Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 1/8 kur. 14-17
  • Bara la Barafu na Theluji Sikuzote

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Bara la Barafu na Theluji Sikuzote
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Safari Yetu Kwenda Kisiwa Baffin
  • Mawazo Yasiyo ya Kweli
  • Giza Halikuingia Kamwe
  • Je! Wainuiti Wangetukaribisha?
  • Je, Ndoto ya Kupata Njia ya Kaskazini-Magharibi Imetimia?
    Amkeni!—2003
  • Safari ya Kupendeza Sana Baharini
    Amkeni!—2003
  • Madubwana Wenye Kuvutia wa Kaskazini mwa Kanada
    Amkeni!—1993
  • Kutembelea Mbuga ya Taifa ya Olympic
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 1/8 kur. 14-17

Bara la Barafu na Theluji Sikuzote

SIKUZOTE nimevutiwa na Kaskazini ya mbali. Hata nilipokuwa mvulana mchanga nikikulia Gold Beach, Oregon, U.S.A., nilikuwa nikichunguza ramani za Kanada na kuota kwamba siku moja ningezuru sehemu zenye majina yasiyo ya kawaida, kama vile Ziwa la Great Slave na Ziwa la Great Bear. Kwa hiyo siku moja katika 1987, rafiki yangu aitwaye Wayne nami tulianza kufanya mipango ya kuzuru Mbuga ya Kitaifa ya Auyuittuq, mbuga ya kitaifa ya kwanza ya Kanada kaskazini mwa Kizingo cha Aktiki.

Auyuittuq, katika lugha ya Kiinuiti, yamaanisha “Bara la Barafu na Theluji Sikuzote,” na mbuga hiyo ilitumiwa kuhifadhi nyika ya Aktiki yenye milima iliyo na vilele vichonge, mabonde makubwa, hori zenye kutazamisha, na wanyama wa bahari. Mbuga hiyo yatia ndani mto wa barafu uitwao Penny Ice Cap, ambao ni tandiko kubwa la barafu na theluji la kilometa za mraba 5,700 linaloondolewa maji kwenye kila pande na mito ya barafu. Si ajabu Auyuittuq hurejezewa kwa upendo kuwa “Uswisi ya Aktiki.”

Kisiwa Baffin, chenye urefu wa kilometa 1,600, ndicho kisiwa cha tano kwa ukubwa ulimwenguni. Na bado, hakuna yeyote wa rafiki zetu aliyekuwa amesikia juu yacho! Kwa kweli, wao waliendelea kuuliza, “Waenda lini Alaska?” (Kisiwa Baffin kiko kilometa zipatazo 3,200 mashariki mwa Alaska lakini kiko karibu latitudi ileile.) Ingawa Mashahidi wa Yehova kutoka Kanada wameongoza katika kazi ya kueneza evanjeli katika Kisiwa Baffin, hakuna Mashahidi wanaoishi kwenye kisiwa hicho. Kwa kweli, kutaniko la karibu zaidi liko umbali wa kilometa 1,000, katika Jiji la Labrador, Newfoundland.

Auyuittuq ina miezi mitatu ya kiangazi na miezi tisa ya kipupwe, kwa hiyo tuliamua kwenda Agosti 1988, barafu ya bahari ikiisha vunjika na wadudu wengi wenye kuuma wakiisha toweka. Hii pia ni kabla ya theluji kuanza kunya katika Septemba.

Safari Yetu Kwenda Kisiwa Baffin

Hatimaye wakati ulifika. Tulisafiri kwa gari kutoka nyumbani mwetu katika North Carolina hadi Montreal, Quebec, ambapo tulipanda ndege ya Boeing 737. Baada ya muda wa saa moja hewani, mawingu yalitoweka, tukaweza kuona waziwazi Nyanda ya Kanada, eneo la miambamiamba lionekanalo kuwa tupu lenye mamia ya maziwa yenye sura na ukubwa tofauti-tofauti na bila miti ya ukubwa wowote. Baada ya kusimama muda mfupi katika Kuujjuaq (iliyokuwa Fort-Chimo), tulianza kuona theluji hadi kufikia usawa wa bahari. Halafu kidogo tukapita Ghuba ya Ungava, ambayo, kwa mshangao wetu, ilijaa vilima vya barafu visivyohesabika kwa umbali wa upeo wa macho.

Baada ya safari ya karibu muda wa saa tatu, tulitua katika Iqaluit, unaomaanisha “Mahali pa Samaki.” Iqaluit ulioitwa Ghuba ya Frobisher, ni kitovu cha Kisiwa Baffin na ndio mji mkubwa zaidi, wenye idadi ya watu karibu 3,000.

Tukiwa na muda wa saa chache kati ya safari za ndege, tuliamua kuzuru mji huo. Jambo la kwanza tuliloona ni wingi wa nyasi-pamba, yenye maua yayo meupe yaliyofurafura, ambayo Wainuiti (walioitwa Waeskimo) huchuna na kukausha na kutumia kama mipira ya pamba. Tulipokuwa tukitembea kuelekea bandari na hadi kufikia kwenye ukingo wa maji, tuliona kwamba maji yalikuwa yakipwa upesi. Katika muda wa dakika mbili, meta sita za ufuko wa bahari zilionekana, zikiwa kavu kabisa!

Muda mfupi baadaye, tulipanda ndege ndogo iendeshwayo kwa vijembe ili kwenda hadi Pangnirtung, ulio chini tu ya Kizingo cha Aktiki. Safari hiyo ya saa moja ilitupa maono ya kimbele ya mambo ya kuvutia yaliyoko mbele. Kupitia mawingu meusi ya hapa na pale, tulikuwa tukiona kidogo nyika halisi yenye mweneo mkubwa wa theluji, miamba, na maji. Kila kitu kilionekana kuwa baridi na kisichopendeza. Na hata tulipokaribia “Pang” (jina lililopewa Pangnirtung) hatimaye, tuliona vivyo hivyo. Chini ya dari la mawingu meusi, ndege ilizunguka juu ya hori ndefu iliyozungukwa na majabali ya milima yaliyofunikwa kwa theluji kabla ya kutua chini kwenye uwanja wa changarawe.

Mawazo Yasiyo ya Kweli

Kulikuwa kukinyesha katika “Pang,” kwa hiyo tulijibanza chini ya ubawa wa ndege hiyo, tukingojea mifuko yetu yenye chakula chetu chote na vitu na mkoba uliojaa fasihi ya Biblia. Sehemu ya shehena ilipopakuliwa, vitu vyetu havikupatikana. Katika jengo dogo la uwanja huo, tuliambiwa kwamba labda vingekuja kwa ndege ambayo ingefuata, ambayo ingewasili katika muda wa saa mbili. Angalau tulikuwa na hema yetu, kwa hiyo tulianza kutembea ili kupata mahali pa kupiga kambi ili tupige hema yetu. Tulijibanza mvua katika duka dogo karibu na sehemu hiyo na tukazungumza na msichana aliyeuza katika duka hilo juu ya mji huo na watu wa mji.

Yeye alifanya baadhi ya mambo tuliyowaza kimakosa yawe wazi. Kwanza, kwa sababu mji huo ulikuwa na idadi ya watu wapatao elfu moja, tulikadiria kwamba kwapaswa kuwa na nyumba zaidi ya 300. Kwa kweli, kuna nyumba karibu 180 tu. Ugavi mwingi huja kwa ndege, sivyo? La. Huo huja kwa meli, mara moja kwa mwaka. Hasa meli nne huja. Moja kwa ajili ya Kampuni ya Hudson Bay, duka la rejareja la North; moja ikiwa na vifaa vya ujenzi; moja ikiwa na mafuta na petroli; na moja ikiwa na bidhaa kwa ajili ya maduka yale mengine, kutia na chakula chote cha mkebe cha mwaka mzima. Bila shaka, vitu vinavyoharibika upesi huja kwa ndege.

Giza Halikuingia Kamwe

Baada ya mzigo wetu kufika hatimaye, tulipiga kambi na kutayarisha chakula cha jioni, yote hayo katika mvua. Mtembezi wetu wa safari alituambia kwamba alikuwa amekuwa huko kwa miezi mitatu na alikuwa ameona siku tisa zenye jua! Kulikuwa joto kuliko ilivyotazamiwa—karibu Sentigredi 10, mchana na usiku.

Hata hivyo, giza halikuingia kamwe; mwangaza wa mchana uliendelea wakati wote tuliokuwa huko. Tulipata kwamba tungeweza kupiga picha kwa nuru ya asili saa saba za usiku. Lakini tungeweza kulalaje ikiwa sikuzote kulikuwako nuru? Kulikuwa baridi vya kutosha kuvaa kofia za sufi, hata kulala tukiwa tumezivaa; kwa hiyo baada ya kuzima taa, tulifunika tu macho yetu kwa kofia.

Usiku mmoja saa tisa, niliamshwa na mwangaza mwingi uliotoka kaskazini. Nilitatanika. Katika Kizio cha Kaskazini, jua huchomoza upande wa mashariki, huwa kusini saa sita, na hutua upande wa magharibi, lakini halionekani upande wa kaskazini kamwe. Halafu nikang’amua tulikuwa kwenye sehemu ya juu ya ulimwengu, na katika kiangazi katikati ya usiku, kwa kweli jua huangaza kutoka kaskazini. Ilichukua muda kuzoeleana na hilo.

Je! Wainuiti Wangetukaribisha?

Karibu nyumba zote katika Pangnirtung zimefungwa chini ardhini kwa kamba nzito kwa ajili ya usalama wakati wa upepo mkali. Familia nyingi zina magari ya theluji kwa ajili ya usafiri wakati wa kipupwe na magari yenye miguu mitatu au minne ya mahali popote katika kiangazi. Na kuna motokaa chache, hata ingawa mji huo una karibu kilometa tatu tu za barabara! Kwa kuwa mji huo umo katika sehemu ndogo iliyo tambarare kando ya hori na imezungukwa na miamba mirefu ya milima, hakuna mahali penginepo pa kuendesha motokaa.

Sehemu kubwa ya chakula cha kila familia hupatikana kwa kuwinda mnyama karibou wa sehemu kame na mnyama sili, pamoja na kuvua tirouti wa aktiki. Katika Iqaluit tulijaribu kitumbua cha karibou, kitumbua cha maski, na hata muktuki kidogo, au ngozi ya nyangumi, mafuta yake yakiwamo. Tofauti na mafuta ya nyama ya ng’ombe, mafuta ya nyangumi hayana ladha ya mafuta-mafuta, hata yakiwa baridi, na tuliambiwa kuwa yana protini fulani.

Katika mji wote, tulipata watu wachache tu waliokuwa wamepata kusikia juu ya Mashahidi wa Yehova, nao hawakuwa wenyeji. Walikuwa wamehamia huko kutoka sehemu nyinginezo. Hivyo, swali kubwa akilini mwetu lilikuwa, Watu hawa wa kaskazini wangeitikiaje ujumbe wa Ufalme? Haikuchukua muda mrefu kujua jibu. Karibu kila mtu tuliyekutana naye alikubali fasihi ya Biblia. Kwa kweli, kila siku nilizuru nyumba 45, na kila siku ni watu watatu tu waliosema, “Sipendezwi.”

Tulipoanza kubisha milango siku ya kwanza, kijana mmoja alitupita upesi akaingia hadi ndani ya nyumba tuliyokuwa tukizuru na kusema: “Msibishe mlango. Ingieni tu ndani. Hivyo ndivyo kila mtu hufanya hapa.” Kwa hiyo tulifuata shauri la kijana huyo, tukifungua mlango wa nje kwa haya-haya, tukiingia ndani hadi kwenye mlango wa pili, ambao kwa kawaida ulikuwa wazi, na kuwaita watu waliokuwa ndani. Mwanzoni, wakazi ambao karibu wote walikuwa Wainuiti walitushuku. Lakini kwa kutabasamu kwa njia ya urafiki, kwa kujitambulisha wenyewe mara hiyo, na kuonyesha vielezi vizuri katika Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia, upesi tuliondoa hofu yao na kuamsha kupendezwa kwao. Kuwaonyesha picha ya mtoto akicheza na simba na kusema juu ya siku ambayo hata dububarafu angefugwa na kuwa mwenye kuamanika na chakula hakingekuwa ghali sana kuliwavutia.

Baada ya kuzuru nyumba zote katika kijiji hicho, tulitumia siku sita tukibeba vitu vyetu kwa mfuko katika Mbuga ya Kitaifa ya Auyuittuq, bara la ajabu la theluji, barafu, mito ya barafu, vilele vya miamba-miamba, na maporomoko ya maji.

Ndege yetu iliporuka kutoka Pangnirtung na kuzunguka kusini juu ya hori, tulimshukuru Yehova Mungu kwa fursa ya kuzuru eneo hilo la mbali. Hata kufikia siku hii, mara nyingi sisi hufikiri juu ya Wainuiti hao wenye urafiki ambao waliitikia sana kweli ya Biblia, katika bara la barafu na theluji sikuzote.—Imechangwa.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nyasi-Pamba. Kilele Thor, Kisiwa Baffin, katika mandhari-nyuma hupanda meta 1,500 kutoka chini ya bonde

Mbali kulia: Mahali imara pa kutembelea pahitajiwa ili kuvuka mto wenye barafu

Mbali kulia chini: Mashua zilizopwelea kwenye maji kupwa katika Pangnirtung

Kulia: Msichana Mwinuiti ashikilia kitabu chake chenye thamani cha “Hadhithi za Biblia”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki