“Barabara Isongayo” ya Kanada Yenye Kuvutia
NA MLETA HABARI ZA AMKENI! KATIKA KANADA
“Huu ni mto gani?” “Ni mto usio na mwisho,” kiongozi mwenyeji akajibu
ULIKUWA mwaka wa 1535.[2] Yule mvumbuzi, Jacques Cartier, mwenye kuuliza maswali hakujua kwamba ule mto ambao alitaka kuandika habari zao siku moja ungekuja kuwa mmoja wa mito muhimu zaidi katika Amerika Kaskazini. Mto huo ukaja kuwa “barabara” pana kwa wafanyabiashara ya manyoya ya wanyama na wakoloni na hatimaye kuwa njia ya meli-shehena za kisasa za baharini.[3] Mto huo una upana unaopita kilometa 130 kwenye mlango wao na una urefu wa kilometa zipatazo 1,200 kuingia barani ukitoka Bahari ya Atlantiki hadi Ziwa Ontario.[4]
Vitabu vya historia vyamsifu Cartier kuwa ndiye aliyeuita mto huo wenye fahari St. Lawrence. Hatimaye, jina hilo lilitumiwa kuutaja mto wenyewe na ghuba iliyoko kwenye mlango wao.[5]
Baadhi ya mandhari nzuri sana za Amerika Kaskazini zapatikana kandokando ya Mto St. Lawrence. Magenge ya majabali na mabonde ya mawe huteremka mpaka majini na kutengeneza mojapo mabonde yenye kuinuka yaliyo marefu zaidi ulimwenguni, lile Bonde la Saguenay, lenye umbali wa kilometa 100 hivi.[6] Ule Mto Saguenay ulio mkubwa sana hujiunga na St. Lawrence kutoka kaskazini na kutokeza hori ambapo maji ya bahari yachangamana na mtiririko wa mto.
Wanabiolojia wa majini wasema kwamba hapo ndipo malimwengu mawili yakutana chini ya maji.[7] Maji baridi ya bahari yenye chumvi huingia kupitia mifereji ya chini ya bahari yenye vina vipatavyo meta 400,[8] kisha maji hayo huinuka na kuchangamana na maji yasiyo na chumvi kutoka kwenye mito. Kuna viumbe vingi vya bahari katika hori hiyo. Kuna beluga (nyangumi wadogo weupe), nyangumi-minke, nyangumi-pezi, na madubwana wa nyangumi-buluu wakiwa pamoja.[10] Kwa kawaida aina hizo nne za nyangumi huishi umbali wa mamia ya kilometa kutoka kwa mwingine. Si ajabu kwamba watalii 70,000 walifunga safari za mashua kutazama nyangumi katika St. Lawrence katika mwaka mmoja wa karibuni.[11]
Ule mchanganyiko wa mimea, wanyama, na ndege kandokando za mto ni mojapo hali zisizo kawaida zaidi kuonwa duniani. Kuna mamia ya aina za samaki, zaidi ya aina 20 za wanyama amfibia na reptilia, na aina 12 za wanyama wa baharini. Inasemwa kwamba kuna aina 300 za ndege ambao hupenda sana kuendea mabwawa yao na kingo zao. Ndege wenye kuhama-hama kama vile bata na bata-bukini wa barafu huja kwa maelfu kwenye maji hayo.[12]
Ukipanda mto kidogo, kuna milima mitulivu yenye rangi ya buluu inayoinuka ng’ambo ya fuko zao. Misitu myeusi imejipanga kwenye kingo za mto huo. Visiwa vyenye fahari husimama wima katika mlango-bahari wao ulio mpana. Mashamba, vijiji, na miji iko kwenye fuko zao.[13]
Kutoka barani Montreal, mifululizo ya maporomoko madogo-madogo yakata-kata mto huo kwa kilometa mia moja sitini.[14] Ng’ambo ya maporomoko hayo, kuabiri kwafurahisha zaidi kupitia sehemu ya kilometa 60 yenye maji yaliyo na vile vinavyoitwa Visiwa Elfu Moja (kwa kweli vyakaribia kuwa visiwa elfu mbili).[15]
Usafiri Katika “Barabara” Hiyo
Mapema kama 1680, walowezi Wazungu walikuwa wakisema juu ya kuongeza “barabara” hiyo itumiwe na meli za baharini hata kupita Montreal kwa kutengenezwa kwa mifereji inayopita kando ya yale maporomoko.[16] Ndoto hiyo ilitimizwa karibu miaka 300 baadaye kwa kufunguliwa kwa mto St. Lawrence Seaway mnamo 1959.[17] Njia hiyo yaonwa kuwa mojapo matimizo makuu ya uhandisi ulimwenguni.[18]
Ili kumaliza sehemu hiyo ya mto yenye umbali wa kilometa 293, milango saba mipya ilijengwa kati ya Montreal na Ziwa Ontario. Hilo lilimaanisha kuchimbwa kwa mchanga na miamba ifikayo meta za kyubiki milioni 150 hivi kwamba kama mchanga huo ungejazwa katika uwanja wa mchezo wa mpira, ungefanyiza mlima wenye kimo cha kilometa 35. Kiasi cha zege ambacho kingetumiwa katika kujenga milango hiyo kingeweza kujenga barabara kuu pana ya kutosha magari manne kwenda sambamba inayotoka London hadi Rome.[19]
Jacques LesStrang, mtungaji wa kitabu Seaway—The Untold Story of North America’s Fourth Seacoast, alimnukuu nahodha wa baharini aliyesema hivi: “Hakuna mto mwingine kama huo ulimwenguni pote. Si rahisi kuusafiria, lakini ule utukufu wa mto huo, yale Maporomoko ya Niagara yenye sauti ya kishindo, maziwa mengi na visiwa vingi visivyokwisha hufanya mto huo uvutie sana.”[20]
Meli za bahari zenye kusafiri kupitia ile “barabara” iliyoongezwa hadi Duluth na Superior katika upande wa United States wa Ziwa Superior hupanda kama kupanda orofa kufikia meta 180 juu ya usawa wa bahari, ambacho ni kimo cha jengo refu lenye orofa 60. Jumla ya umbali wa safari yote kuingia bara ni kilometa 3,700 kutoka Bahari ya Atlantiki.[21]
Usafiri kama huo umeleta ufanisi wa kibiashara kwa majiji yaliyoko kandokando za mto huo. Kitabu The Great Lakes/St. Lawrence System chaeleza hivi: “Ndani ya mipaka yao ya mataifa mawili mna kitovu cha viwanda vya Kanada na United States, mna msongamano wa watu wapitao milioni 100 na chanzo kimoja kikubwa zaidi cha utajiri wa kiviwanda na utengenezaji wa bidhaa katika ulimwengu wa magharibi.”
Miongoni mwa bandari zaidi ya 150 zilizoko kandokando za mto huo kutoka Bahari ya Atlantiki hadi Ziwa Superior ni (katika Kanada) Jiji la Quebec, Montreal, Toronto, Hamilton, Sault Sainte Marie, na Thunder Bay na (katika United States) Buffalo, Erie, Cleveland, Detroit, Chicago, Duluth na Superior.[22] Meli kutoka Casablanca, Le Havre, Rotterdam, na sehemu nyinginezo husafirisha mamilioni ya tani za mizigo kwenye St. Lawrence kila mwaka.[23] Matumizi ya “barabara” hiyo hutokeza makumi ya maelfu ya kazi za kufanya na mapato ya mabilioni ya dola kila mwaka.[24]
Vilio vya Kutahadharisha
Hata hivyo, baada ya miaka zaidi ya 30 ya kuabiri kwenye “barabara” hii, vilio vya kutahadharisha vimesikika. Kwa karne kadhaa Mto St. Lawrence pamoja na akiba yao ya yale Maziwa Makuu “umetumiwa kuwa sehemu ya kutupia uchafu wa choo na takataka,” lakazia Shirika la Mazingira la Kanada.[25] Huo “Mto Mkuu” ungeweza kushughulikia takataka hizo vizuri hadi hivi karibuni.
Meli kubwa za bahari zimemwaga mawe zayo katika maziwa yenye maji yasiyo na chumvi na kwenye mto huo.[26] Viwanda na majiji yaliyoko kandokando yamemwaga kemikali zenye sumu kwenye mto huo. Ukulima umechangia kumwagika ndani ya huo mto dawa fulani za kuua wadudu. Matokeo ya hayo yote yamehatarisha mto huo.[27]
Kadiri vichafuzi vilivyozidi kumwagwa ndani ya huo mto, aina za samaki nazo zikapotea polepole. Baada ya muda kuogelea kulikatazwa. Kisha marufuku ikapigwa juu ya kula samaki wa aina fulani na kamba wa baharini.[28] Kunywa maji ya mfereji yaliyotoka kwenye mto huo kukaanza kutiliwa shaka.[29] Aina fulani za wanyama wa pori zikatangazwa rasmi kuwa zaelekea kuangamizwa. Beluga waliokufa waliletwa na maji ufuoni, wakifa kutokana na magonjwa yaliyotokezwa na sumu zilizokuwa majini.[30]
Kuisafisha ile “Barabara”
Mto huo ulikuwa ukitoa ujumbe wa wazi. Ile “barabara isongayo” yenye kuvutia sana ilihitaji kurekebishwa. Kwa hiyo katika 1988 serikali ya Kanada iliitikia kwa kuanzisha mpango maalumu ulioitwa Mpango wa Kuokoa St. Lawrence uliokusudiwa kusafisha huo mto kukiwa na programu ya kuuhifadhi, kuulinda, na kuurudisha kwa hali ya zamani, hasa kutoka Montreal hadi Bahari ya Atlantiki.
Kuna mipango inayoendelea sasa ya kushughulikia viumbe wanaoelekea kuangamizwa. Maeneo ya hifadhi yanaanzishwa yahifadhi viumbe wale wanaobaki. Ile Hifadhi ya Viumbe vya Baharini ya Saguenay iliyo mpya, iliyoko mahali Mto Saguenay ukutanapo na St. Lawrence, ulianzishwa kuhifadhi mazingira makubwa na makao ya viumbe vya baharini.
Sheria mpya ziliwekwa. Viwanda viliwekewa tarehe za mwisho za kupunguza vichafuzi vya mto kwa asilimia 90. Mbinu mpya zinatokezwa ili kupunguza uchafuzi.[31] Sehemu zilizochafuliwa na sumu zilizoachwa na mto au kutokana na takataka zilizo chini ya maji. Katika maeneo fulani mazingira mapya ya viumbe yataanzishwa kandokando ya fuko za mto kwa kutumia takataka za mto zilizotolewa sumu.[32] Hatua zinachukuliwa ili kudhibiti idadi na miendo ya maelfu ya watalii ambao huja kuona mto huo kila mwaka.[33]
Uharibifu huo waweza kurekebishwa. Jambo moja ni kwamba, tofauti na barabara zenye kutengenezwa na binadamu, mto huo utajirekebisha wenyewe watu wakiacha kuuchafua. Uhitaji mkubwa zaidi ni kubadili mtazamo wa wenye viwanda na watu wa kawaida wenye kutumia vitu vilivyotengenezwa, wote ambao hufaidika na biashara inayofanywa kandokando za mto huo na yale Maziwa Makuu.
Ishara moja ya kuonyesha mafanikio katika kurekebisha hali hiyo mbaya ni nyangumi-beluga. Ingawa bado waelekea kuangamizwa, beluga wanaongezeka sana baada ya kupungua kutoka kuwa 5,000 hadi karibu 500.[34]
Umma umejulishwa juu ya uharibifu ambao umefanywa kwa utajiri wa asili wa mto huo na utukufu wao uliopita. Je! kufahamu jambo hilo kutasaidia jitihada za wakati ujao za kuurudisha mto huo kwenye hali yao ya zamani? Kutasaidia, wakati viumbe vya kibinadamu vitakapostahi na kuthamini viumbe vya Mungu.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]
Kwa hisani ya The St. Lawrence Seaway Authority