Je! Mtoto Wako Ataka Mnyama-Rafiki?
WATOTO katika sehemu zote za ulimwengu wanavutiwa na wanyama-rafiki. Nao ni unamna-namna mwingi kama nini wa wanyama walio nao ambao kutokana nao waweza kuchagua! Kwa mfano, Tabitha wa miaka kumi na mitatu, hufuga panya wa kufugwa akiwa mnyama-rafiki wake. Naomi wa miaka mitano hufuga panya mweupe. Na Bobby-John wa miaka kumi na mitano kwa sasa hufurahia kuwa na kitoto—kitoto kangaruu-jike. “Ana kikapu chake mwenyewe naye hujikunja ndani yacho kama vile angefanya akiwa katika kifuko cha mamake,” aeleza Bobby-John. “Hapendi sana kuchukuliwa, lakini yeye ni maridadi sana.”
Watu wengi walio wazima pia wanapenda sana wanyama-rafiki. Na kufuga na kutumia wanyama wakiwa wanyama-rafiki hurudi nyuma mpaka nyakati za kale. Kwa mfano, Wamisri walifuga paka na manyani wakubwa. Halafu alikuwako yule maliki Mroma aliyekuwa na mnyama-rafiki asiye wa kawaida—simba aliyeitwa Skimitari. Alimpenda sana huyo mnyama-rafiki wake wa jamii ya paka hivi kwamba aliketi mezani pamoja naye na kulala miguuni pa kitanda chake usiku. Waroma walizoeza mbwa na masokwe-watu pia. Kitumbuizo kilichopendwa sana kilikuwa kuona masokwe-watu wakipanda juu ya migongo ya mbwa au wakiendesha magari-farasi.
Wakizoezwa ifaavyo na kuongozwa na wazazi wao, watoto wanaweza kujifunza kutunza vizuri wanyama-rafiki wao. Wanaweza kupewa daraka la kuwalisha na kuwatunza. Kuwa na wanyama-rafiki kwaweza pia kuwa jambo lenye kufundisha sana kwa watoto. Kama ionyeshwavyo katika The New Encyclopædia Britannica, “kuweka wanyama-rafiki hutoa fursa ya kufundisha watoto jinsi pendeleo linavyotegemea sana daraka na pia jambo fulani juu ya ngono. Ile njia ya kufanya ngono huonekana upesi, ikifuatwa na mambo kama vile vipindi vya kuchukua mimba na matatizo mbalimbali yanayohusiana na kuzaa na kutunza watoto.”
Wazazi wametumia wanyama-rafiki kuonyesha watoto wao maoni yafaayo kuelekea vitu vyote vilivyo hai—kwa mfano, kutokuwa wakatili kamwe au kusababisha mnyama-rafiki kuteseka, na kutomwacha kamwe awe na njaa au akae akiwa mchafu. Hapa, pia, pana njia yenye kutumika ya kuonyesha watoto hekima na ustadi mwingi wa Muumba wa wanyama, aliyeumba kila mmoja ‘kwa jinsi yake.’—Mwanzo 1:24.
Lakini watoto mara nyingi huchoka na daraka au husahau. Mara nyingi sana idili ya mtoto kwa mnyama-rafiki hutoweka haraka. Upendezi wa juma hili waweza kwa urahisi kuwa uchovu wa juma lijalo. Hivyo, wazazi, ikiwa mnafikiria kumpa mtoto wenu daraka la kuwa na mnyama-rafiki, kumbukeni kwamba ni nyinyi, mlio watu wazima, mtakaolazimika kuchukua daraka la mwisho.
Usafi wa Kiafya Ufaao wahitajiwa Kabisa
Usafi wa kiafya ufaao ni wa maana kwa ajili ya wanyama-rafiki, lakini ni wa maana kadiri hiyohiyo—na labda hata zaidi—kwa watoto wenu. Vyumba vya wanyama-rafiki vyapasa kuwekwa vikiwa safi, na wanyama-rafiki fulani huhitaji kuchanwa manyoya na kuogeshwa kwa ukawaida. Pia yapasa kufikiriwa wanadamu watagusana mwili na wanyama kwa kadiri gani. Kumbuka kwamba ulimi wa wanyama wengi ndio pia kitambaa chao cha kuogea, ambacho hutumiwa kwa sehemu zote za mwili wao. Na ingawa wamepewa uwezo wa kushughulikia vijidudu ambavyo huingia ndani ya miili yao, watoto hawana uwezo huo. Msimtie moyo mtoto wenu ambusu mnyama.
Pia wanyama-rafiki wapaswa kuwa na sahani zao za kulia na hawapasi kuruhusiwa warambe sahani zitumiwazo na wanadamu. Hilo ni jambo la hatari, kwa kuwa wanyama na ndege wana maradhi mengi yawezayo kuambukia wanadamu ikiwa tahadhari za kiakili hazichukuliwi. Na wanyama-rafiki wengi huuma. Ni kweli kwamba baadhi ya maradhi hayo si makali sana na mara nyingi huenda yakapita bila kuhisiwa au huenda chanzo kikaonwa kuwa kingine badala ya mnyama-rafiki. Lakini maradhi fulani ya kupumua na vipele vya ngozi mara nyingi huambukiwa na wanyama-rafiki. Maradhi mengine ni hatari zaidi na yaweza kuua. “Paka wa nyumbani huambukiza akina mama waja-wazito wapatao 3,300 [ugonjwa wa neva uitwao] toksoplasmosisi kila mwaka, hilo likitokeza vifo vya vijusu kwa kiwango cha asilimia 15,” lasema U.S. News & World Report.
Wafundisheni Watoto Kwamba Wanyama-rafiki Si Wanadamu
Kadiri shauku ya watoto kwa ajili ya mnyama-rafiki iongezekavyo, tahadhari yahitaji kuchukuliwa wasipite kiasi na kuanza kumtendea mnyama-rafiki wao kama binadamu mwenzao au kama wana sifa au viwango vya uelewevu kama vya binadamu. Hilo lingetokeza maumivu ya hisia yasiyo ya lazima kabisa mnyama-rafiki azeekapo na kufa au labda akiuawa kwa aksidenti.
Bila shaka, hilo si jambo ambalo ni watoto peke yao hulazimika kufunzwa. Baadhi ya watu wazima pia wahitaji kuwa waangalifu kuhusu jambo hilo. Katika visa fulani mnyama-rafiki huguswa-guswa na kutendewa kana kwamba alikuwa kitoto au mtoto mchanga. Watoto huenda wakaiga kwa haraka mambo waonayo watu wazima wakifanya, wakiwaonyesha wanyama-rafiki shauku nyingi mno.
Kwa hiyo twahitaji kuwa na maoni yaliyosawazika kuhusu wanyama-rafiki na kufundisha watoto wetu kuwa nayo vilevile. Wasaidie kuona kwamba wanyama-rafiki na viumbe vyote vya Mungu vyenye uhai vipo ili kumpendeza na kutumiwa na wanadamu. Lakini lazima tuwe waangalifu tusiwakweze kamwe wanyama na ndege juu ya fungu ambalo Mungu aliwakusudia wawe nalo. Si kusudi la Mungu kwamba wanyama waishi milele. Muda wa maisha yao wenye kikomo haukusababishwa na dhambi ya Adamu na Hawa na kurithi dhambi na kifo, kama ilivyo kwa habari ya wanadamu.—Warumi 5:12; 2 Petro 2:12.
Wanyama-rafiki wawekwapo mahali pawafaapo, wao ni zawadi yenye kupendeza kutoka kwa Mungu kwa ajili ya furaha ya wanadamu. Na si kwa watoto peke yao. Watu wengi wenye umri mkubwa walio wapweke na wagonjwa, wamepata manufaa pamoja na furaha kutoka kwa wanyama-rafiki wao wenye shauku. “Wachunguzi husema kwamba, katika hali fulani, mnyama-rafiki—au, kama vile wengine hupendelea, ‘mnyama mwandamani’—aweza kufanyia maendeleo utendaji wa moyo wa wenye kuwamiliki, aharakishe kupona baada ya kupata maradhi ya moyo, apunguze hangaiko na kushusha msongo wa damu,” laandika jarida AARP News Bulletin.
Kuwa au Kutokuwa na Mnyama-Rafiki?
Basi, wewe utafanya nini mtoto wako akikuomba mnyama-rafiki? Lazima wewe uamue, ukikumbuka manufaa na hasara zote. Mambo kama vile eneo unamoishi, gharama ya utunzaji ufaao na kumlisha mnyama-rafiki, umri wa mtoto wako, na wakati uhitajiwao kusimamia utunzaji ufaao wa mnyama yatahitaji kufikiriwa kwa uangalifu.
Lakini ukiamua kwamba ingemnufaisha mtoto wako kuwa na mnyama-rafiki, kumbuka shauri hilo lililotolewa. Kisha, mkiwa na mnyama-rafiki ndani ya familia, sababu gani msimfurahie kabisa? Mtunzeni vizuri, na kufundisha mtoto wako afanye hivyohivyo. Wakiwekwa mahali pao, wanyama-rafiki ni waandamani wenye kufaa na pia uthibitisho wenye kupendeza wa unamna-namna wenye kupendeza, wa uanzilishi usiokoma wa Muumba mwenye ufikirio.