Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/8 kur. 26-28
  • Ndizi—Tunda la Ajabu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ndizi—Tunda la Ajabu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mashamba ya Ndizi
  • Jinsi Mgomba Unavyokua
  • Kutoka Shambani Hadi Meza Yako
  • Manufaa Halisi na Lishe
  • Kutembelea Shamba la Migomba
    Amkeni!—2003
  • Tunda la Kimataifa Lenye Kupendeza Mno
    Amkeni!—1995
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2003
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/8 kur. 26-28

Ndizi—Tunda la Ajabu

NA MLETA HABARI ZA AMKENI! KATIKA HONDURAS

WAGIRIKI na Waarabu waliuita “mgomba wa ajabu.”[1] Ilipatikana mwaka 327 K.W.K. katika India na majeshi ya Aleksanda Mkuu. Kulingana na hadithi moja ya kale, wahenga wa India walipumzika kwenye kivuli cha mgomba na kula matunda yao. Kwa hiyo limeitwa “tunda la watu wenye hekima.”[2] Hilo ni tunda gani? Kumbe, ni ndizi!

Lakini ndizi ilitokaje Asia na kwenda Karibea? Naam, wafanya biashara Waarabu walibeba mizizi ya mgomba kutoka Asia hadi pwani ya mashariki ya Afrika. Katika 1482, wavumbuzi Wareno waligundua migomba iliyokuwa ikimea huko na kuchukua baadhi ya mashina yenye mizizi pamoja na jina la Kiafrika banana (ndizi), hadi kwenye koloni za Wareno katika Visiwa vya Canary. Hatua iliyofuata ilikuwa ni safari ya kuvuka Bahari ya Atlantiki hadi zile zilizoitwa Nchi Mpya. Hiyo ilitendeka mwaka wa 1516, miaka michache baada ya safari za Columbus. Wamishonari kutoka Hispania walipeleka migomba kwenye visiwa na bara la kitropiki la Karibea.[2] Hivyo, ilibidi mgomba huo wa ajabu usafiri nusu ya ulimwengu ili kufika Amerika ya Kati na Kusini.

Inaripotiwa kwamba mnamo 1690 ndizi ilipelekwa New England mara ya kwanza zikitoka Visiwa vya Karibea. Wanadini wa Puriti walichemsha tunda hilo la kigeni na hawakulipenda.[3] Lakini, katika nchi za Amerika Kusini na ya Kati, na vilevile nchi nyinginezo za kitropiki, mamilioni ya watu huchemsha ndizi mbichi yenye rangi ya kijani na kuzila kwa furaha.

Mashamba ya Ndizi

Kati ya 1870 na 1880, wafanya biashara kadhaa kutoka Ulaya na Amerika Kaskazini walianza kutafuta uwezekano wa kusafirisha ndizi nchi za nje. Walianzisha makampuni na mashamba ya ndizi, yaliyoitwa finka. Kwa sababu hiyo, ilibidi wafanyakazi na wahandisi kukata misitu, kutengeneza barabara, na kujenga reli na mifumo ya mawasiliano. Vijiji vilijengwa vikiwa na nyumba, shule, na hata hospitali kwa ajili ya wafanyakazi na familia zao. Makampuni ya meli yalianzishwa ili kusafirisha ndizi ulimwenguni pote.[4] Biashara hiyo ilipoendelea, makampuni yalinunua ardhi zaidi katika nchi zilizokuwa zikikuza ndizi.

Leo hii, nchi za Amerika ya Latini zinakuza zaidi ya asilimia 90 za ndizi zinazoliwa katika Amerika Kaskazini. Brazili ndiyo inayoongoza katika kusafirisha ndizi nje.[5] Honduras ni namba sita kwenye orodha, ikisafirisha nje ndizi zipatazo kilo bilioni moja kila mwaka.[6]

Jinsi Mgomba Unavyokua

Mgomba si mti. Hauna nyuzi za mbao. Lakini, huo ni mjusi mkubwa wa mti unaofanana na mnazi. Ukuzi na ukubwa wa mgomba hutegemea hali-hewa na mchanga. Migomba hukua vizuri zaidi katika hali-hewa zenye joto na unyevu nayo hufanya vizuri katika aina ya udongo wa tifutifu-kichanga ulio na rutuba na wenye kupitisha maji vizuri.[7] Kwa ukuzi bora, hali-joto haipasi kupungua digrii za Sentigredi 20 wakati wowote ule.[8]

Ili kupanda mgomba, ni lazima upande mashina yaliyokatwa, yanayoitwa miche, ambayo hukatwa kutoka mashina yaliyo chini ya ardhi ya migomba iliyokomaa. Miche huwekwa kwa mashimo ya futi moja kwenda chini na meta 5 kutoka kwa shimo jingine. Kwa majuma matatu hadi manne, matawi ya kijani hutokea, na magomba (majani) yaliyokunjwa kabisa hutokea na kukunjuka kadiri yakuavyo. Migomba hukua haraka sana, karibu sentimeta 3 kila siku. Baada ya miezi kumi, mgomba huwa umekua kabisa na hufanana na mnazi, ukiwa na kimo cha meta 3 hadi 6.[9]

Kwenye mgomba uliokomaa, chipukizi kubwa lenye majani madogo-madogo yenye rangi ya zambarau hukua kutoka kwenye magomba yanayojikunja na kufanyiza bunda. Kisha chane ndogo-ndogo za maua hutokea. Mgomba hutokeza mkungu mmoja wa ndizi, wenye uzito wa kutoka kilo 30 hadi 50 na ambao una chane zipatazo 9 hadi 16 za ndizi. Kila chane, unaoitwa mkono, huwa na ndizi 10 hadi 20. Hivyo, ndizi huitwa vidole.[10]

Kwanza ndizi hukua zikielekea chini, na kisha nje na juu, zikifanyiza upinde ujulikanao sana wa ndizi. Vipi juu ya lishe na ulinzi wakati wa ukuzi? Baada ya muda mfanyakazi huja na kung’oa lile chipukizi ili ndizi ziweze kupokea nishati zote kutoka kwa mgomba. Kisha afunika ndizi na karatasi ya polithini ili kuzuia wadudu. Kwa kuwa migomba hukua ikielekea juu na kuwa mizito sana, mmea huo hufungwa kwenye msingi wa mimea iliyo karibu ili kuzuia upepo au uzito wa mkungu usiuangushe. Hatimaye, kamba yenye rangi hufungwa juu yao ili kuonyesha wakati matunda yatakapokuwa tayari kuvunwa shambani.

Kila siku, ndege hupitia juu ya mashamba ili kunyunyiza dawa kwenye magomba (majani ya mgomba). Jambo hilo hukinza mimea hiyo kutokana na maradhi tatu kuu. Moja ni maradhi ya Panama, yenye ukungu unaoharibu baadhi ya migomba. Lakini migomba hiyo hubadilishwa na aina za migomba inayoweza kukinza maradhi hayo. Maradhi nyingine ni Mako, isababishwayo na bakteria. Hiyo inadhibitiwa kwa kuondoa migomba na maua yoyote yanayovutia wadudu fulani wenye kueneza maradhi hayo. Kisha kuna maradhi ya Sigatoka, yanayoharibu majani ya mgomba lakini hayaharibu ndizi zenyewe dawa za kemikali za kunyunyiza zikitumiwa haraka iwezekanavyo.[11] Ndizi huhitaji maji mengi sana, yanayoandaliwa na mifumo ya kunywesha maji na ya kunyunyiza maji kwa msongo mkubwa. Twaweza kuongezea kwamba nyasi na magugu huondolewa kwenye shamba.

Kutoka Shambani Hadi Meza Yako

Katika wakati ambapo rangi ya kamba inaonyesha kwamba ndizi ziko tayari kuvunwa, kwanza zinapimwa ili kuhakikisha kwamba ni kubwa vya kutosha kuweza kukatwa. Jambo jingine kuu ni kwamba ndizi haziachwi ziwe mbivu zikiwa kwenye mgomba, hata zile zitakazoliwa. Kwa nini? Kwa sababu zitapoteza ladha. Kabla ya kuamua wakati wa kuzivuna, ni lazima umbali wa sehemu zinazosafirishwa na aina ya usafiri ufikiriwe. Mfanyakazi hukata mkungu kwa upanga wake, na kisha unapelekwa kwenye kituo cha kupakia ndizi. Na mgomba hufanywaje baada ya mavuno? Huo hukatwa ili uwe rutuba kwa mimea mipya itakayochukua mahali pao.

Ndizi huoshwa katika kituo cha kuzipakia, na ndizi zenye makovu huondolewa, nazo zitaliwa na wafanyakazi na familia zao. Ndizi changa hutumiwa zikiwa vikolezo na kuwa chakula cha watoto. Ndizi bora zaidi hupakiwa katika sanduku zikiwa na kilo 18 na kupelekwa nchi za nje kwa magari-moshi na meli zilizo na friji.

Ubora wa ndizi huchunguzwa bandarini, na hali-joto yayo hupimwa. Baada ya kukatwa, ni lazima tunda hilo libaki likiwa kijani mpaka lifike kwenye soko. Kwa kuwa ndizi huharibika haraka, ni lazima ivunwe, isafirishwe, na kuuzwa kwa siku 10 hadi 20. Tunda hilo huwekwa likiwa baridi kwa hali-joto ya digrii za Sentigredi 12 hadi 13 ili lisiwe mbivu.[12] Kukiwa na njia za kisasa za usafirishaji, ndizi zaweza kupelekwa kutoka Amerika ya Kati na Kusini hadi mbali kufikia Kanada na Ulaya bila matatizo.

Manufaa Halisi na Lishe

Kuna aina mia moja au zaidi za ndizi. Ndizi-mbilikimo ndiyo aina ya kawaida, ambayo husafirishwa hasa Ulaya, Kanada, na United States. Aina nyingine ndogo-ndogo, zenye maganda membamba sana hivi kwamba haziwezi kusafirishwa, zapatikana kwa wingi katika Honduras. Hizo huitwa manzana (Tofaa) na Jamaika-Jekundu.[13]

Magomba ya mgomba yana nyuzi zenye mafaa zinazotumiwa kwa kazi mbalimbali katika nchi za kitropiki. Ukienda soko la wazi, utaona magomba hayo yamerundikwa barabarani yakiuzwa kwa ajili ya kufungia tamale moto, ambayo hupendwa sana katika nchi nyingi.

Watu wengi katika Honduras hupenda kula ndizi katika milo yao. Chakula kitamu katika pwani ya kaskazini ya Honduras inaitwa machuca. Ili kukitayarisha, ndizi mbichi inasagwa kwa kinu, vikolezo vyaongezwa, na mchanganyiko unapikwa na kaa katika mafuta ya nazi.

Katika United States, karibu ndizi bilioni 11 huliwa kila mwaka. Kiasi kikubwa husafirishwa Kanada na Uingereza na nchi nyinginezo za Ulaya. Kuna mafaa gani ya lishe yanayopatikana kwa kula tunda hilo? Ndizi zina vitamini A na C, kabohidrate, fosforasi, na potasiamu nyingi sana.[14]

Ndizi hutumiwa kwa njia nyingi sana! Inafaa kwa kumbwe, nafaka, mchanganyiko wa matunda, pai, na bila shaka kwa keki. Lakini wakati mwingine ulapo ndizi mbivu, fikiria juu ya sifa zayo zenye kutokeza sana. Tunda hili lina kifuniko chalo chenyewe. Lina vitamini nyingi na madini mengi. Naam, na huenda ndizi ilitoka nusu ya ulimwengu ili iweze kufikia meza yako.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki