirika mtu anapozungumza juu ya tabia yako ya unywaji?
◻ Je! mtu yeyote amepata kukushauri au kufanya ucheshi kuhusu utumizi wako wa kileo?
◻ Je! unaamini kwamba divai baridi au pombe ni SAWA kwako kunywa kwa sababu hizo si pombe kali?
◻ Je! umeacha kupendezwa na au kuacha kazi za kujipendeza na michezo uliyofurahia hapo mbeleni?
Ikiwa umejibu ndiyo kwa zaidi ya maswali mawili, huenda ikaonyesha kwamba una tatizo kubwa la unywaji. Ikiwa ndivyo, ungekuwa mwenye hekima kutafuta msaada mara hiyo.
Chanzo: HOSPITALI YA REGENT, New York, NY.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Walevi wengi walisitawisha matatizo ya unywaji katika umri wa mapemay